JUMANNE JUMA 22 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1The.5:1-6,9-11
Ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini
ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama,
ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.
Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa
wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine,
bali tukeshe, na kuwa na kiasi. Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu, kwa
Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, kwamba twakesha au
kwamba twalala. Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.27:1,4,13-14 (K)13
1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
katika nchi ya walio hai.
2. Neno Moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K).
3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)
SHANGILIO: 2The.1:10
Aleluya, aleluya!
siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake
na heshima kutoka kwa wote wanaoamini.
Aleluya!
INJILI: Lk.4:31-37
Yesu alishuka mpaka Kapernaumu, mji wa Galilaya, akawa akiwafundisha siku ya sabato; wakashangaa
mno kwa mafundisho yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo. Na ndani ya sinagogi mlikuwa na
mtu mwenye roho ya pepo mchafu, akalia kwa sauti kuu, akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa
Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema,
Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno. Mshangao
ukawashika wote, wakasemezana wakisema, Ni neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa
uwezo na nguvu, nao hutoka. Habari zake zikaenea kila mahali katika nchi ile.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, malaika wanakutumikia daima huko
mbinguni. Kwa vile nasi twatamani kufika huko
waliko, tunakuomba tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Askofu wetu F. na wahubiri wote wa neno
lako kuwakumbusha watu, kwamba siku yako
itakuja ghafla kama mwivi. Ee Bwana.
2. Ubariki juhudi za viongozi wetu wa serikali, ili kazi
zao njema zitufae sisi sote. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kujiandaa vema kwa ujio wako
Bwana siku ya mwisho ili, hata ukija ghafla, utukute
tukikesha katika nuru yako. Ee Bwana.
4. Roho wako anayeyachunguza yote, awajalie
wanaoutafuta ukweli kutambua kuwa yanayofundishwa
na Roho hufasiriwa kwa maneno ya rohoni. Ee Bwana.
5. Uwaponye wagonjwa wetu, uwafukuze pepo
wabaya, na uwajalie ndugu zetu marehemu
uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tukeshe na kuwa na kiasi, uipokee
sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.