Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 6 PASAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana amefufuka kweli, aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!

Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!

Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!

Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534

2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ

3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.

Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876

4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.

Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.

Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.

Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.

Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.

Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.

Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.

Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7

5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.

Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.

Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal

6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.

Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.

Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750

7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.

Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.

Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.

Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.

Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695

ANT. I: Umeujia Mlima Sion, na mji wa Mungu aliye hai, aleluya.

Zab.43 Sala ya mkimbizi yaendelea
Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani (Yoh.12:46)

Uwe upande wangu, Ee Mungu;*
unitetee haki zangu;

unikinge na watu wanaokuchukia,*
watu waongo na waovu.

Wewe Mungu wangu, uliye nguvu yangu,*
kwa nini umenitupilia mbali?

Mbona naendelea kuteseka,*
nikisumbuliwa na adui zangu?

Upeleke mwanga wako na ukweli wako,*
vipate kuniongoza na kunipeleka kwako;

mpaka kwenye mlima wako mtakatifu, kwenye makao yako.*
Hapo, Ee Mungu, nitakwenda madhabahuni pako;

nitakuja kwako, Ee Mungu, asili ya furaha yangu.*
Nitakusifu kwa kinubi, Ee Mungu, Mungu wangu.

Mbona ninahuzunika hivyo moyoni?*
Kwa nini nahangaika hivyo?

Nitamtumainia Mungu!*
Nitamsifu tena Mungu, mwokozi wangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Umeujia Mlima Sion, na mji wa Mungu aliye hai, aleluya.

ANT. II: Bwana, umeilinda roho yangu isiharibiwe, aleluya.

WIMBO: Isa.38:10-14,17-20 Kihoro cha mgonjwa mahututi; furaha ya aliyepona.

Nalisema, Katika usitawi wa siku zangu/
nitakwenda kuingia malango ya kuzimu;*
Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.

Nalisema, Sitamwona BWANA, yeye BWANA,*
katika nchi ya walio hai;

Sitamwona mwanadamu tena*
pamoja na hao wakaao duniani.

Kao langu limeondolewa kabisa,*
limechukuliwa kama hema ya mchungaji;

Nimekunja maisha yangu kama mfumaji;*
atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi;

Naliomboleza usiku kucha;/
kama simba ameivunja mifupa yangu yote;*
Tangu mchana hata usiku wananimaliza.

Kama mbayuwayu au korongo ndivyo nilivyolia;/
Naliomboleza kama hua;*
macho yangu yamedhoofu kwa kutazama juu;

Ee BWANA, nimeonewa,*
na uwe mdhamini wangu.

Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi*
kwa ajili ya amani yangu;

Lakini kwa kunipenda/
umeniokoa na shimo la uharibifu;*
Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako.

Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu;*
mauti haiwezi kukuadhimisha;

Wale washukao shimoni*
hawawezi kuitarajia kweli yako.

Aliye hai, naam, aliye hai, /
ndiye atakayekusifu, kama mimi leo;*
Baba atawajulisha watoto kweli yako.

BWANA yu tayari kunipa wokovu.*
Basi, kwa vinubi tutaziimba nyimbo zangu,

Siku zote za maisha yetu*
Nyumbani mwa BWANA.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana, umeilinda roho yangu isiharibiwe, aleluya.

ANT. III: Umeijilia nchi na kuistawisha, aleluya.

Zab.65 Wimbo wa shukrani
Sion ieleweke kuwa ni mji wa Mungu (Origen)

Wastahili sifa, Ee Mungu, katika Sion;*
nasi tutakutimizia nadhiri zetu,

maana wewe wasikiliza sala zetu.*
Watu wote watakujia na kukiri dhambi zao:

dhambi zetu zinapotulemea,*
wewe watuondolea.

Heri uliowachagua wakae patakatifu pako,/
Sisi tutashiba kwa mema ya nyumba yako;*
kwa baraka za Hekalu lako takatifu.

Kwa matendo ya ajabu, Ee Mungu, mkombozi wetu,*
wewe watusikiliza na kutupatia ushindi.

Duniani kote na kupita bahari za mbali,*
watu wakutumainia wewe.

Wewe umejawa nguvu tele tele:*
kwa nguvu yako waisimika milima mahali pake,

watuliza mshindo wa bahari na wa mawimbi yake,*
wakomesha ghasia za watu.

Ulimwengu wote washangazwa na matendo yako./
Wasababisha furaha kila mahali,*
toka mashariki hata magharibi.

Wewe waitunza nchi kwa kuinyeshea mvua,/
waijalia rutuba na kuisitawisha;*
mito yake waijaza maji ya mbinguni,

waifanikisha nchi na kuipatia mavuno.*
Hivi ndivyo ufanyavyo:

Mashamba wayanyeshea mvua kwa wingi,*
na kuyalowanisha kwa maji;

ardhi wailainisha kwa manyunyu,*
na kuibariki mimea ichipue.

Wautunukia mwaka wote mema yako,*
kila ulipopitia pamejaa fanaka.

Mbuga za majani zimejaa mifugo,*
milima nayo imejawa furaha.

Malisho yamejaa kondoo,/
mabonde yamefunikwa kwa ngano.*
Kila kitu kinashangilia kwa furaha.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Umeijilia nchi na kuistawisha, aleluya.

SOMO: Mate.13:30-33
Mungu alimfufua Yesu katika wafu. Naye, kwa siku nyingi aliwatokea wale waliofuatana naye kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu wa Israeli. Sisi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema; jambo lile Mungu alilowaahidia babu zetu amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi tulio wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka wafu. Kama ilivyoandikwa katika zaburi ya pili: "Wewe ni mwanangu, leo mimi nimekuwa baba yako“.

KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Baada ya muda mfupi, ulimwengu hautaniona tena; lakini ninyi mtaniona; kwa kuwa ninaishi, nanyi mtaishi, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Baada ya muda mfupi, ulimwengu hautaniona tena; lakini ninyi mtaniona; kwa kuwa ninaishi, nanyi mtaishi, aleluya.

MAOMBI
Tumwombe Mungu Baba, ambaye Mwana wake alipata kuwa Kondoo asiye na hatia, ili aondolee mbali dhambi za ulimwengu.
W. Mungu wa uzima, utuokoe.

Baba, umkumbuke Mwanao, aliyekufa msalabani na kufufuliwa;
- umsikie sasa anapotuombea. (W.)

Tuitupilie mbali chachu ya ubaya na uovu;
- utujalie tuiadhimishe pasaka ya Kristo kwa utakatifu wa kweli. (W.)

Utuwezeshe leo kushinda kila aina ya wivu na ufarakano;
- utusaidie tuweze kuwapatia ndugu zetu kila wanachohitaji. (W.)

Ututie mioyoni mwetu mwamko wa injili yako;
- injili hiyo itutie ari ya kuzishika amri zako leo na sikuzote. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Bwana utukumbuke katika utawala wako, kwa kuwa kwa kufuata mafundisho yako tunasali: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, uwajalie watu wako furaha ya daima kwa kutiwa nguvu mpya rohoni mwao. Wanafurahi kwa sababu umewarudishia utukufu wa kufanywa watoto wako: uwafanye waungojee kwa furaha na matumaini ufufuko ambao hakika wataupata. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.