JUMANNE JUMA KUU
MASOMO
SOMO 1: Isa.49:1-6
Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana
ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa
changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa
mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha. Akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli,
ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakni nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure
bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana, na thawabu yangu ina Mungu wangu. Na sasa Bwana
asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli
wakusanyike mbele zake tena. Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo,
na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa
wokovu wangu hata miisho ya dunia.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.71:1-6,15,17(K)15
1. Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe,
Unitegee sikio lako, uniokoe.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki
na wokovu wako.
2. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Nitakakokwenda siku zote.
Umeamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi,
Katika mkono wake mwovu, mdhalimu. (K)
3. Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,
Ninakusifu Wewe daima. (K)
4. Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.
Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu;
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. (K)
SHANGILIO: Amo.5:14
Tafuteni mema,
wala si mabaya, mpate kuishi,
hivyo Bwana, atakuwa pamoja nanyi.
INJILI: Yn.13:21-33,36-38
Pale alipokuwa na mitume wake mezani Yesu alifadhaika rohoni, akashuhudia akisema, Amin, amin,
nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti. Wanafunzi wakatazamana, huku wakiona shaka ni nani amtajaye.
Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda. Basi Simoni
Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye? Basi yeye, hali akimwelekea Yesu kifua
chake, akamwambia, Bwana, ni nani? Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa.
Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Na baada ya hilo tonge Shetani
alimwingia. Basi Yesu akamwambia, Uyatendayo yatende upesi. Wala hakuna mtu katika wale walioketi
chakulani aliyeijua sababu ya kumwambia hivyo. Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua
mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua tunavyohitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu.
Basi huyo, akiisha kulipokea lile tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa ni usiku. Basi huyo
alipokwisha kutoka, Yesu alisema, Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.
Mungu naye atamtukuza ndani ya nafsi yake; naye atamtukuza mara. Enyi watoto wadogo, bado kitambo
kidogo sitakuwa pamoja nayi; mtanitafuta; na kama vile nilivyowaambia Wayahudi ya kwamba, Mimi
niendako ninyi hamwezi kuja; kadhalika sasa nawaambia ninyi. Simoni Petro akamwambia, Bwana,
unakwendapi? Yesu akamjibu, Niendako huwezi kunifuata sasa lakini utanifuata baadaye. Petro
akamwambia Bwana, kwa nini mimi nisiweze kukufuata sasa. Mimi nitautoa uhai wangu kwa ajili yako.
Yesu akamjibu, Je! Wewe utautoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin, nakuambia, Jimbi hatawika
hata wewe utakapokuwa umenikana mara tatu.
MAOMBI
Ndugu, mtumishi wa Bwana yupo tayari kujitoa sadaka, ili kuziinua kabila za Yakobo, na kutufanya nuru
ya mataifa. Tuombe ili tulishiriki vema fumbo hili la ukombozi wetu.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwajalie wote uliowaita tangu tumboni mwa mama zao kuitikia wito wako kila siku na bila masharti yoyote.
2. Wote wenye mamlaka wajaliwe unyenyekevu, ili jina lako litukuzwe siku zote na duniani kote.
3. Utuepushe na tamaa mbaya ya mali au chochote chenye kusababisha usaliti dhidi ya Kristo wako.
4. Utujalie sisi sote, wazima na wafu, kuzifuata nyayo zako huko uendako.
Ee Bwana, mara nyingi tunaahidi kukutumikia kiaminifu na hata kutoa msaada kwa wenzetu. Lakini udhaifu
wetu ndio unaoturudisha nyuma. Utupe ujasiri wa kudumu siku zote katika imani na uaminifu wetu kwako.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.