JUMANNE JUMA 33 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 2Mak.6:18-31
Eliazari, mmoja wa waandishi wakuu, mkuu wa umri mkubwa na sura njema, alishurutishwa kufunua kinywa
chake kulishwa nyama ya nguruwe. Lakini akaitema ile nyama, akasogea mwenyewe kwenye mahali pa kuteswa,
akiona afadhali kufa kwa heshima kuliko kwa unajisi. Akatenda kama yampasavyo mtu aliyekaza nia yake
kuvikataa vitu visivyo halali kuonjwa hata kwa kutaka kujiokoa maisha. Basi, wale waliosimamia
dhabihu hiyo haramu, kwa kuwa wamejuana naye kwa miaka mingi walimchukua kando wakamsihi alete
nyama yake mwenyewe, iliyo halali ya kuliwa, na kufanya kana kwamba anaila nyama ya dhabihu, kama
mfalme alivyoamuru. Hivyo atajiponya na mauti, na kutendewa nao kwa hisani kwa sababu ya urafiki
wao wa tangu zamani. Lakini yeye aliikaza nia yake madhubuti, nia iliyostahili umri wake na jadi
yake, na mvi zake stahivu, na mwendo wake wa adili tangu utoto wake katika kuzishika amri takatifu
zilizotolewa na Mungu. Akakataa kabisa, na kuwaambia wampeleke kuzimuni upesi akisema haipatani na
miaka yetu kudanganya, isije vijana wengi wadhani ya kuwa Eliazari, katika mwaka wake wa tisini,
ameicha dini yake kwa dini ya kigeni; na hivyo, kwa sababu ya udanganyifu wangu, watapotoshwa na
mimi mwenyewe nitajipatia unajisi na aibu katika uzee wangu. Na hata nikiepukana na adhabu ya wanadamu
sasa, lakini sitaweza kuepukana na mikono ya Mwenyezi, nikiwa hai au nimekufa. Basi, nikitoa maisha
yangu sasa kwa ushujaa, nitajionyesha kuwa nimestahili miaka yangu mingi, na kuwaachia vijana mfano
wa kufa mauti ya fahari kwa hiari na kwa uthabiti, kwa ajili ya amri takatifu zenye heshima. Alipokwisha
kusema hayo, alipaendea mara mahali pa kuteswa. Nao waliokuwa wakimwonyesha urafiki walibadili nia zako
kwa wabaya kwa sababu ya maneno yake waliyoyaona ya kiwazimu. Naye alipokuwa kufani kwa ajili ya
mapigo yake, aliugua akasema, kwake Bwana ajuaye yote ni dhaniri ya kuwa, ingawa ningaliweza kuepukana
na mauti, lakini ninavumilia maumivu makali mwlini mwangu; hata rohoni mwangu ninayavumilia kwa
furaha kwa sababu ya kicho changu kwake. Hivyo alikufa; na kwa kufa kwake aliacha mfano wa unyofu
na ukumbusho wa wema, si kwa vijana tu, ila kwa jamii yote ya taifa lake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.3:1-6 (K)5
1. Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi,
Ni wengi wanaonishambulia,
Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu,
Hana wokovu huyu kwa Mungu.
(K) Bwana ananitegemeza.
2. Na Wewe, Bwana, U ngao yangu pande zote,
Utukufu wangu na mwinua kichwa changu.
Kwa sauti yangu namwita Bwana
Naye aniitikia toka mlima wake mtakatifu. (K)
3. Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka,
Kwa kuwa Bwana ananitegemeza.
Sitayaogopa makumi elfu ya watu,
Waliojipanga juu yangu pande zote. (K)
SHANGILIO: Mt.11:25
Aleluya, aleluya!
Nakushukuru, Baba,
kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili,
ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya!
INJILI: Lk.19:1-10
Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo,
mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu
wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio,
akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. Na Yesu, alipofika
mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda
nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona,
walinung’unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama, akamwambia
Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa
hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu
naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, tunapaswa kuikiri imani yetu tuwapo katika mazingira yoyote na kwa gharama
yoyote bila unafiki. Tuombe neema ya Mungu tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Viongozi wa Kanisa wazidi kuwahimiza watu wakutafute Wewe kwa gharama yoyote,
wakukaribishe na kupata wokovu kwa imani yao kwako. Ee Bwana.
2. Uwasaidie viongozi wa serikali kusimamia vema raslimali za nchi yetu; ili utajiri
uliopo uwanufaishe hasa wanyonge na wote wenye shida. Ee Bwana.
3. Wazazi wote wazidi kuwa mfano mzuri kwa jamii, wakidumu katika imani safi, mwendo
wa adili katika kuzishika amri takatifu zilizotolewa nawe. Ee Bwana.
4. Sisi sote tudumu katika imani yetu bila unafiki, kwani hata tukiepukana na adhabu
ya wanadamu sasa, hatutaweza kuepukana na mikono yako. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wasamehewe dhambi zao na kupokelewa kwako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetafuta na kuokoa kile kilichopotea, uyapokee maombi yetu. Kwa njia
ya Kristo Bwana wetu. Amina.