DOMINIKA YA 20 YA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.84:9-10
Ee Mungu, ngao yetu, uangalie, umtazame uso Masiya wako. Hakika siku moja katika nyua zako ni bora
kuliko siku elfu.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, umewaandalia wakupendao mema yasiyoonekana. Uwashe mioyoni mwetu moto wa
upendo wako, ili, kwa kukupenda wewe katika yote na kuliko yote, tuzifikie ahadi zako zinazopita hamu
zote. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho
Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Yer.38:4-6,8-10
Ndipo wakuu wakamwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa
vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu
huyu hawatafutii watu hawa heri, bali shari. Naye mfalme Sedekia akasema, tazama, yu mikononi mwenu;
maana mfalme siye awezaye kufanya neno lolote kinyume chenu. Basi wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika
shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo katika uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni
hamkuwa na maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo. Ebedmeleki akatoka nyumbani
mwa mfalme, akamwambia mfalme, akisema, Ee Bwana wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika mambo
yote waliyomtenda Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi atakufa pale alipo, kwa sababu
ya njaa; kwa kuwa hapana mkate kabisa katika mji. Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, mkushi, akisema,
chukua pamoja nawe watu thelathini; toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla hajafa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.40:1-3,17,(K)13
1. Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu.
(K) Ee Bwana, unisaidie hima.
2. Akanipandisha toka shimo la uharibifu,
Toka udongo wa utelezi;
Akaisimamisha miguu yangu mwambani,
Akaziimarisha hatua zangu. (K)
3. Akatia wimbo mpya kinywani mwangu,
Ndio sifa zake Mungu wetu.
Wengi wataona na kuogopa,
Nao watamtumaini Bwana. (K)
4. Nami ni maskini namhitaji,
Bwana atanitunza.
Ndiwe msaada wangu na wokovu wangu,
Ee Mungu wangu, usikawie. (K)
SOMO 2: Ebr.12:1-4
Wapenzi, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo
mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa
mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha
iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti
cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya
watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika
damu, mkishindana na dhambi.
SHANGILIO: Lk.19:38
Aleluya, aleluya!
Ndiye Mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana;
Amani mbinguni, na utukufu huko juu.
Aleluya!
INJILI: Lk.12:49-53
Siku ile Yesu aliwaambia makutano: Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini
nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatizwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe?
Je, Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. Kwa kuwa
tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa
watatu. Watafarakana, baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye;
mkwe mtu na mkwewe; mkwe na mkwe mtu.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Japo Yesu ameleta amani duniani kwa wanaomuamini, kumfuata
Yesu kunaleta utengano na mafarakano kwa baadhi ya watu
wasiomuamini.
Ee Bwana Mungu tunaomba,
1. Uwajalie wakubwa na wenye mamlaka serikalini kulinda
uhuru wa kubudu kwa wananchi wao.
2. Utuwezeshe kutambua hatari zinazopinga imani yetu na
hivyo kuzipinga.
3. Utupe nguvu ya kushinda vishawishi vyote vinavyotuzuia
kufuata njia yako.
4. Utupe neema ya kupokea mwito wako wa kukufuata na
kukupenda zaidi ya yote.
5. Uwakirimie marehemu wote raha ya milele.
Ee Mungu Mwenyezi, ulitupa amani yako tupate kutofautisha
amani yako na kila aina ya amani ya uwongo. Usikilize maombi
yetu kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliyetupatia amani yako.
Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uvipokee vipaji vyetu vinavyotufanya tushirikiane nawe katika muungano huu mtukufu, ili
tunapokutolea vile ulivyotupatia, tustahili kukupokea wewe mwenyewe. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.130:7
Kwa Bwana kuna fadhili, na kwake kuna ukombozi mwingi.
Au:
Yn.6:51-52
Bwana asema: Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula
hiki, ataishi milele.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, kwa njia ya sakramenti hii tumefanywa washiriki wa Kristo. Tunakuomba kwa unyenyekevu
huruma yako, ili, kwa kufanana naye hapa duniani, tustahili kuwa washiriki pamoja naye pia kule
mbinguni. Anayeishi na kutawala milele na milele.