DOMINIKA YA 27 YA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Est.4:17b.17c
Ee Bwana, ulimwengu wote u katika uweza wako, wala hakuna awezaye kuyapinga mapenzi yako.
Wewe umeviumba mbingu na nchi, na vitu vyote vya ajabu vilivyopo chini ya mbingu; nawe ndiwe Bwana
wa vyote.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, kwa wingi wa huruma yako watenda mambo ya ajabu sana kuliko
yote tunayostahili na kuyatamani sisi tukuombao. Utushushie rehema yako, utuondolee yale yanayozitia
hofu dhamiri zetu, na kutuongezea yale ambayo hatuthubutu kuomba. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Hab.1:2-3;2:2-4
Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia?
Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa.
Mbona wanionesha uovu, na kunitazamisha ukaidi?
Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea.
Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao,
ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka
ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia; ingojee; kwa kuwa haina budi kuja,
haitakawia. Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa
imani yake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.95:1-2,6-9,(K)7-8
1. Njoni tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele yake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yetu.
2. Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi, tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)
3. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake:
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba;
Kama siku ya Masa jangwani,
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)
SOMO 2: 2Tim.1:6-8;13-14
Mwanangu, nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana
Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda
wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili,
kwa kadiri ya nguvu ya Mungu. Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani
na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.
SHANGILIO: Yn.15:15
Aleluya, aleluya!
Ninyi nimewaita rafiki,
kwa kuwa yote niliyoyasikia
kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya!
INJILI: Lk.17:5-10
Mitume walimwambia Bwana, Tuongezee imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe
ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii. Lakini, ni nani kwenu
mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng'ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi,
keti, ule chakula? Je, hatamwambia, Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe
kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je, atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya
aliyoagizwa? Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio
na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Imani ina nguvu ya kuhamisha miti au milima. Mwanzo wa imani
yetu labda ni mdogo mno, lakini imani inaweza kukua polepole.
Tumuombe Mungu Baba atuimarishe katika imani yetu.
Ee Baba Mungu,
1. Ufanikishe imani yetu kushindana na vikwazo na magumu
yote yanayotuzuia kuishi kwa uaminifu.
2. Utushirikishe nguvu yako katika kuvunja ukaidi, uzembe na
kutowajibika kwetu.
3. Utupe matumaini ya kutambua kwamba sala zetu
zitasikilizwa kadiri ya uamuzi wako.
4. Utupe moyo wa shukrani kwa maombi uliyotutimizia kwa
upendo wako.
5. Utukumbushe kwamba ukarimu wako ni mkubwa kuliko
matumaini yetu.
Ee Mungu Baba, ulitutia moyo wa kukujia na maombi yetu. Kwa
hiyo uyasikilize maombi tunayokuletea kwa jina la Bwana wetu
Yesu Kristo. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba tu upokee sadaka hii iliyowekwa kwa amri yako. Na, kwa haya mafumbo
matakatifu tunayoadhimisha kwa mujibu wa utumishi wetu wa kikuhani, uwe radhi kutimiza ndani
yetu kazi ya ukombozi wako unaotutakatifuza. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Omb.3:25
Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, kwa hiyo nafsi imtafutayo.
Au
1Kor 10:17
Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja: kwa maana sisi sote twashiriki mkate
mmoja na kikombe kimoja.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu mwenyezi, utujalie sakramenti hii tuliyopokea ituchangamshe na kutulisha. tupate
kugeuka kuwa kile tunachokipokea. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.