DOMINIKA YA 25 YA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA:
Bwana asema: Mimi ndimi wokovu wa watu. Katika shida yoyote wataniita, nami nitawasikiliza; nami nitakuwa Bwana wao hata milele.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu, uliyaweka maagizo yote ya sheria takatifu katika upendo kwako na kwa jirani. Utujalie kuzishika amri zako, tupate kustahili kuufikia uzima wa milele. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Amo.8:4-7
Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi, mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini, tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandika ngano? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu, tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano. Bwana ameapa kwa fahari ya Yakobo, Hakika sitazisahau kamwe kazi zao hata mojawapo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.113:1-2,4-8,(K)1,7
1. Aleluya! Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
Lisifuni jina la Bwana.
Jina la Bwana lihimidiwe,
Tangu leo na hata milele.

(K) Msifuni Bwana anayewakweza maskini.

2. Bwana ni Mkuu juu ya mataifa yote,
Na utukufu wake ni juu ya mbingu.
Ni nani aliye mfano wa Bwana,
Mungu wetu aketiye juu;
Anyenyekeaye kutazama, mbinguni na duniani? (K)

3. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Na kumpandisha maskini kutoka jaani.
Amketishe pamoja na wakuu,
Pamoja na wakuu wa watu wake. (K)

SOMO 2: 1Tim.2:1-8
Kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake. Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani ya kweli. Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.

SHANGILIO: 1Sam.3:9;Yn 6:68
Aleluya, aleluya!
Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia;
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya!

INJILI: Lk.16:1-13
Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake. Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena. Yule wakili akasema moyoni mwake. Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao. Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu? Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini. Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini. Yule bwana akamasifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru. Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele. Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Wakili kwenye mfano katika Injili ya leo alitumia akili yake ili kuokoa maisha yake. Alipoteza fedha ya bwana wake na kuogopa atafukuzwa kazini. Yesu alimsifu kama mwenye busara ili kutuhamasisha tutumie akili yetu ili kujiokoa kwenye uzima wa milele.

Tumuombe Mungu Baba,
1. Tamaa zetu zinatuhimiza kusitawisha maisha yetu duniani tu: Utuamshe tusisahau uzima wa milele baada ya maisha duniani.

2. Mali haiwezi kununua mbingu: Utuangaze tutumie mambo ya dunia hii kama msaada wa kupata yale ya mbinguni.

3. Watu wa dunia ni werevu sana: utuepushe tusinaswe kwa mitego ya udanganyifu wa kujipatia mali na kukusahau wewe.

4. Uwashirikishe heri ya uzima wa milele marehemu waliotegemea busara ya imani.

Ee Mungu Baba, sisi mara nyingi tunaogopa kabisa kujitoa kwako na kufuata mpango wako. Utujalie werevu wa huyu wakili mwenye busara. Tunaomba hayo kwa Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uwe radhi kuvipokea vipaji vya taifa lako, ili hayo wanayoungama kwa imani na uchaji wayapate kwa njia ya sakramenti za mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.119:4-5
Wewe umetuamuru mausia yako, ili sisi tuyatii sana. Ningependa njia zangu ziwe thabiti, nizitii amri zako.

Au:
Yn.10:14

Bwana asema: Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sisi unaotulisha kwa sakramenti zako uwe radhi kutuinua kwa njia ya misaada yako ya siku zote, ili tuyapokee matunda ya ukombozi katika mafumbo na katika mwenendo wetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.