DOMINIKA YA 19 YA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.74:20,19,22,23
Ee Bwana, ulitafakari agano, usisahau milele uhai wa watu wako walioonewa. Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe, usiisahau sauti ya watesi wako.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, kwa kufundishwa na Roho Mtakatifu tunathubutu kukuita Baba. Uikamilishe mioyoni mwetu roho ya kuwa wana, ili tustahili kuingia katika urithi tulioahidiwa. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Hek.18:6-9
Usiku ule baba zetu walitangulia kuonywa, ili wakiwa na ufahamu hakika, wafurahishwe na viapo walivyovitegemea; kwa hiyo watu wako waliutazamia wokovu wa wenye haki na uharibifu wa adui. Madhali uliwalipia kisasi watesi wale, na kwa njia ile ile uliwatukuza ukituita ili tukujie. Zaidi ya hayo watoto watakatifu wa watu wema walitoa dhabihu kwa siri, na kwa moyo mmoja walijitwalia agano la torati ya dini, ya kwamba watashirikiana katika mambo mema na vilevile katika hatari; pindi walipoimbisha nyimbo takatifu za mababu katika kumhimidi Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:1,12,18-19,20-22 (K)12
1. Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake.

(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.

2. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojea fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

3. Nafsi zetu zinamngoja Bwana,
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe. (K)

SOMO 2: 2Ebr.11:1-2,8-19 (au somo fupi 11:1-2.8-12)
Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa. Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu. Kwa imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba, alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu. Na kwa ajili ya hayo wakazaliwa na mtu mmoja, naye alikuwa kama mfu, watu wengi kama nyota za mbinguni wingi wao, na kama mchanga ulio ufuoni, usioweza kuhesabika.
(11:13-19) Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi. Maana hao wasemao maneno kama hayo waonesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea. Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji. Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee; Naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.

SHANGILIO: Yn.8:12
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana;
Yeye anifuataye atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya!

INJILI: Lk.12:32-48 (au somo fupi 12:35-40)
Yesu aliwaambia makutano: Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme. Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu. Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu.
(12:35-40) Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao. Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwizi; angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.
(12:41-48) Petro akamwambia, Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia? Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo. Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini. Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Bwana Yesu alitutia moyo tusihangaike kwa sababu waumini ni kundi dogo. Lakini sisi tumepewa enzi ya ufalme wa Mungu kama chachu ambayo kazi yake ni kuchachusha dunia yote.

Ee Bwana Yesu,
1. Ulisema kwamba ilimpendeza Mungu Baba kutupa sisi Ufalme wa Mungu: Utupe matumaini tusilegee katika bidii ya kueneza Ufalme huo.

2. Imani yetu ina nguvu ya chachu: Utuoneshe njia ya kuwaangaza wenzetu kwa mwanga wa imani yetu na kuyakoleza maisha kwa matendo yetu mema.

3. Utusaidie tusinaswe na tamaa ya kujilundikia mali zaidi na zaidi, bali tuwasaidie wale wanaohitaji msaada wa kulisha familia zao.

4. Utufanye tuwe tayari kuwagawia wenzetu mali kabla ya kufariki dunia.

5. Utusaidie kujitayarisha kwa siku ya kufa kwetu.

Ee Baba wa mbinguni, uliwachagua waumini wawe kama chachu kwa dunia. Utusikilize kwa jina la Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uwe radhi kuvipokea vipaji vya kanisa lako ulivyotujalia kwa huruma yako tupate kukutolea; nawe kwa uweza wako unavifanya vigeuke kuwa sakramenti ya wokovu kwa ajili yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.147:12.14
Msifu Bwana, ee Yerusalemu, akushibishaye kwa unono wa ngano.

Au:
Yn 6:51

Bwana asema: Chakula nitakachotoa mimi, ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti yako tuliyoipokea ituokoe na ituimarishe katika nuru ya ukweli wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.