JUMANNE JUMA LA 6 PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.16:22-34
Siku ile, pale Filipi, wenyeji waliwakamata Paulo na Sila, wakawaendea, makadhi wakawavua nguo
zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa
gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika
chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa
wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula
pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka,
vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza
imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza
sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia
ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu,
yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba
yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake. Akawakaribisha saa ile ile
ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati huo huo. Akawaleta juu
nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha
kumwamini Mungu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.138;1-3,7-8(K)7
1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
(K) Utanyosha mkono, Ee Bwana, utaniokoa.
Au:
Aleluya.
2. Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako,
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)
3. Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu,
Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako. (K)
SHANGILIO: Kol.3:1
Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo,
yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko,
ameketi mkono wa kuume wa dunia.
Aleluya.
INJILI: Yn.16:5-11
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka,
wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwenda wapi? Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa
mioyoni mwenu. Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi
nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye
akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari
ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba,
wala hamnioni tena; kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.
MAOMBI
Wapendwa, maandiko matakatifu yanazidi kututhibitishia kuwa Bwana asipoulinda mji, waulindao
wanakesha bure. Ndiyo kusema, daima na popote tunahitaji msaada wa Mungu katika maisha yetu
ya kila siku. Tuombe:
Kiitikio: Kwa huruma yako, pokea ombi letu.
1. Penye dhuluma, viongozi wa dini wawe mfano mwema kwa kujikabidhi kwako na kutangaza toba
kwa watesi wa Kanisa lako. Ee Bwana.
2. Viongozi na wafanyakazi wa taasisi zote katika jamii wasisahau kumpa Mungu nafasi na utukufu
katika utumishi wao wa kila siku. Ee Bwana.
3. Utuongezee sisi sote matumaini ya kwamba, tukimwamini Bwana wetu Yesu Kristo, tutaokoka. Ee
Bwana.
4. Waliokata tamaa ya maisha wasijidhuru, bali wayakabidhi matatizo yao yote kwako; na uwapokee
kadiri ya mapenzi yako ndugu zetu waliokufani. Ee Bwana.
Ee Mungu, kila mmoja wetu bado anayo mengi ya kukuomba; uyapokee hayo pia na utupe neema ya
kukutambua zaidi na zaidi katika matukio na kazi zetu za kila siku, hasa tulisomapo neno lako
na tuumegapo mkate. Kwa jina la Kristo Bwana wetu. Amina.