DOMINIKA YA 26 YA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Dan.3:31,29,30,43,42
Ee Bwana, yote uliyotutendea, umeyatenda kwa haki, kwa kuwa sisi tumetenda dhambi, wala hatukuzitii amri
zako. Ulitukuze jina lako na kututendea sawasawa na wingi wa huruma zako.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, unayedhihirisha uweza wako hasa kwa kusamehe na kuhurumia. Utuongezee neema yako, ili,
kwa kuzikimbilia ahadi zako, tushirikishwe mema ya mbinguni. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Amo.6:1,4-7
Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria; ninyi mnaolala
juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya masemadari yenu; ninyi mnaokula wanakondoo wa kundi,
na ndama waliomo zizini; ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia
vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi; ninyi mnaokunywa divai katika mabakuli, na kujipaka marhamu
iliyo nzuri; lakini hawahuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu. Basi kwa ajili ya hayo sasa watakwenda
utumwani pamoja na wa kwanza watakaokwenda utumwani, na kelele za machezo za hao waliojinyosha zitakoma.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.146:6-10,(K)1
1. Bwana huishika kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa.
Huwapa wenye njaa chakula,
Bwana hufungua waliofungwa.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
2. Bwana huwafumbua macho waliopofuka,
Huwainua walioinama.
Bwana huwapenda wenye haki,
Huwahifadhi wageni. (K)
3. Bwana huwategemeza yatima na mjane,
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. (K)
SOMO 2: 1Tim.6:11-16
Wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole. Piga
vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele
ya mashahidi wengi. Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu,
aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato, kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa,
pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha,
yeye aliyehimidiwa. Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana; ambaye yeye peke yake
hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala
awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.
SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya!
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana;
Ututakase sisi kwa ile kweli.
Aleluya!
INJILI: Lk.16:19-31
Yesu aliwaambia Mafarisayo, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi,
na kula siku zote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye
alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba
vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye
akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali,
na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole
chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu,
kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa
yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa,
ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu. Akasema, Basi, baba,
nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika
mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu,
lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa
hata mtu akifufuka katika wafu.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Tunapojaliwa mali, tuna wajibu wa kuwashirikisha wote wenye
shida. Kwa kuwashirikisha wengine tunatimiza lile neno lisemalo:
"Nilikuwa na njaa mkanipa chakula." Tumuombe Mungu Baba atusaidie.
Ee Baba Mungu,
1. Mali ni msingi wa maisha ya binadamu. Utupe moyo wa
kutosahau kuwa wafadhili wa wenzetu na kuwa tayari
kuwashirikisha wenzetu mali zetu.
2. Mapambano mengi duniani yanatokana na ugawaji wa mali
usio sawa: Ufungue macho ya wenye mamlaka na mali ili
wasiwe na tama ya mali na wasigandamize haki za
wanyonge.
3. Mali yetu ikiongezeka,tusiambatane nayo kama msingi wa
usalama wetu: Utusaidie tusinaswe katika uroho wa mali.
4. Uzima wetu wa huko mbinguni utategemea ukarimu wetu
wa hapa duniani: Utufungue mioyo yetu tuwaone wenye
shida na kuwasaidia.
Ee Mungu, hakimu wa wanadamu wote, utamhukumu kila mtu
kadiri ya matendo yake. Uyasikilize maombi yetu ili tuepuke
hukumu kali kwa kuzembea maonyo ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu mwenye huruma, ukubali dhabihu yetu hii ikupendeze, nayo itufungulie chemchemi ya
baraka zote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.119:49-50
Ee Bwana, likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, kwa sababu umenitumainisha. Hii
ndiyo faraja yangu katika taabu yangu.
Au
1Yn.3:16
Katika hili tumelifahamu pendo la Mungu, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu;
imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti hii ya mbinguni itufanye wapya rohoni na mwilini, ili tuwe warithi pamoja
naye katika utukufu wake yeye, ambaye tunayashiriki mateso yake tukiitangaza mauti yake. Anayeishi na
kutawala milele na milele.