DOMINIKA YA 29 YA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.17:6,8
Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, utege sikio lako ulisikie neno langu. Ee Bwana, unilinde
kama mboni ya jicho, unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, utuwezeshe daima kuyafuata mapenzi yako kwa uchaji na kuitumikia
fahari yako kwa moyo mnyofu. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala
nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Kut.17:8-13
Wakati huo Waamaleki walitokea, wakapigana na Israeli huko Refidimu. Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie
watu, ukatoke upigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo ya Mungu nitakuwa
nayo mkononi mwangu. Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na
Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima. Ikawa, Musa alipoinua mkono wake, Israeli walishinda;
na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda. Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; bali wakatwaa
jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na
mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa. Yoshua akawaangamiza Amaleki na
watu wake kwa ukali wa upanga.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.121,(K)2
1. Nitayainua macho yangu niitazame milima;
Msaada wangu utatoka wapi?
Msaada wangu u katika Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi.
(K) Msaada wangu u katika Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi.
2. Asiuache mguu wako usongezwe,
Yeye akulindaye asisinzie.
Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi,
Yeye aliye mlinzi wa Israeli. (K)
3. Bwana ndiye mlinzi wako;
Bwana ni uvuli, husimama mkono wako wa kuume,
Jua halitakupiga mchana,
Wala mwezi wakati wa usiku. (K)
4. Bwana atakulinda na mabaya yote,
Atakulinda nafsi yako.
Bwana atakulinda utokapo na uingiapo,
Tangu sasa na hata milele. (K)
SOMO 2: 2Tim.3:14-4:2
Wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao
ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha
hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa
mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;
ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema. Nakuagiza mbele za Mungu,
na mbele za Kristo Yesu, atakayehukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake;
lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu
wote na mafundisho.
SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya!
Neno lako ndiyo kweli, ee Bwana;
Ututakase sisi kwa ile kweli.
Aleluya!
INJILI: Lk.18:1-8
Yesu aliwaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa. Akasema,
Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na
mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendeaendea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda
alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa
mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema,
Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je, Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia
mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja
Mwana wa Adamu, je, ataiona imani duniani?
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Yesu alitufundisha Baba yetu ili tumwendee Baba na maombi yetu
yote. Tukiwa na njaa, tumwambie; tunapokosa kazi, tumwombe
msaada. Hakuna shida ambazo hatuwezi kumwambia kwani yupo
tayari kutusikiliza kadiri uamuzi wake.
Ee Baba Mungu,
1. Mjane wa Injili hakuacha kumwomba hakimu ampatie
haki yake: Utupe neema ya kudumu katika sala zetu kwa
matumaini ya kusikilizwa kadiri ya uamuzi wako.
2. Utupelekee Roho wako Mtakatifu ili atuongoze katika
maisha yetu ya kila siku.
3. Utusaidie tusisahau kuwaombea wengine wenye shida,
wazazi, jamaa, adui na marafiki.
4. Uwapokee waumini wote marehemu waliokutegemea na
kukutumikia.
Ee Baba wa huruma, njia moja ya kukujia wewe hapa duniani ni
sala na maombi yetu. Tunakuomba uyapokee kwa jina la Kristo
Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utujalie tuweze kukutumikia kwa uhuru wa moyo kwa vipaji vyako. Ututakase
kwa neema yako, na utusafishe kwa mafumbo hayohayo tunayoyaadhimisha. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.33:18-19
Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, wazingojeao fadhili zake. Yeye huwaponya nafsi zao
na mauti, na kuwahuisha wakati wa njaa.
Au:
Mk.10:45
Mwana wa Adamu amekuja apate kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakuomba utujalie ili, kwa njia ya kushiriki mara nyingi mafumbo haya ya mbinguni,
tuweze kupata msaada wa riziki za duniani, na ufahamu wa mema ya milele. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu.