JUMANNE JUMA LA 2 PASAKA
MASOMO

SOMO: Mdo.4:32-37
Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji. Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.93:1-2,5(K)1
1. Bwana ametamalaki, amejivika adhama,
Bwana amejivika, na kujikaza nguvu.

(K) Bwana ametamalaki, amejivika adhama.

2. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani;
Wewe ndiwe uliye tangu milele. (K)

3. Shuhuda zako ni amini sana;
Utakatifu ndio uifaao nyumba yako,
Ee Bwana, milele na milele. (K)

SHANGILIO: Yn.10:14
Aleluya, aleluya,
Bwana asema:
mimi ndimi mchungaji mwema;
Nao walio wangu nawajua,
nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.

INJILI: Yn.3:7-15
Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho. Nikodemo akajibu, akamwambia, Yawezaje kuwa mambo haya? Yesu akajibu, akamwambia, Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu? Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali. Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni? Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.

MAOMBI
Ee Mungu, katika Roho wako Mtakatifu avumaye kokote anakopenda twakuomba:

Kiitikio: Mungu Mtukufu, pokea ombi letu.
1. Uwaongezee Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa ujasiri wa kuyanena yale yahusuyo mapenzi yako na kuyashuhudia kwa dhati yote wayajuayo kuhusu ufalme wako.

2. Watawala wa nchi wawasadikishe watu kwa dhati kuhusu ukweli wa mambo ya dunia hii inayopita.

3. Zidisha mioyoni mwa watu tabia ya kuyaishi mafundisho mema ya viongozi wote wenye nia njema.

4. Uwarehemu marehemu wetu na uwashirikishe utukufu wa Yesu mfufuka.

Ee Baba Mwema, uyaelekeze macho ya watu wako kwa Mwanao Mfufuka na Mshindi wa shetani na dhambi; aliyeinuliwa msalabani na kuyashinda mauti, ili kila amwaminiye awe na uzima wa milele. Kwa huyo Kristo Bwana wetu. Amina.