JUMANNE JUMA 25 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ezr.6:7-8,12,14-20
Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; kama mfereji wa maji huugeuza popote apendapo.
Mfalme Dario alimwandikia liwali wa ng’ambo wa mto, na wenzake; Waacheni liwali wa Wayahudi na
wazee wa Wayahudi, waijenge nyumba hii ya Mungu mahali pake. Tena, natoa amri kuwaagiza ninyi
mtakayowatendea wazee hao wa Wayahudi kwa kazi hii ya kuijenga nyumba ya Mungu; katika mali ya
mfalme, yaani, katika kodi za nchi iliyo ng’ambo ya Mto, watu hao wapewe gharama zote kwa bidii,
ili wasizuiliwe. Na Mungu huyu, aliyelifanya jina lake likae pale, na aangamize wafalme wote, na
watu wote, watakonyosha mikono yao kulibadili neno hili, na kuiharibu nyumba hii ya Mungu,
iliyoko Yerusalemu. Mimi, Dario, nimetoa amri; na ifanyike kwa bidii nyingi. Nao wazee wa Wayahudi
wakajenga, wakafanikiwa, kwa masaada wa kuhubiri kwao Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido.
Wakajenga, wakaimaliza kazi yao, kwa maagizo ya Mungu wa Israeli, na kwa amri ya Koreshi, na
Dario, na Artashasta mfalme wa Uajemi. Nyumba hiyo ikamalizika siku ya tatu ya mwezi Adari,
katika mwaka wa sita wa kutawala kwake mfalme Dario. Na wana wa Israeli, na makuhani, na walawi
na watu wengine katika hao waliohamishwa, wakaiweka wakfru nyumba ya Mungu kwa furaha. Na katika
kuiweka wakfu nyumba ya Mungu, wakatoa sadaka, ng’ombe mia, na kondoo waume mia mbili, na wanakondoo
mia nne; tena wakatoa mbuzi waume kumi na wawili, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli wote,
kwa hesabu ya kabila za Israeli. Wakawaweka makuhani katika kura zao, wakawaweka na Walawi
vilivyoandikwa katika chuo cha Musa. Kisha, wana wa uhamisho wakaifanya Pasaka, mwezi wa kwanza,
siku ya kumi nan ne ya mwezi. Kwa maana makuhani na Walawi walikuwa wamejitakasa wote pamoja; wote
walikuwa hali ya tohara; wakachinja pasaka kwa ajili ya wana wote wa uhamisho, na kwa ajili ya ndugu
zao makuhani, na kwa ajili ya nafsi zao.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:1,27,30,34-35,44(K)35
1. Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
(K) Nalifurahi waliponiambia,
na twende nyumbani kwa Bwana.
2. Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, ee Yerusalemu!
Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ulioshikamana. (K)
3. Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana;
Ushuhuda wa Israeli,
Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. (K)
SHANGILIO: 1Pet.1:25
Aleluya, aleluya!
Neno la Bwana hudumu hata milele,
na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya!
INJILI: Lk.8:19-21
Walimwendea Yesu mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano. Akaletewa
habari akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe. Akawajibu
akasema, Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Mungu aliyetuita katika imani na
anayetawala maisha yetu tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Umjalie Askofu wetu F. na Wachungaji wote wa
Kanisa lako kuwaimarisha waamini wao, katika
kufundisha imani na kuadhimisha mafumbo ya
ukombozi. Ee Bwana.
2. Ubariki juhudi za wote wenye mamlaka,
wanaoshirikiana na Wachungaji wako, katika
kuifanikisha kazi ya ukombozi wa watu wako. Ee Bwana.
3. Tunakushukuru kwa zawadi ya imani uliyotujalia,
na tunaomba utusaidie kudumisha udugu na umoja
katika Kristo Mwanao. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wajasiriamali wote, ili wasitafute
utajiri ila mahitaji; na akiba yao halali iwe fadhili
kwa jirani mwenye shida. Ee Bwana.
5. Uwakaribishe ndugu zetu marehemu kwenye makao
yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayependa tukae pamoja kama ndugu na
kulisikiliza neno lako, uyapokee maombi yetu. Kwa njia
ya Kristo Bwana wetu. Amina.