JUMANNE JUMA 2 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Ebr.6:10-20
Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia. Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho; ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu. Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza. Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi. Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha. Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati; ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu; tuliyo nayo kama nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia, alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.111:1-2,4-5,9-10 (K)5
1. Aleluya,
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu,
Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.

(K) Bwana atalikumbuka agano lake milele.
Au:
Aleluya

2. Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;
Bwana ni mwenye fadhili na rehema.
Amewapa wamchao chakula,
Atalikumbuka agano lake milele. (K)

3. Amewapelekea watu wake ukombozi,
Ameamuru agano lake liwe la milele,
Jina lake ni takatifu la kuogopwa,
Sifa zake zakaa milele. (K)

SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atashika neno langu,
na Baba yangu atampenda,
na sisi tutakuja kwake.
Aleluya.

INJILI: Mk.2:23-28
Yesu alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato? Akawaambia, Hamkusoma popote alivyofanya Daudi, alipokuwa ana haja, na kuona njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, zamani za kuhani mkuu Abiathari, akaila mikate ile ya Wonyesho, ambayo si halali kuliwa ila na makuhani, akawapa na wenziwe? Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato. Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, katika malaika wako tunaona fahari kukusifu na kukuomba tukisema.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa wadumu katika kulihudumia Kanisa lako. Ee Bwana.

2. Uwabariki viongozi wa nchi yetu ili watekeleze kiaminifu yale waliyowaahidi raia wao. Ee Bwana.

3. Umjalie kila mmoja wetu kuidhihirisha bidii ya kuliishi neno lako kwa ukamilifu wa matumaini hata mwisho. Ee Bwana.

4. Wewe unaye utazama moyo, na siyo sura ya nje, utupe ari ya kukujia daima kwa amani na upatanisho ili ibada, sadaka na utume wetu vipate kibali mbele zako. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wasamehewe dhambi zao na kushirikishwa uzima wa milele walio utumainia. Ee Bwana.

Ee Bwana Mungu unayetaka tuizingatie roho ya sheria yako iletayo wokovu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.