JUMANNE JUMA 24 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1Tim.3:1-13
Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu
asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye
kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala
asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu;
(yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) Wala asiwe
mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa
mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi. Vivyo hivyo mashemasi na
wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana,si watu wanaotamani fedha ya
aibu. wakiishika siri ya imani katika dhamiri safi. Hawa pia na wajaribiwe kwanza; baadaye waitende
kazi ya shemasi, wakiisha kuonekana kuwa hawana hatia. Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si
wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote. Mashemasi na wawe waume wa mke mmoja,
wakiwasimamia watoto wao vizuri, na nyumba zao. Kwa maana watendao vema kazi ya shemasi hujipatia
daraja nzuri, na ujasiri mwingi katika imani iliyo katika Kristo Yesu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.100:1-3,5-6 (K)2
1. Rehema na hukumu nitaziimba,
Ee Bwana, nitakuimbia zaburi.
Nitaiangalia njia ya unyofu;
Utakuja kwangu lini?
(K) Nitakwenda kwa unyofu wa moyo.
2. Nitakwenda kwa unyofu wa moyo
Ndani ya nyumba yangu.
Sitaweka mbele ya macho yangu
Neno la uovu. (K)
3. Amsingiziaye jirani yake kwa siri,
Huyo nitamharibu.
Mwenye macho ya kiburi na moyo wa majivuno,
Huyo sitavumilia naye. (K)
SHANGILIO: Lk.7:16
Aleluya, aleluya!
Nabii mkuu ametokea kwetu;
na Mungu amewaangalia watu wake.
Aleluya!
INJILI: Lk.7:11-17
Yesu alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na
mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni
mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana
alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa
wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi,
akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii
mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi
wote, na katika nchi zote za kando kando.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu Baba, malaika wanayalinda maisha yetu hapa
duniani. Hata hivyo, Wewe wabaki kuwa Mkuu kuliko
vitu vyote. Na hivyo twakuomba:-
Kiitikio: Upokee sala yetu.
1. Umjalie Askofu wetu F. kudumisha fadhila ya
upendo wa kweli na uaminifu kwa Jimbo lake na
kwa Kanisa kwa ujumla. Ee Bwana.
2. Tunawaombea viongozi wote, wapate kuheshimiana
na kusaidiana; ili karama zao ziwe kwa
manufaa ya watu wao. Ee Bwana.
3. Wote walio katika malezi, wajaliwe kujiandaa vema
hatua kwa hatua; waijue vema miito yao na kuishika
siri ya imani katika dhamiri safi. Ee Bwana.
4. Utujalie kumwendea Mwanao Yesu Kristo kwa imani
na matumaini ya kusaidiwa katika matatizo yetu ya
kimwili na kiroho. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wajaliwe kukujia Wewe kwenye
ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka kila mmoja wetu atimize kiaminifu
ahadi au viapo vya wito wake, uyapokee maombi yetu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.