JUMANNE JUMA 3 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Sef.3:1-2,9-13
Bwana asema: Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa;
hakumwamini Bwana; hakumkaribia Mungu wake. Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate
kuliitia jina la Bwana, wamtumikie kwa nia moja. Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua,
yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu. Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote
uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena
katika mlima wangu mtakatifu. Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la
Bwana. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao;
kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:1-2,5-6,16-17,18,22
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi. (K)
(K) Maskini aliita, Bwana akasikia.
2. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote.(K)
3. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote. (K)
Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Uje, Bwana, wala usikawie;
Uzisamehe dhambi za taifa lako.
Aleluya.
INJILI: Mt.21:28-32
Siku ile Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee: Mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea
yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda,
Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu,
akaenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu
akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu.
Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini,
nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.
MAOMBI
Ee Bwana Yesu uliyeahidi wokovu kwa maskini wote, twakuomba:
Kiitikio: Bwana utusikie, Bwana utusikilize.
1. Umdumishie Askofu wetu F. ari ya kichungaji na ulijalie kundi lako moyo
wa utii, kujirudi na kumkaribia Mwanao Yesu Kristo aliye Bwana na Mkombozi wetu.
2. Mataifa yote watumie lugha safi kuliitia jina lako, wakutumikie kwa nia moja na kukutolea sadaka safi.
3. Utuepushe na ulimi wa hadaa na watu wenye kutuogofya, hasa katika kipindi hiki cha Ujio wa Mwokozi wetu.
4. Utuwashie mapendo ya kweli kwa wakosefu wanaotubu, na tushirikiane nao katika kuitengeneza njia ya Bwana.
Ee Bwana Yesu, uje wala usikawie; uzifute dhambi za taifa lako na kutuokoa katika taabu zetu zote. Unayeishi
na kutawala daima na milele.Amina.