DOMINIKA YA 1 MAJILIO

MASOMO MWAKA A

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.25:1-3
Nakuinulia nafsi yangu, Ee Mungu wangu, nimekutumaini Wewe, nisiaibike. Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda. Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, twakuomba, uwajalie waamini wako ari ya kumlaki kwa matendo ya haki Kristo wako anayekuja, ili, akiisha kuwaweka kuumeni kwake, wapate kuumiliki ufalme wa mbinguni. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa.2:1-5
Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi katika habari za Yuda na Yerusalemu. Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.122:1-4,8-9.(K)1
1. Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.

(K) Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana.

2. Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. (K)

3. Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu
Niseme sasa, Amani ikae nawe.
Kwa ajili ya nyumba ya Bwana, Mungu wetu,
Nikutafutie mema. (K)

SOMO 2: Rum.13:11-14
Ndugu zangu, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini. Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia; basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru. Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.

SHANGILIO: Zab.85:7
Aleluya, aleluya!
Ee Bwana utuoneshe rehema zako, Utupe na wokovu wako,
Aleluya!

SOMO 3: INJILI: Mt.24:37-44
Siku ile, Yesu aliwaambia wafuasi wake kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni, mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. Kesheni basi, kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu katika kristo, mwanzoni mwa Majilio Enjili inatukumbusha habari ya Nuhu aliyemtii Mungu na kuokolewa katika gharika kuu iliyowaangamiza wale wote wasiokuwa na imani kwa Mungu. Tumuombe Mungu Baba. Ee Mungu Mwenyezi,

1. Utufumbue macho yetu tuione na kuifuata njia yako ya wokovu katika maisha yetu ya kila siku.

2. Uwaongoze viongozi wote kujiandaa kutoa hesabu mbele yako kuhusu utawala na uongozi wao.

3. Utusaidie sisi wanadamu kuishi tukijua na kuamini kwamba Kristu atakuja tena siku ya mwisho kuwahukumu wazima na wafu.

4. Utuongoze kujitayarisha kwa toba, sala, kujinyima anasa na matendo ya huruma ili kuweka mioyo yetu tayari kumpokea Kristu atakapokuja.

5. Uwafanye waliojitenga nawe kwa udhaifu na tamaa ya mambo ya dunia, kulipokea tena Neno lako kwa amani, furaha na upendo na hivyo kujiunga tena na jamii ya waumini.

6. Uwapokee Marehemu wetu katika ufalme wako wa milele.

Ee Mungu, Baba mwenyezi, usikilize maombi yetu kwa jina la Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana tunakuomba, uvipokee vipaji tunavyokutolea, ambavyo tumevipokea kutoka kwa mema yako. Na yale unayotujalia kuyatenda kwa ibada katika wakati huu, yawe kwetu tuzo ya ukombozi wako wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

1. UTANGULIZI WA MAJILIO:
MAJILIO I:

K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye, katika ujio wake wa kwanza, alipokuja katika unyenyekevu wa mwili, aliutimiza mpango ulioandaliwa nawe tangu kale. Hivyo, akatufungulia njia ya wokovu wa milele, ili, atakapokuja tena katika utukufu wa enzi yake, hatimaye tupewe waziwazi mema yaliyoahidiwa, ambayo kwa sasa tunathubutu kuyatarajia, tukikesha.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.85:12
Bwana atatoa kilicho chema, na nchi yetu itatoa mazao yake.

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Bwana tunakuomba, yatufae sisi mafumbo tuliyoyaadhimisha, ambayo tangu sasa, wakati tunapoenenda kati ya mambo yapitayo, tunaandaliwa kwayo kuyapenda mambo ya mbinguni na kuambatana na yale yadumuyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.