JUMANNE JUMA LA 6 PASAKA
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!
Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!
Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!
Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534
2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ
3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.
Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876
4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.
Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.
Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.
Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.
Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.
Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.
Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.
Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7
5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.
Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.
Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal
6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.
Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.
Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750
7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.
Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.
Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.
Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.
Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695
ANT. I: Yatafuteni mambo ya mbinguni, na si ya ulimwengu huu, aleluya.
Zab.49 Upumbavu wa kutegemea mali
Itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni (Mt.19:23)
I
Enyi watu wote, sikilizeni jambo hili!*
Tegeni masikio, nyote mnaoishi duniani;
wote, wakubwa kwa wadogo,*
matajiri na fukara.
Maneno yangu yatakuwa mazito mazito;*
mimi nitasema maneno ya hekima.
Nitategea sikio nisikilize mithali,*
na kufafanua maana yake kwa muziki wa kinubi.
Mimi siogopi wakati wa hatari,*
wakati nizungukwapo na adui;
watu waovu wategemeao mali zao,*
na kujisifia wingi wa utajiri wao.
Hakika binadamu hawezi kujikomboa mwenyewe;*
hawezi kumlipa Mungu gharama ya maisha yake,
maana fidia ya maisha ni kubwa mno.*
Hawezi kutoa kitu chochote kinachotosha,
kimwezeshe aendelee kuishi,*
asipate kuonja kaburi.
Wote wajua kwamba hata wenye hekima hufa,/
wapumbavu, hali kadhalika na watu wajinga.*
Wote huwaachia wengine mali zao.
Makaburi ni makao yao hata milele;/
ni makao yao vizazi hata vizazi;*
ingawa hapo awali walikuwa wamemiliki ardhi.
Binadamu hatadumu katika fahari yake;*
atakufa tu kama mnyama.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Yatafuteni mambo ya mbinguni, na si ya ulimwengu huu, aleluya.
ANT. II: Bwana aliiokoa roho yangu kutoka katika nguvu ya mauti, aleluya.
II
Hayo ndiyo yawapatayo wanaojiamini kipumbavu,*
ndio mwisho wa wale wanaojivunia mali zao.
Watakufa tu kama kondoo,*
kifo kitakuwa mchungaji wao.
Waadilifu wataona fahari juu ya waovu,/
miili yao itakapokuwa ikioza huko kuzimu,*
mbali na nyumba zilizokuwa zao wenyewe.
Lakini mimi, Mungu atanisalimisha;*
ataniokoa na nguvu za kuzimu.
Usihangaike ukiona mtu anatajirika,*
wala mali yake ikiongezeka, zaidi na zaidi.
Atakapokufa hatachukua chochote,*
mali haitashuka kuzimu pamoja naye.
Ajapojikuza katika maisha haya,*
na kusifiwa kwa sababu ya kufanikiwa,
atajiunga tu na wazee wake huko kuzimu,*
ambako giza linatawala milele.
Binadamu hatadumu katika fahari yake.*
atakufa tu kama mnyama.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Bwana aliiokoa roho yangu kutoka katika nguvu ya mauti, aleluya.
ANT. III: Bwana, ukuu na nguvu, utukufu na ushindi ni vyako, aleluya.
WIMBO: Ufu.4:11;5:9,10,12 Wimbo wa waliookolewa
Wewe ni Bwana na Mungu wetu,*
unastahili utukufu na heshima na nguvu;
maana wewe uliumba vitu vyote,/
na kwa matakwa yako*
kila kitu kimepewa uhai na uzima.
Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu*
na kuivunja mihuri yake,
kwa sababu wewe umechinjwa,/
na kwa damu yako umemnunulia Mungu*
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.
Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani/
wamtumikie Mungu wetu,*
nao watatawala duniani.
Mwanakondoo aliyechinjwa*
anastahili kupokea
uwezo, utajiri, hekima,*
nguvu, heshima, utukufu na sifa.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Bwana, ukuu na nguvu, utukufu na ushindi ni vyako, aleluya.
SOMO: 1Pet.2:4-5
Basi, mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa na watu; lakini mbele ya Mungu ni
jiwe teule, na la thamani kubwa. Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya
kiroho, ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea sadaka za kiroho zenye kumpendeza
Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
KIITIKIZANO
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Walipomwona Bwana.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wanafunzi...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Nawaambieni ukweli, ni afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda, Msaidizi hatakuja
kwenu, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Nawaambieni ukweli, ni afadhali kwenu mimi niende zangu, maana
nisipokwenda, Msaidizi hatakuja kwenu, aleluya.
MAOMBI
Tumwombe Kristo, ambaye kwa ufufuko wake anawaimarisha watu wake katika matumaini.
W. Kristo unayeishi milele, utusikie.
Bwana Yesu, damu na maji vilitoka katika ubavu wako uliofunguliwa kwa mkuki;
- uliondolee Kanisa, bi-arusi wako, kila doa la dhambi. (W.)
Mchungaji mwema, uliyefufuka kutoka wafu, ulimkabidhi mtume Petro alichunge kundi lako;
- tunaomba, Papa F... aimarike katika upendo na bidii. (W.)
Ukiwa umesimama kando ya ziwa Galilaya, uliwaelekeza wanafunzi wako hata wakafaulu kuvua samaki
wengi sana;
- uzielekeze kazi za wanafunzi wako siku hizi, na uwapatie baraka zako kwa wingi. (W.)
Uliwatayarishia chakula wanafunzi wako ufukoni mwa ziwa;
- utusaidie tuweze kupata furaha yako katika kuwashughulikia wenzetu. (W.)
Yesu, Adamu wa mwisho, Roho utiaye uzima, uwafanye marehemu wafanane nawe;
- na uikamilishe furaha yao. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Kufuatana na mafundisho ya Bwana wetu, kwa imani na
matumaini tunasali: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, uwajalie watu wako furaha ya daima kwa kutiwa nguvu mpya rohoni mwao. Wanafurahi
kwa sababu umewarudishia utukufu wa kufanywa watoto wako: uwafanye waungojee kwa furaha na matumaini
ufufuko ambao hakika wataupata. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi
na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.