DOMINIKA YA 1 KWARESIMA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.91:15-16
Ataniita nami nitamwitikia; nitamwokoa na kumtukuza, kwa siku nyingi nitamshibisha.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, utujalie tuzidi kulifahamu fumbo la Kristo, kwa njia ya mazoezi ya kipindi cha Kwaresima tunachojaliwa kila mwaka. Na kwa njia hiyo, tuyafuate yale yanayotokana na fumbo hilo, kwa mienendo inayostahili. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Kum.26:4-10
Musa aliwaambia Waisraeli wote: Kuhani atakipokea kikapu mkononi mwako, akiweke chini mbele ya madhabahu ya Bwana, Mungu wako: Nawe ujibu, ukaseme mbele za Bwana Mungu wako. Baba yangu alikuwa Mwarami karibu na kupotea, akashuka Misri akakaa huko ugenini, nao ni wachache hesabu yao; akawa taifa kubwa huko, lenye nguvu na watu wengi. Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito. Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu. Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu; naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali. Na sasa, tazama, nimeleta malimbuko ya mazao ya ardhi uliyonipa, ee Bwana. Kisha ukiweke chini mbele za Bwana, Mungu wako, ukasujudu mbele za Bwana, Mungu wako.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.91:1-2,10-15 (K)15
1. Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu
Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu
na ngome yangu.
Mungu wangu nitakayemtumaini.

(K) Ee Bwana, uwe pamoja nami
Katika taabu zangu.

2. Mabaya hayatakupata wewe,
Wala tauni haitakaribia hema yako.
Kwa kuwa atakuagizia malaika zake
Wakulinde katika njia zako zote. (K)

3. Mikononi mwao watakuchukua,
Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
Utawakanyaga simba na nyoka,
Mwanasimba na joka utawaseta kwa miguu. (K)

4. Kwa kuwa amekaza kunipenda
Nitamwokoa; na kumweka palipo juu,
Kwa kuwa amenijua jina langu.
Ataniita nami nitamwitikia;
Nitakuwa pamoja naye taabuni,
Nitamwokoa na kumtukuza. (K)

SOMO 2: Rum.10:8-13
Ndugu zangu, Musa asemaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.

SHANGILIO: Mt.4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu,
ila kwa kila neno
litokalo katika kinywa cha Mungu.

INJILI: Lk.4:1-13
Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa. Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate. Yesu akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu. Akampandisha juu, akamwonesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa yeyote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; na ya kwamba, Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu zangu, shetani anatumia ujanja ili amnase Yesu kwa vishawishi. Yesu ana ujanja na akili kuliko shetani, Anamshinda shetani. Shetani anataka kutumia ujanja kutushawishi pia. Tumuombe Yesu atusaidie kushinda vishawishi.

1. Utupe nguvu ya kupambana na vishawishi vinavyotukabili katika maisha yetu ya kila siku.

2. Utufungue macho ya akili zetu tutambue kuwa Ufalme wa Mungu si ufalme wa kupigania mamlaka na madaraka, bali ni kutimiza amri zako kwa njia ya kuwatumikia wenzetu.

3. Utupe nguvu ya kupambana na kuvumilia shida, taabu na mateso ya duniani ili kustahili tuzo ya mbinguni.

4. Utusaidie kwa nguvu ya Roho Mtakatifu ili tuweze kushinda vishawishi na tamaa ya madaraka na mali.

5. Uwaimarishe wale wote wanaoteseka kwa sababu ya magonjwa, njaa, vita na magomvi wasikate tamaa bali wategemee msaada wako.

Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utufanye tustahili kukutolea inavyofaa vipaji hivi, vinavyotusaidia kuadhimisha mwanzo wa kipindi hiki kitakatifu cha Kwaresima. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI
Kujaribiwa kwa Bwana
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye kwa siku arobaini alijinyima chakula cha kidunia, akaonesha hivyo namna ya kufanya kitubio. Yeye, kwa kupindua hila zote za nyoka wa kale, alitufundisha kushinda chachu ya uovu, ili kwa kuadhimisha fumbo la Pasaka kwa mioyo inayostahili, hatimaye tuifikie Pasaka ya milele.
Kwa hiyo, sisi pamoja na umati wa Malaika na Watakatifu, tunakuimbia utenzi wa sifa, tukisema bila Mwisho.
Mtakatifu, Mtakatifu,Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

AU: Zab.91:4
Bwana atakufunika kwa manyoya yake, chini ya mbawa zake utapata kimbilio.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tumekula mkate wa mbinguni unaolisha imani, kuhamasisha tumaini na kuyatia nguvu mapendo. Tunakuomba, tujifunze kumtamani Yeye aliye mkate hai na wa kweli, na tuweze kuishi kwa kila neno litokalo kinywani mwako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

SALA YA KUWAOMBEA WAAMINI:
Ee Bwana, tunakuomba baraka yako iwashukie kwa wingi watu wako; ili, palipo na taabu, matumaini yaongezeke; palipo na kishawishi, nguvu ithibitishwe; na wajaliwe wokovu wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.