DOMINIKA YA 18 YA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.70:1,5
Ee Mungu, uniokoe; ee Bwana, unisaidie hima. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, ee Bwana, usikawie.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Bwana, uwe karibu na watumishi wako, na uwaoneshe wema wako wa milele hao wakuombao. Na kwa hao wanaojisifia kwamba wewe ndiwe muumba na mtawala wao, utengeneze upya vilivyoumbwa, na kuvihifadhi vilivyotengenezwa. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Mhu.1:2; 2:21-23
Mhubiri asema, Ubatili mtupu ubatili mtupu. Mambo yote ni ubatili. Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu. Kwa maana mtu hupata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake alivyojitahidi chini ya jua? Kwa kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.95:1-2,6-9,(K)7-8
1. Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi.

(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake,
Msifanye migumu mioyo yenu.

2. Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)

3. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)

SOMO 2: Kol.3:1-5,9-11
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu. Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu. Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu. Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba. Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote.

SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Ewe Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,
uyatie nuru macho ya mioyo yetu,
ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya!

INJILI: Lk.12:13-21
Mtu mmoja katika mkutano alimwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu. Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu? Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Kwa mfano wa tajiri mjinga, Yesu alitaka kutuonya tusinaswe na tamaa ya kulundika mali, kumsahau Mungu na kuwadharau wenzetu.

Ee Bwana Yesu,
1. Katika mfano, Tajiri alisahau kwamba mali haiwezi kusalimisha maisha yake; utusaidie tusiabudu mali na kusahau amri ya upendo.

2. Tajiri huyu alifariki dunia bila kuwa na faida ya utajiri wake; utufundishe kwamba usalama wetu haupatikani katika lundo la mali ya duniani bali katika wewe.

3. Kosa la tajiri huyo lilikuwa kujifikiria binafsi tu. Utusaidie kukumbuka wajibu wetu wa kuwapa chochote wenye shida.

4. Mapambano mengi duniani yanatokea kwa kuwa wenye mali wanawanyima wenzao mahitaji ya maisha. Utuhimize kuhakikisha kuwa kila mtu anapata haki yake.

Ee Mungu mwenye utajiri wote mbinguni na duniani, uliwapa wanadamu wote neema ya kurahia dunia nzima kwa pamoja, bila ubaguzi. Tunakupelekea maombi yetu tupate kuelewa mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakusihi uvitakase vipaji hivi, uipokee na kafara hii ya kiroho, na utufanye sisi tuwe kwako sadaka ya milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Hek.16:20
Ee Bwana, ulitupa sisi mkate toka mbinguni, chakula kitamu na cha kupendeza tamaa ya kila mtu.

Au:
Yn 6:35

Bwana asema: Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, uwalinde daima wale uliowatia nguvu kwa chakula cha mbinguni. Na wote unaowatunza daima, wastahili kupata ukombozi wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.