DOMINIKA YA 22 YA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.86:3,5
Wewe, Bwana, unifadhili, maana nakulilia wewe mchana kutwa. Kwa maana wewe, Bwana, u mwema, umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili kwa watu wote wakuitao.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu wa majeshi, ambaye kila kilicho bora ni chako, ututilie mioyoni mwetu upendo wa jina lako. Pia, kwa kutuongezea uchaji, uyasitawishe ndani yetu yale yaliyo mema, na uyahifadhi kwa ulinzi wako imara yale uliyoyasitawisha. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: YbS.3:17-20,28-29
Mwanangu, wakati wa kufanikiwa uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapendwa kuliko mwenye ukarimu. Kadiri ulivyo mkuu uzidi kujinyenyekesha, nawe utapata kibali machoni pa Bwana; kwa maana rehema zake Bwana zi kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu. Msiba wa mwenye kiburi hauleti kupona, Mche wa uovu umepandika ndani yake. Moyo wa busara utatambua mithali, Na sikio sikivu ni tamaa ya mtaalamu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.68:3-6,9-10,(K)10
1. Wenye haki watafurahi,
Na kuushangilia uso wa Mungu;
Naam, watapiga kelele kwa furaha.
Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake,
Furahini katika Bwana, shangilieni mbele zake.

(K) Ee Mungu,
Kwa wema wako uliwahifadhi walioonewa.

2. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane,
Mungu katika kao lake takatifu.
Mungu huwakalisha wapweke nyumbani,
Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa. (K)

3. Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema,
Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu.
Kabila lako lilifanya kao lake huko;
Ee Mungu,
Kwa wema wako uliwahifadhi walioonewa. (K)

SOMO 2: Ebr.12:18-19,22-24
Hamkufikilia mlima uwezao kuguswa, uliowaka moto, wala wingu jeusi, na giza, na tufani, na mlio wa baragumu na sauti ya maneno; ambayo wale walioisikia walisihi wasiambiwe neno lolote lingine. Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na Kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya.

SHANGILIO: Mt.11:25
Aleluya, aleluya!
Ninakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi,
Kwa kuwa mambo haya uliwaficha
wenye hekima na akili,
Ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya!

INJILI: Lk.14:1,7-14
Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Akawaambia mfano wale walioalikwa, alipoona jinsi walivyochagua viti vya mbele; akisema, Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma. Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe. Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ikiwa tunawaalika rafiki tu na kuwasaidia wenye uwezo wa kuturudishia mema, tunafanya ubaguzi ambao ni dhambi.

Ee Bwana Mungu,
1. Ulitupenda kabla sisi hatujakutambua wala kukuamini: Urekebishe mioyo yetu iwe na ukarimu na wema kwa wote bila ubaguzi.

2. Utujalie roho ya umoja bila kutengana katika misingi ya ukabila, utaifa, jinsia na itikadi za kisiasa.

3. Utupe bidii ya kuwaimarisha wote waliojaliwa mwaliko wako.

4. Uzima wa milele utakuwa maisha ya jumuiya ya waumini wote: Utusaidie tusimpoteze hata mmoja wa wateule wako kwa mifano yetu mibaya.

Ee Mungu Mwenyezi, kwa ufunuo wako ulitaka kugeuza maisha yetu. Utupe nguvu ya kubadilika na usikilize maombi yetu, kwa Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, sadaka takatifu tunayokutolea ituletee daima baraka na wokovu, ili jambo linalotendwa kwa fumbo, likamilishwe ndani yetu kwa nguvu ya sadaka hii. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.31:19
Ee Bwana, jinsi zilivyo nyingi fadhili zako ulizowawekea wakuchao.

Au:
Mt.5:9-10

Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sisi tuliolishwa mkate wa meza ya mbinguni, tunakuomba sana, ili chakula hicho cha mapendo kitutie nguvu moyoni, hata tuhamasishwe kuwatumikia jirani zetu kwa ajili yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.