DOMINIKA YA 15 YA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.17:15
Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, niamkapo nishibishwe kwa sura yako.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, unawaonesha mwanga wa ukweli wako wale wanaopotea, ili waweze kurudi kwenye
njia ya haki. Uwawezeshe wote ambao, kwa imani wanayoungama, wanahesabiwa kuwa Wakristo,
wayakatae mambo yanayopingana na jina hilo, na kuyafuata yale yanayopatana nalo. Kwa njia
ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu,
Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Kum.30:10-14
Ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa
katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako
yote. Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali. Si mbinguni, hata
useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya? Wala si
ng'ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie,
tupate kuyafanya? Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.69:13,16,29-30,32-33,
1. Nami maombi yangu nakuomba wewe, Bwana,
Wakati ukupendezao; Ee Mungu,
Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.
Katika kweli ya wokovu wako.
Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema,
Kwa kadiri ya rehema zako unielekee.
(K) Enyi mmtafutao Mungu,
mioyo yenu ihuishwe.
2. Nami niliye maskini na mtu wa huzuni.
Mungu, wokovu wako utaniinua.
Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
Nami nitamtukuza kwa shukrani. (K)
3. Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mumtafutao Mungu mioyo yenu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji.
Wala hawadharau wafunga wake. (K)
4. Maana Mungu ataiokoa Sayuni,
na kuijenga miji ya Yuda,
Wazao wa watumishi wake watairithi,
Nao walipendao jina lake watakaa humo. (K)
SOMO 2: Kol.1:15-20
Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye
vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana;
ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na
kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye
kichwa cha mwili, yaani, cha Kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba
awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye
kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye,
ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.
SHANGILIO: Mdo.16:14
Aleluya, aleluya!
Fungua moyo wetu, Ee Bwana,
ili tuyatunze maneno ya mwanao.
Aleluya!
INJILI: Lk.10:25-37
Siku ile, mwanasheria mmoja alisimama amjaribu, akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa
milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako
kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani
yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi. Naye akitaka kujidai haki,
alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu
kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang'anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha
karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi
vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika
hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai;
akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa
dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na chochote utakachogharimiwa zaidi,
mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule
aliyeangukia kati ya wanyang'anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako,
nawe ukafanye vivyo hivyo.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Habari ya Msamaria mwema ni mfano wa Yesu mwenyewe. Yeye
alikuwa Msamaria mwema aliyeshuka kutoka mbinguni ili
kuponya majeraha yetu.
Ee Bwana Yesu,
1. Uamshe mioyo yetu tusimnyime mtu yeyote msaada wetu
hasa wale walio katika shida kama vile ajali, njaa,
magonjwa na msiba.
2. Tunawaombea wenye madaraka katika jumuiya, wawe
tayari kuwasaidia raia wanaokandamizwa kwa sababu ya
hali ngumu ya kazi au uchumi.
3. Wazee wengi katika vijiji na mitaa yetu wanaishi bila
msaada, utujaze moyo wa kuwa wasamaria wema wao
kuwatuliza na kuwaondolea shida zao.
4. Uwasaidie viongozi wa Kanisa kuangalia na kuhakikisha
kuwa huduma za Caritas zinawasaidia maskini na wote
wenye shida.
Ee Baba wa huruma, wewe u mwema na mkarimu na ulitaka
waumini wako wafuate mfano wa wema wako. Uyapokee maombi
yetu kwa Kristo Bwana wėtu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uvitazame vipaji vya Kanisa lako likuombalo, ujalie vipokelewe kwa ajili ya kukuza
utakatifu wa waamini. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.84:3-4
Shomoro naye ameona nyumba, na mbayuwayu amejipatia kioto, alipoweka makinda yake, kwenye
madhabahu zako, ee Bwana wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu. Heri wakaao nyumbani mwako,
watakuhimidi daima.
Au:
Yn 6:56
Bwana asema: Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kuila sadaka hii, tunakuomba matunda ya wokovu wetu yaongezeke kadiri
tunavyoshiriki mara nyingi mafumbo haya. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.