JUMANNE JUMA 26 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Zek.8:20-23
Bwana wa majeshi asema hivi, Itatokea halafu ya kwamba watakuja mataifa na wenyeji wa miji mingi;
wenyeji wa mji huu watauendea mji huu, wakisema, Haya! Twendeni zetu kwa haraka tuombe fadhili za
Bwana, na kumtafuta Bwana wa majeshi; Mimi nami nitakwenda. Naam, watu wa kabila nyingi na mataifa
hodari watakuja Yerusalemu kumtafuta Bwana wa majeshi, na kuomba fadhili za Bwana. Bwana wa majeshi
asema hivi, Siku hizo watu kumi, wa lugha zote za mataifa, wataushika upindo wa nguo yake yeye aliye
Myahudi; naam, wataushika wakisema, Tutakwenda pamoja nanyi, kwa maana tumesikia kwamba Mungu yu
pamoja nanyi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.87 (K)Ez.8:23
1. Msingi wake upo Juu ya milima mitakatifu.
Bwana ayapenda malango ya Sayuni
Kuliko maskani zote za Yakobo.
Umetajwa kwa mambo matukufu,
Ee Mji wa Mungu.
(K) Mungu yu pamoja nasi.
2. Nitataja Rahabu na Babeli
Miongoni mwao wanaonijua.
Tazama Filisti, na Tiro, na
Kushi; Huyu alizaliwa humo.
Naam, mintarafu Sayuni itasemwa,
Huyu na huyu alizaliwa humo.
Na Yeye Aliye juu Ataufanya imara. (K)
3. Bwana atahesabu, awaandikapo mataifa,
Huyu alizaliwa humo.
Waimbao na wachezao na waseme,
Visima vyangu vyote vimo mwako. (K)
SHANGILIO: Zab.119:105
Aleluya, aleluya!
Neno lako ni taa ya miguu yangu,
na mwanga wa njia yangu.
Aleluya!
INJILI: Lk.9:51-56
Ilikuwa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, Yesu aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu;
akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili
kumtengenezea mahali. Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu.
Wanafunzi wake Yakobo na Yohane walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka
mbinguni, uwaangamize? Akawageukia akawakanya, wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa unyenyekevu tumpelekee Mungu maombi
yetu. Ee Mungu unayetukuka kati ya malaika,
twakuomba.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwajalie Askofu wetu F. na
Wachungaji wote wa Kanisa lako, kutatua matatizo ya watu wako
kwa huruma, upole na uvumilivu. Ee Bwana.
2. Wafalme, washauri na wakuu wa dunia wajaliwe
kuzitumia mali za nchi kwa faida ya raia wote, hasa
wale wenye shida. Ee Bwana.
3. Watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa wakutafute
Wewe, Bwana wa majeshi, na kuomba fadhili zako. Ee Bwana.
4. Uwajalie wafuasi wote wa Kristo kulitangaza jina lako
kwa imani safi na matendo mema, ili wale wasiokujua
bado wapate kujiunga nao.
5. Ndugu zetu marehemu wapewe msamaha wa dhambi
na kuingizwa mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu msamehevu na mwenye kutukuka kati ya
malaika, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.