JUMANNE JUMA 32 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Hek.2:23-3:9
Mungu alimwumba mwanadamu ilia pate kutokuharibika, kwa mfano wake mwenyewe, ila ulimwengu uliingiwa na muti kwa husuda yake Shetani, nao walio wa upande wake hupata kuionja. Bali roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa. Machoni pa watu walio wajinga walionekana kwamba wamekufa, na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao, na kusafiri kwao kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika Amani. Kwa sababu hata ikiwa (waonavyo watu) wanaadhibiwa, hata hivyo taraja lao limejaa kutokufa, na wakiisha kustahimili kurudiwa kidogo watapokea wingi wa mema. Kwa kuwa Mungu amewajaribu, na kuwaona kuwa wamemstahili, kama dhahabu katika tanuru aliwajaribu, akawakubali mithili ya kafara. Wakati wa kujiliwa kwao watang’aa, na kama vimulimuli katika mabua makavu watametameta. Watahukumu mataifa na kuwatawala kabila za watu; naye Bwana atawamiliki milele na milele. Wenye kumtumaini watafahamu yaliyo kweli, na waaminifu watakaa naye katika upendo; mradi neema na rehema zina wateule wake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:1-2,15-18 (K)1
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

(K) Nitamhimidi Bwana kila wakati.

2. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao, Uso wa Bwana ni juu ya watenda mambaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. (K)

3. Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. (K)

SHANGILIO: Zab.25:4,5
Aleluya, aleluya!
Ee Bwana, unijulishe njia zako,
unifundishe mapito yako.
Aleluya!

INJILI: Lk.17:1-10
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng’ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? Je! Hatamwambia, Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa neema na rehema zina wateule wake Mungu, tumwombe tukisema.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Kwa maongozi ya malaika wako watakatifu, uwape viongozi wetu wa Kanisa roho ya utumishi usio na faida za kidunia. Ee Bwana.

2. Wote wenye mamlaka wawahukumu na kuwatawala watu wao kwa njia za haki, amani na usawa. Ee Bwana.

3. Utukinge na hila za shetani aletaye mauti na utuimarishe katika ushuhuda wa imani iletayo uzima wa milele. Ee Bwana.

4. Sisi sote tujaliwe kuishi kwa kiasi na haki; tukitazamia tumaini lenye baraka ambalo litakuja katika ufunuo wako. Ee Bwana.

5. Uwahurumie marehemu wetu na kuwapatia tuzo la wenye haki, huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayewajalia wakutumainio ufahamu wa ukweli wako, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.