DOMINIKA YA 17 YA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.68:5-6,35
Mungu yu katika kao lake takatifu; Mungu huwakalisha wapweke nyumbani, Yeye huwapa watu
wake nguvu na uwezo.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, wewe ndiwe ngao yao wote wanaokukimbilia. Pasipo wewe hapana kilicho thabiti
wala kitakatifu. Utuzidishie rehema yako, ili kwa mamlaka na maongozi yako, tupate kuzitumia
mali za muda huu kwa namna inayotuwezesha kuambatana na zile zinazodumu milele. Kwa njia ya
Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu,
Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Mwa.18:20-32
Bwana alisema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana. Basi,
nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi
wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana.
Ibrahimu akakaribia, akasema, Je, Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki
hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? Hasha,
usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu
wote asitende haki? Bwana akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali
pote kwa ajili yao. Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na
majivu tu. Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, Je, Utaharibu mji wote kwa kupungua
watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano. Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda
wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini. Akasema, Bwana asiwe na hasira,
nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. Akasema,
Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya
hao ishirini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi?
Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.138:1-3.6-9.(K)3
1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
(K) Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.
2. Nitalishukuru jina lako,
Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umekuza ahadi yako,
Kuliko jina lako lote.
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)
3. Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu,
Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali.
Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha,
Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu. (K)
4. Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
Bwana atanitimiliza mambo yangu;
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako. (K)
SOMO 2: Kol.2:12-14
Mlizikwa pamoja na Kristo katika Ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu
za Mungu aliyemfufua katika wafu. Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa
kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati
iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea
msalabani.
SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya!
Mtu akinipenda, atashika neno langu,
na Baba yangu atampenda;
nasi tutakuja kwake.
Aleluya!
INJILI: Lk.11:1-13
Yesu alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana,
tufundishe sisi kusali, kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, Msalipo, semeni,
Baba [yetu uliye mbinguni]. Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani
kama huko mbinguni.] Utupe siku kwa siku riziki yetu. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi
tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu]. Akawaambia, Ni nani
kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu,
kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake; na yule
wa ndani amjibu akisema, usinitaabishe; mlango umekwishafungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto
wangu; siwezi kuondoka nikupe? Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake,
lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake. Nami nawaambia, Ombeni,
nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye
atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba
mkate, atampa jiwe? au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa
ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je, Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa
Roho Mtakatifu hao wamwombao?
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Yesu alitufundisha wafuasi wake kusali. Aliwafundisha sala ya
Baba yetu ambayo tunarudia mara kwa mara katika maisha yetu.
Ee Bwana Yesu,
1. Ulituonesha Baba yetu wa mbinguni: Utusaidie kumpenda
Mungu kama Baba yetu ambaye anatutunza kwa wema
wake.
2. Tunamuomba Baba aoneshe utukufu na enzi yake katika
maisha yetu ya kila siku hapa duniani.
3. Tunaomba ufalme wa amani na haki uenee katika familia
na jumuiya zetu.
4. Utuoneshe mapenzi ya Baba na utupe msaada wa
kuyatimiza.
5. Tunaomba msaada katika shughuli zetu za kujipatia
mahitaji ya maisha ya kila siku.
6. Tunaomba tupewe nguvu ya kushinda yote yanayoweza
kututenga na Mungu Baba.
7. Dunia imejaa maovu; utujalie nguvu ya kupambana na
nguvu za ubaya ndani yetu na katika mazingira yetu.
Ee Baba wa mbinguni, Mwana wako alitufundisha tukuendee
wewe katika shida zetu. Kwa hiyo tunakupelekea maombi yetu
kwa jina la Kristo Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba uvipokee vipaji. hivi tunavyokutolea kutoka wingi wa vitu ulivyotukirimia.
Kwa nguvu tendaji ya neema yako mafumbo haya matakatifu yatakatifuze mwenendo wetu wa maisha ya
sasa, na kutufikisha kwenye furaha za milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.103:2
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usizisahau fadhili zake zote.
Au:
Mt.5:7-8
Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema.
Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tumepokea sakramenti ya kimungu, ambayo ni ukumbusho wa daima wa Mateso ya
Mwanao. Tunakuomba zawadi hii aliyotujalia Mwanao kwa mapendo yasiyo na kifani ituletee
wokovu. Anayeishi na kutawala milele na milele.