DOMINIKA YA 21 YA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.86:1-3
Ee Bwana, utege sikio lako unijibu. Wewe uliye Mungu wangu, umwokoe mtumishi wako
anayekutumaini. Wewe, Bwana, unifadhili, maana nakulilia wewe mchana kutwa.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, wewe waiunganisha mioyo ya waamini katika nia moja. Uwawezeshe watu wako wapende
unayoamuru, na kutamani unayoahidi, ili katika ulimwengu huu geugeu, mioyo yetu iwe imejikita kule
kunako furaha za kweli. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe
katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Isa.66:18-21
Bwana asema hivi: Wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona
utukufu wangu. Nami nitaweka ishara kati yao, nami nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, Tarshishi,
na Puli, na Ludi, wavutao upinde, kwa Tubali na Yavani, visiwa vilivyo mbali; watu wasioisikia habari
yangu, wala kuuona utukufu wangu; nao watahubiri utukufu wangu katika mataifa. Nao watawaleta ndugu
zenu wote kutoka mataifa yote, kuwa sadaka kwa Bwana, juu ya farasi, na katika magari, na katika machela,
na juu ya nyumbu, na juu ya wanyama wepesi, mpaka mlima wangu mtakatifu Yerusalemu, asema Bwana; kama
vile wana wa Israeli waletavyo sadaka yao nyumbani kwa Bwana katika chombo safi. Na baadhi ya hao
nitawatwaa kuwa makuhani na Walawi, asema Bwana.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.117, (K)Mk.16:15
1. Aleluya!
Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
Enyi watu wote, mhimidini
(K) Enendeni ulimwenguni mwote,
Mkaihubiri Injili.
2. Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)
SOMO 2: Ebr.12:5-7,11-13
Ndugu zangu, mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau
marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi.
Naye humpiga kila mwana amkubaliye.
Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa
na babaye? Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye
huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani. Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea
na magoti yaliyopooza, mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe,
bali afadhali kiponywe.
SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya!
Maneno yako ndiyo kweli, Ee Bwana,
Ututakase sisi kwa ile kweli.
Aleluya!
INJILI: Yn.1:1-18
Yesu alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja
akamwuliza, Je, Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio
mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. Wakati mwenye nyumba atakaposimama
na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana tufungulie; yeye
atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe
ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote
mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka
na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. Nao watakuja watu toka
mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu. Na
tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Yawezekana kwamba sisi tunabisha mlango wa mbingu na
kuomba utufungulie, lakini Bwana anaweza kutuambia: siwajui
ninyi. Ili kuepuka jibu la kutisha, afadhali tushike mafundisho ya
Bwana.
Bwana Mungu,
1. Ututie bidii ya kupambana na magumu yaliyopo katika
kufuata njia ya kuingia kwenye mlango wa mbinguni.
2. Tukumbuke kwamba maneno matupu hayatatufungulia
mlango wa mbingu: Utuhimize kutekeleza imani yetu kwa
matendo.
3. Uwasaidie Wakubwa wa Kanisa kuwa viongozi wa njia ya
kwenda mbinguni na Uamshe wasaidizi kati ya waumini
katika kazi ya uongozi na ukatekesi.
4. Uwapokee marehemu wote waliojitahidi kuhubiri Neno
lako kwa maneno na matendo yao.
Ee Baba wa huruma, ulitufungulia milango ya mbinguni.
Uyasikilize maombi yetu ili tupitie mlango aliotufungulia Yesu
Kristo, Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, wewe umejipatia taifa la wanao kwa dhabihu moja idumuyo hata milele. Uwe radhi
kutujalia zawadi ya umoja na amani katika Kanisa lako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.104:13-15
Ee Bwana, nchi imeshiba mazao ya kazi zako, ili utoe chakula katika nchi, na divai imfurahishe mtu
moyo wake.
Au:
Yn.6:54
Bwana asema: Aulaye mwili wangu na kuinywa
damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua
siku ya mwisho.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakuomba utuponye kabisa kwa dawa ya huruma yako. Utukamilishe kwa wema wako na
kutuhifadhi hivi, hata tuweze kukupendeza katika mambo yote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.