JUMANNE JUMA 31 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.12:5-16
Sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa
tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri
ya Imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kuonya kwake; mwenye
kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia, kwa bidi; mwenye kurehemu, kwa furaha.Pendo na lisiwe
na unafiki; lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi
kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho
zenu; mkimtumikia Bwana; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu;
kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni, mkijitahidi. Wabarikini
wanaowaudhi; barikini, wala msilaani. Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.
Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo
manyonge.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.131
1. Bwana, moyo wangu hauna kiburi,
Wala macho yangu hayainuki.
Wala sijishughulishi na mambo makuu,
Wala na mambo yashindayo nguvu zangu.
(K) Moyo wangu uwe na Amani kwako, Ee Bwana.
2. Hakika nimeituliza nafsi yangu,
Na kuinyamazisha.
Kama mtoto aliyeachishwa
Kifuani mwa mama yake;
Ndivyo roho yangu ilivyo kwangu. (K)
3. Ee Israeli, umtarajie Bwana,
Tangu leo n ahata milele. (K)
SHANGILIO: Zab.147:12,15
Aleluya, aleluya!
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu,
huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya!
INJILI: Lk.14:15-24
Mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja na Yesu alimwambia, Heri yule atakayekula mkate
katika ufalme wa Mungu. Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akaalika watu wengi, akamtuma
mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa
tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti
niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda
kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. Yule
mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika,
akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya miji, ukawalete hapa
maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka,
na hata sasa ingaliko nafasi. Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani,
ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambia ya kwamba katika wale
walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu ndiye mpaji wa neema na karama
mbalimbali. Tumwombe katika shida zetu:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ili wote wanaoitwa kuihubiri Injili na kulihudumia
Kanisa lako wasitoe udhuru, bali waupokee wajibu huo kwa
moyo mkunjufu. Ee Bwana.
2. Ili wote wenye mamlaka serikalini wasione
madaraka kama ni kitu cha kushikamana nacho; bali wawe
watumishi wenye utayari hata wa kutoa uhai wao kwa ajili
ya wengine. Ee Bwana.
3. Ili ndugu, mali au kitu chochote tulichopewa hapa
duniani kitufae kwa wokovu; utuondolee vikwazo kwa miito
yetu. Ee Bwana.
4. Ili kila mmoja wetu atumie kipaji alichonacho kwa
manufaa ya wengine na kwa sifa na utukufu wako. Ee Bwana.
5. Ili marehemu wetu wakaribishwe kwenye karamu ya
uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetupatia mahitaji yetu na kutuongoza
katika kweli yako, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.