Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 6 PASAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya

Zab.119:49-56 VII Kuwa na imani na sheria ya Mungu
Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mtumishi wako,*
ahadi ambayo imenipa matumaini.

Hata niwapo taabuni napata kitulizo,*
maana ahadi yako yanipa uhai.

Wenye kiburi hunidharau daima,*
lakini mimi sikiuki sheria yako.

Ninapoyakumbuka maagizo yako ya tangu kale,*
nafarijika, Ee Mungu.

Nashikwa na hasira kali,*
nionapo waovu wakivunja sheria zako.

Nikiwa huku ugenini,*
tenzi zangu ni juu ya amri zako.

Usiku ninakukumbuka, Ee Mungu,*
na kuzingatia sheria zako.

Hii ni baraka kubwa kwangu,*
kwamba nazishika amri zako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.53 Mtu asiyemcha Mungu
Watu wote wametenda dhambi, na wametindikiwa utukufu wa Mungu (Rom.3:23)

Wapumbavu hujisemea: "Hakuna Mungu!"/
Wote wamepotoka, wametenda mambo ya kuchukiza;*
hakuna hata mmoja atendaye jema.

Toka mbinguni Mungu awachungulia wanadamu,/
aone kama kuna yeyote mwenye busara,*
kama kuna mtu yeyote anayemcha Mungu.

Lakini wote wamepotoka,/
wote kwa pamoja wameharibika,*
hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja.

Mungu asema,“Je, hao watendao maovu hawana akili?"*
Wanawamaliza watu wangu,

kama kwamba wanakula mikate;*
tena hawamchi Mungu!"

Hapo, watetemeka kwa hofu,*
hofu ambayo hawajapata kuiona;

maana Mungu ataitawanya mifupa ya adui.*
Hao watashindwa, maana Mungu amewaacha.

Laiti ukombozi wa Israeli*
ungefika kutoka Sion!

Mungu atakapowafanikisha tena watu wake,*
Israeli atafurahi, na Yakobo atashangilia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.54:1-4,6-7 Sala ya kujikinga na maadui
Nabii anaomba ili kwa jina la Bwana aokolewe na uovu wa wale wanaomdhulumu (Kasiani)

Uniokoe, Ee Mungu, kwa jina lako;*
unisalimishe kwa enzi yako.

Uisikie, Ee Mungu, sala yangu;*
uyapokee maneno yangu.

Watu wenye kiburi wananishambulia;/
wakatili wanayawinda maisha yangu,*
watu wasiomjali kamwe Mungu.

Lakini Mungu ni msaada wangu,*
Bwana hutegemeza maisha yangu.

Kwa moyo radhi nitakutolea sadaka;*
nitalisifu jina lako kwa kuwa wewe ni mwema.

Maana umeniokoa katika taabu zangu zote,*
nami nimewaona adui zangu wameshindwa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Mate. 4:11-12
Yesu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema juu yake: 'Jiwe mlilokataa ninyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.' Wokovu haupatikani kwa mwingine ye yote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.

K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: 1Pet.3:21-22a
Ubatizo unawaokoa ninyi sasa. Ubatizo si shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Ubatizo huwaokoeni kwa njia ya ufufuko wa Yesu Kristo, ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu.

K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Kol.3:1-2
Basi, ikiwa mmekufa pamoja na Kristo, panieni mambo ya juu, kule Kristo aliko, amekaa upande wa kulia wa Mungu. Muwe na hamu ya mambo ya huko juu, na siyo mambo ya hapa duniani.

K. Kaa nasi, Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, uwajalie watu wako furaha ya daima kwa kutiwa nguvu mpya rohoni mwao. Wanafurahi kwa sababu umewarudishia utukufu wa kufanywa watoto wako: uwafanye waungojee kwa furaha na matumaini ufufuko ambao hakika wataupata. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.