DOMINIKA YA 28 YA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.130:3-4
Bwana, kama wewe ungehesabu maovu, ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, ee Mungu wa Israeli.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Bwana, tunakuomba neema yako itutangulie daima na kutusindikiza, nayo itubidiishe kutenda mema. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: 2Fal.5:14-17
Naamani alishuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli, basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako. Lakini akasema, Kama Bwana aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa. Naamani akasema, Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-4 (K)2
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umetenda wokovu.

(K) Bwana ameufunua wokovu wake
Machoni pa mataifa.

2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

3. Miisho yote ya dunia imeuona;
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote.
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)

SOMO 2: 2Tim.2:8-13
Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo Injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana,
Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia;
kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye;
kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi;
kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa.
Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.

SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, asema Bwana:
Nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya!

INJILI: Lk.17:11-19
Yesu na wanafunzi wake walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajioneshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je, hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako,imani yako imekuokoa.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Tunavipokea vipaji vingi kama vile uhai, afya, familia, jamaa, mavuno na kazi, lakini tunafikiri kwamba tumeyapata hayo yote kama haki yetu. Tunasahau kumshukuru Mungu.

Tumshukuru Mungu,
1. Utupe moyo wa shukrani kwa mema yote tunayopokea kila siku katika maisha yetu.

2. Utusaidie kuwarudisha wengi walioachwa pembeni, katika hali ya kukaa nasi kwa amani.

3. Utukumbushe kwamba imani yetu ina shabaha ya kututayarisha hapa duniani kwa uzima ujao.

4. Uwaponye na kuwafariji wagonjwa wote hasa wale walio katika hali ya kukata tamaa.

5. Utusaidie kuamini kwamba imani yetu ina nguvu ya kubadili hali ya maisha ya dunia iwe nzuri na ya kupendeza kwa wote.

Ee Mungu Mwenyezi, unatujalia mema bila kungojea shukrani zetu. Tunaomba radhi na kukuomba uyapokee maombi yetu kwa jina la Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, upokee sala pamoja na matoleo ya dhabihu ya waamini wako, ili, kwa matendo haya ya ibada, tupate kuufikia utukufu wa mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.34:10
Matajiri hutindikiwa, huona njaa; bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu chochote kilicho chema.

Au:
1Yn.3:2

Bwana atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana mtukufu, tunakuomba kwa unyenyekevu, utushirikishe umungu wako kama unavyotulisha Mwili na Damu takatifu ya Mwanao. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.