DOMINIKA YA 16 YA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.54:4,6
Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu. Kwa ukunjufu wa
moyo nitakutolea dhabihu; ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Bwana, uwabariki watumishi wako, na uwaongezee kwa huruma vipaji vya neema yako, ili,
wakiwa na ari katika matumaini, imani na mapendo, wadumu daima katika kuzishika kiaminifu
amri zako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja
wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Mwa.18:1-10a
Bwana alimtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana
wakati wa hari. Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona
alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, Bwana wangu, kama nimeona
fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu,
mkapumzike chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee,
iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya,fanya kama ulivyosema. Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa
Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. Ibrahimu akapiga mbio kwenda
kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa
siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao
wakala. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati uu huu
mwakani. Na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.15.(K)1
1. Bwana, ni nani atakayefanya maskani yake
Katika kilima chako kitakatifu?
Ni yeye aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki;
Asemaye kweli kwa moyo wake,
Asiyesingizia kwa ulimi wake.
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako?
2. Yeye ambaye hakumtenda mwenziwe mabaya,
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana. (K)
3. Yeye ambaye hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo
Hataondoshwa milele. (K)
SOMO 2: Kol.1:24-28
Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale
yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, Kanisa lake, ambalo nimefanywa
mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri
ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake;
ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni
Kristo ndani yenu; tumaini la utukufu; ambaye sisi tunamhubiri habari zake, tukimwonya kila mtu, na
kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo.
SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya!
Mtu akinipenda, atalishika neno langu;
Na Baba yangu atampenda;
Nasi tutakuja kwake.
Aleluya!
INJILI: Lk.10:38-42
Ikawa katika kuenenda kwao Yesu aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha
akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi mniguuni pake
Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea,
akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie
anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu
vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Yesu alikubali kualikwa na kukaribishwa chakulani. Maria na
Martha, dada wawili wa Lazaro walikuwa rafiki wa Yesu kadiri ya
mapokeo ya zamani.
Ee Bwana Yesu,
1. Ulikubali kualikwa kirafiki: Utusaidie kuheshimu urafiki
wa kweli kama tunda la Ufalme wa Mungu.
2. Martha na Maria walikuwa na tabia tofauti; mchapa kazi
kati yao anahitaji nafasi ya kufikiria neno la Mungu:
Utuoneshe njia ya kuunganisha shughuli zetu na saa za
sala zetu.
3. Tukubali onyo, Tusinaswe katika shughuli bila kukumbuka
shabaha yetu ya kualikwa mbinguni.
4. Utuongoze tusifanye shughuli zetu bila kumtegemea
Mungu Baba katika hali yote.
5. Mara kwa mara tunafikiri kwamba kazi zetu ni muhimu
zaidi kuliko imani yetu: Utusaidie kumpa Mungu baba
nafasi ya kwanza katika maisha ya kila siku.
Ee Baba wa huruma, uyapokee maombi yetu tupate msaada kwa
kazi na bidii katika sala zetu kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu, ulikamilisha kafara mbalimbali za sheria ya zamani kwa njia ya sadaka pekee ya Kristo.
Uipokee sadaka hii kutoka kwa watumishi wako waaminifu, uibariki na kuitakatifuza kama ulivyoibariki
sadaka ya Abeli, ili kile alichokutolea kila mmoja wetu kwa heshima ya adhama yako, kifae kwa
wokovu wa wote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.111:4-5
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu; Bwana ni mwenye fadhili na rehema; amewapa
wamchao chakula.
Au:
Ufu.3:20
Bwana asema: Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua
mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakuomba kwa wema wako uwe nasi taifa lako. Na sisi uliotulisha mafumbo ya mbinguni,
utufanye tuondokane na maisha ya zamani, tuingie katika upya wa uzima. Kwa njia ya Kristo Bwana
wetu.