DOMINIKA YA 2 MAJILIO

MASOMO MWAKA A

ANTIFONA YA KUINGIA: Isa.30:19,30
Enyi watu wa Sayuni, tazameni Bwana atakuja kuwaokoa mataifa; naye Bwana atawasikizisha sauti yake ya utukufu katika furaha ya mioyo yenu.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi na mwenye rehema, utujalie ili shughuli zozote za kidunia zisituzuie kufanya hima kumlaki Mwanao, bali mafundisho ya hekima ya mbinguni yatufanye tuwe washirika wake. Anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa.11:1-10
Siku ile: litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho wa Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia. Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwanakondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono Watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao Watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika tundu la fira. Hawatadhuru wala pango hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari. Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzika patakuwa na utukufu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.72:1-2,7-8,12-13,17(K)7
1. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.

(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.

2. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka Mto hata miisho ya dunia. (K)

3. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K).

4. Jina lake na lidumu milele,
Pindi ling'aapo jua jina lake liwe na wazao;
Mataifa yote na wajibariki katika yeye,
Na kumwita heri. (K)

SOMO 2: Rum.15:4-9
Ndugu zangu, yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini. Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunia mamoja ninyi kwa ninyi kwa mfano wa Kristo Yesu; ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe. Kwa maana nasema, ya kwamba Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa baba zetu; tena ili Mataifa wamtukuze Mungu kwa ajili ya rehema zake; kama ilivyoandikwa, Kwa hiyo nitakushukuru kati ya Mataifa, nami nitaliimbia jina lako.

SHANGILIO: Lk.3:4,6
Aleluya, aleluya!
Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake, Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu,
Aleluya!

SOMO 3: INJILI: Mt.3:1-12
Siku zile aliondokea Yohane Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Uyahudi, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Kwa sababu huyo ndiye aliyenenwa na Nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Naye Yohane mwenyewe alikuwa na vazi lake la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake; na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani; naye akawabatiza katika mto wa Yordani, huku wakiziungama dhambi zao. Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia Ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto. Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Yohane Mbatizaji ni sauti ya nabii aliaye nyikani. Sauti yake ilitaka kuwaita watu wamwongokee Mungu, Mkombozi wao. Ee Mungu Mwenyezi,

1. Utuzibue masikio yetu tupate kusikia sauti za maskini wanaolilia msaada.

2. Uwasaidie waandishi na watangazaji wa habari waseme ukweli na kuzingatia maadili ya kazi yao.

3. Uwahamasishe viongozi wa serikali wasiwatumainishe raia mambo kwa ahadi hewa, bali wahakikishe kuwa ukweli na uwazi unatekelezwa.

4. Utuamshe sisi tupokee ukweli wa Enjili kwa moyo wa furaha na kuutekeleza katika maisha yetu ya kila siku.

5. Uwakaribishe mbinguni waumini marehemu waliofuata sauti yako katika maisha yao ya hapa duniani.

Ee Baba mwema, usikilize maombi yetu kwa jina la Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba sala na dhabihu zetu sisi wanyonge zikutulize; na kwa kuwa mastahili yetu hayatoshi kitu, ututie shime kwa rehema yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

1. UTANGULIZI WA MAJILIO:
MAJILIO I:

K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye, katika ujio wake wa kwanza, alipokuja katika unyenyekevu wa mwili, aliutimiza mpango ulioandaliwa nawe tangu kale. Hivyo, akatufungulia njia ya wokovu wa milele, ili, atakapokuja tena katika utukufu wa enzi yake, hatimaye tupewe waziwazi mema yaliyoahidiwa, ambayo kwa sasa tunathubutu kuyatarajia, tukikesha.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Bar.5:5;4:36
Ondoka, ee Yerusalemu, usimame juu; tazama uione furaha inayokujia kutoka kwa Mungu wako.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kushibishwa kwa chakula cha kiroho, tunakuomba kwa unyenyekevu, ili kwa kushiriki fumbo hili, utufundishe kuyapima kwa hekima malimwengu na kuambatana na mambo ya mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.