JUMANNE OKTAVA YA PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.2:36-41
Petro aliwaambia Wayahudi: Nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya
Yesu huyo mliyesulibisha kuwa Bwana na Kristo. Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia
Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja
kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa
wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na
kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa;
na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:4-5,18-20,22(K)5
1. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana.
(K) Nchi imejaa fadhili za Bwana
Au:
Aleluya.
2. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)
3. Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe. (K)
SHANGILIO: Zab.118:24
Aleluya, aleluya,
Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana,
tutaishangilia na kuifurahia.
Aleluya.
INJILI: Yn.20:11-18
Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na
kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani
na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia,
Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka. Naye akiisha kusema hayo, akageuka
nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini?
Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua
wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa. Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia
kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa
kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye
ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi
habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo.
MAOMBI
Ee Mungu uliyemfufua Yesu aliyesulibiwa na ukamfanya Bwana na Kristo, twakuomba:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie wakosefu wote toba ya kweli, ili wapate ondoleo la dhambi na kipawa cha Roho Mtakatifu.
2. Ukiokoe kizazi chetu hiki na ukaidi, ili watu wa rika zote na wa mahali pote wamtii Mwanao Mfufuka.
3. Utujalie bidii ya kumtafuta Yesu Mfufuka kama alivyofanya Mama Maria Magdalena.
4. Utuimarishe katika imani ya ufufuko na kutufanya watangazaji hodari wa Injili yako.
Maombi yetu yapae kwako Wewe uliye baba yetu na Mungu wetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.