DOMINIKA YA 23 YA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.119:137,124
Ee Bwana, wewe ndiwe mwenye haki, na hukumu zako ni za adili. Kama zilivyo rehema zako umtendee
mtumishi wako.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, umetuletea ukombozi na kutufanya watoto wako. Utusikilize kwa wema sisi watoto wa
upendo wako. Tunakuomba ili wote wanaomwamini Kristo wapewe uhuru wa kweli na urithi wa milele.
Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho
Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Hek.9:13-19
Hekima atajisifu nafsi yake, na katikati ya watu wake atajiadhimisha; katika mkutano wake aliye
juu atafumbua kinywa chake, na kujitukuza mbele ya majeshi yake. Ndipo Muumba vitu vyote aliponiagiza,
Aliyeniumba aliisimamisha hema yangu; Akasema, Maskani yako iwe katika Yakobo, Urithi wako na uwe katika
Israeli. Tangu awali aliniumba kabla ya ulimwengu, Wala sikomi kabisa hata milele. Katika hema takatifu
nikahudumu mbele zake, Vivyo hivyo nikathibitika katika Sayuni, Katika mji upendwao akanistarehesha,
Na katika Yerusalemu nikapewa amri; Nikatia shina katika Taifa lililo tukufu, Naam, katika sehemu ya
urithi wa Bwana.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.90:3-6,12-14,17(K)1
1. Wamrudisha mtu mavumbini,
Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku.
(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu
Kizazi baada ya kizazi.
2. Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
Asubuhi huwa kama majani yameayo.
Asubuhi yachipuka na kumea,
Jioni yakatika na kukauka. (K)
3. Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana, urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako. (K)
4. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu.
Na kazi ya mikono yetu uithibitishe. (K)
SOMO 2: Flm.1:9-10,12-17
Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika
vifungo vyangu, yaani, Onesimo; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi
nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili. Lakini sikutaka kutenda
neno lolote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana,
labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali
zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana; na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana.
Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe.
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Ewe Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
Uyatie nuru macho ya mioyo yetu,
Ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya!
INJILI: Lk.14:25-33
Makutano mengi walipokuwa wakifuatana na Yesu, yeye aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye
hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume kwa wake; naam, na hata
nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma
yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi
kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga
msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za
kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya
shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu
ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali. Basi,
kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Bwana Yesu anawaita watu kwake wawe wafuasi kwa namna
mbalimbali. Wengine wanaitwa waache yote ili kumtumikia kwa
utume wa pekee bila familia. Wengine wanaitwa kwa utume wa
maisha ya kikristo katika familia.
Ee Baba Mungu,
1. Kukufuata kunadai nguvu zetu zote, kwa hiyo tunaambiwa
kujipima tunaposikia sauti ya mwito wako: Uwasaidie wale
uliowaita kutambua sauti yako na uwape nguvu ya kuifuata.
2. Uwaimarishe uliowaita katika utumishi waliokabidhiwa.
3. Uwaimarishe watu wa ndoa na uwaongoze kutunza amani,
maelewano na umoja katika familia zao.
4. Uwaongoze vijana wetu wajali udumifu wa maisha ya
ndoa, waache mtindo wa ndoa za majaribio.
5. Uwapokee waumini wote marehemu waliojitahidi kuishi
vizuri maisha yao ya ndoa.
Ee Mungu Mwenyezi, unawaita watu kwa miito mbalimbali ya
maisha. Utusaidie kutambua mwito wetu na uyasikilize maombi
yetu kwa Kristo Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu, uliye asili ya ibada ya kweli na ya amani, tunakuomba utujalie ili kwa vipaji hivi
tuitukuze inavyotakiwa adhama yako, na kwa njia ya kushiriki fumbo hili takatifu tuunganike kiaminifu
katika nia moja. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.42:1-2
Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji, vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, ee Mungu. Nafsi
yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.
Au:
Yn.8:12
Bwana asema: Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali
atakuwa na nuru ya uzima.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, umewalisha waamini wako na kuwatia uzima kwenye meza ya neno lako na ya sakramenti ya
mbinguni. Uwajalie, ili kwa vipaji hivyo bora vya Mwanao mpendwa, wastahili kushirikishwa daima uzima wake.
Anayeishi na kutawala milele na milele.