DOMINIKA YA 14 MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.48:9-10
Tumezitafakari fadhili zako, ee Mungu, katikati ya hekalu lako. Kama lilivyo jina lako, ee
Mungu, ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia. Mkono wako wa kuume umejaa haki.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, kwa njia ya unyenyekevu wa Mwanao umeuinua ulimwengu uliokuwa umeanguka. Uwajalie
waamini wako furaha takatifu ili, hao uliowaondoa katika utumwa wa dhambi, wapate kuifikia
furaha ya milele. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika
umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Isa.66:10-14
Furahini pamoja na Yerusalemu, shangilieni kwa ajili yake, ninyi nyote mmpendao; furahini pamoja
naye kwa furaha, ninyi nyote mliao kwa ajili yake; mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya
faraja zake, mpate kukama, na kufurahiwa kwa wingi wa utukufu wake. Maana Bwana asema hivi, Tazama,
nitamwelekezea amani kama mto, na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho, nanyi mtapata kunyonya;
mtabebwa; na juu ya magoti mtabembelezwa. Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji, ndivyo nitakavyowafariji
ninyi; nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu. Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu
itasitawi kama majani mabichi; na mkono wa Bwana utajulikana, uwaelekeao watumishi wake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.66:1-7,16,20,(K)1
1. Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake.
Tukuzeni sifa zake,
Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini!
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe,
nchi yote,
2. Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimba jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu,
Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu. (K)
3. Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa miguu;
Huko ndiko tuliko mfurahia,
Atawala kwa uweza wake milele. (K)
4. Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu,
Wala kuniondolea fadhili zake. (K)
SOMO 2: Gal.6:14-18
Mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa
huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala
kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya. Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na
rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini
mwangu chapa zake Yesu. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.
SHANGILIO: Yn.1:12,14
Aleluya, aleluya!
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;
wote waliompokea aliwapa uwezo wa
kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya!
INJILI: Lk.10:1-12,17-20 (au somo fupi Lk.10:1-9)
Baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji
na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni
wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni,
nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie
mtu njiani. Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana
wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo,
mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihamehame kutoka nyumba
hii kwenda nyumba hii. Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele
yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.
(10:10-12,17-20) Na mji wowote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni
humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yetu
tunayakung'uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia. Nawaambia ya kwamba
siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo. Ndipo wale sabini
waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani,
akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za
yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini
kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Bwana Yesu alitaka kuwatayarisha wasaidizi na kuwaita mitume
atakaowatuma kuendeleza utume alioanzisha yeye mwenyewe.
Aliwapa mitume wake maagizo mengi tuliyosikia katika Enjili ya
leo. Baada ya kupaa mbinguni, Yesu aliwapelekea Roho wake ili
awaimarishe kutimiza maagizo waliyopewa.
Ee Bwana Yesu,
1. Uliwapeleka mitume duniani ili watangaze habari ya
Ufalme wa Mungu; uwaimarishe wote uliowachagua kwa
utumishi wako.
2. Uliwaambia mitume wafuate njia uliyotangulia kuienda;
utupe moyo tutegemee njia yako zaidi kuliko maarifa yetu
ya kibinadamu.
3. Uliwatayarisha mitume wako waishi kadiri ya masharti ya
Ufalme wa Mungu: utuwezeshe kuishi kadiri ya yale
tunayoyatangaza.
4. Mitume wako walijaliwa amani wawashirikishe waumini.
Utusaidie kueneza amani yako bila magomvi wala
mafarakano.
5. Ulisema kwamba mti mwema unajulikana kwa matunda
yake, utusaidie tuzalishe matendo mema kwa imani.
Ee Mungu Mwenyezi, uliweka mitume wawakusanye waumini
wako. Uyasikilize maombi yetu tuwe waumini waaminifu kwa
Bwana wetu Yesu Kristo. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunaomba sadaka tunayotoa kwa heshima ya jina lako itutakase, na ituwezeshe kutenda
siku kwa siku kadiri ya uzima wa mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.34:8
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; heri mtu yule anayemtumaini.
Au:
Mt.11:28
Bwana asema: Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sisi tulioshibishwa na sadaka kubwa namna hii, tunakuomba utujalie kuitunza zawadi
hiyo iletayo wokovu, wala tusiache kamwe kukusifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.