JUMANNE JUMA 27 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Yon.3:1-10
Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu. Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.130:1-4,7-8 (K)3
1. Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia. Bwana, uisikie sauti yangu. Masikio yako na yaisikilize Sauti ya dua zangu.

(K) Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
nani angesimama?

2. Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, Ili Wewe uogopwe. (K)

3. Ee Israeli, umtarajie Bwana; Maana kwa Bwana kuna fadhili, Na kwake kuna ukombozi mwingi. Yeye atamkomboa Israeli na maovu yake yote. (K)

SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,
awape roho ya hekima,
mjue tumaini ya mwito wake.
Aleluya!

INJILI:Lk.10:38-42
Yesu aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu anataka watu wote watende mema kwa moyo mnyofu, wapate kuokoka. Hivyo tuombe msaada wake tukisema.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwatie moyo na ari ya uinjilishaji viongozi wetu wa Kanisa, ili neno lako lipate kupenya mioyo ya watu kwa wakati wake kokote waliko. Ee Bwana.

2. Uamshe ndani ya wote wenye mamlaka hapa duniani roho ya uwajibikaji, na hivi kuwakumbusha watu wao juu ya hasara ya uovu na faida ya kutenda mema. Ee Bwana.

3. Utujalie sisi sote kulipatia neno lako nafasi ya kwanza katika maisha yetu ya kila siku, tupate kukujua na kukutumikia kwa ukarimu hasa katika nafsi za wenzetu wenye shida. Ee Bwana.

4. Uwaamshie roho ya toba wote wanaoliudhi Kanisa lako; kwani twaamini hata hao waweza kuongoka wakawa wahubiri wazuri wa imani hiyo. Ee Bwana.

5. Uwarehemu waliokufani; na marehemu wetu wapewe utukufu wa ufufuko wa Mwanao. Ee Bwana.

Ee Mungu, uliyetualika kulichagua fungu lililo jema na lisiloondolewa kamwe, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.