JUMANNE JUMA 29 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.5:12,15,17-21
Kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu
wote kwa sababu wote wamefanya dhambi; Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa
kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema
yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi. Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu
mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile
kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo. Basi tena, kama kwa kosa moja
watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye
uzima. Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi,
kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki. Lakini sheria
iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi; ili kwamba,
kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima
wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.40:6-9,17 (K)8,9
1. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja,
(K) Tazama nimekuja, Ee Bwana.
Kuyafanya mapenzi yako.
2. Katika gombo la chuo nimeandikiwa,
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
3. Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa.
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)
4. Nami ni maskini na mhitaji,
Bwana atanitunza.
Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu,
Ee Mungu wangu, usikawie. (K)
SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu waisikia sauti yangu,
nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya!
INJILI: Lk.12:35-38
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka;
nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na
kubisha, wamfungulie mara. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin,
nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. Na akija zamu ya
pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa kwa kutii kwake Bwana wetu Yesu
Kristo ulimwengu umepata uzima, tumwombe Mungu
kwa imani na matumaini.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uzibariki juhudi za Maaskofu na Wachungaji wote
wa Kanisa lako wanazozifanya, ili kutetea uhai na
kuzilinda haki za binadamu na mali zao. Ee Bwana.
2. Serikali za mataifa yote zitende haki mintarafu
uhuru wa kuabudu; na kuwa kiungo cha amani na uelewano kati
ya dini au madhehebu yanayofarakana sababu ya ubinafsi. Ee Bwana.
3. Uwaingize watu wengi katika jamii ya wenye haki, ili
nao wapate kutangaza msamaha wako ulimwenguni. Ee Bwana.
4. Kwa neema yako tustahimili kukesha mpaka ajapo
Mwanao, Bwana wetu Yesu Kristo, kwa hukumu yake ya mwisho. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wanaomngoja Bwana wapewe uzima
wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, twayaleta kwako maombi yetu haya. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.