JUMANNE JUMA 23 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kol.2:6-15
Kama mlivyompokea Kristo Yesu Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa
katika yeye; mmefanywa imara kwa Imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu
asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa
jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Maana katika yeye unakaa
utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha
enzi yote na mamlaka. Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili
wa nyama, kwa tohara ya Kristo. Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja
naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu. Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya
makosa yenu na kutotahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote.
Akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa kwa kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu;
akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa
mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.145:1-2,8-11 (K)9
1. Ee Mungu wangu Mfalme, nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele,
Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
(K) Bwana ni mwema kwa watu wote.
2. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. (K)
3. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako. (K)
SHANGILIO: Zab.111:7,8
Aleluya, aleluya!
Maagizo yako yote, Ee Bwana,
ni amini, yamethibitika milele na milele.
Aleluya!
INJILI: Lk.6:12-19
Yesu aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata
kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao
aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohane,
na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote,
na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti. Akashuka pamoja nao, akasimama
mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi
wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao;
na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa,
kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Bwana wetu Yesu Kristo tuliyempokea
ametufanya hai na imara kwa imani. Tunamshukuru
pamoja na malaika watakatifu na kumwomba:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwajalie Baba Mtakatifu F.,
Askofu wetu F. na
Mapadre wote ambao ni warithi wa kazi ya mitume
kuutimiza wajibu huo mkubwa, ili watu wakujue na
kukuongokea Wewe. Ee Bwana.
2. Viongozi wa serikali waunge mkono juhudi za
wahubiri wa neno lako kukemea dhuluma, wizi,
ulevi, unyang'anyi na madhambi yote. Ee Bwana.
3. Malaika wako wawalinde wafuasi wa Mwanao Yesu
Kristo dhidi ya mafundisho potofu, na wawaongoze
kunako ukweli. Ee Bwana.
4. Utujalie sisi sote kutekeleza wajibu wa kuwa mitume
miongoni mwetu, ili watu wapate kumjua Mwanao
Yesu Kristo na kusaidiwa katika matatizo yao. Ee
Bwana.
5. Uwaponye wenye kuonewa na ibilisi na uwape marehemu
wetu uzima wa milele mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetaka sala ituunganishe sisi na Wewe,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.