JUMANNE JUMA 19 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kum.31:1-8
Musa alienda akawaambia Waisraeli maneno haya yote. Akawaambia, Mimi leo ni mwenye miaka mia na
ishirini; siwezi tena kutoka na kuingia, na Bwana ameniambia, Hutavuka mto huu Yordani. Bwana Mungu
wako, ndiye atakayevuka mbele yako, atawaangamiza mataifa haya mbele yako, nawe utawamiliki; na
Yoshua atavuka mbele yako, kama Bwana alivyonena. Na Bwana atawatenda hao kama vile alivyowatenda
Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, na nchi yao, ambao aliwaharibu. Naye Bwana atawatia mikononi
mwenu, nanyi mtawatenda kadiri ya amri ile niliyowaamuru. Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope
wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia
wala kukuacha. Musa akamwita Yoshua, akamwambia machoni pa Israeli wote, Uwe hodari na moyo wa
ushujaa, maana utakwenda pamoja na watu hawa hata nchi Bwana aliyowaapia baba zao, ya kwamba
atawapa; nawe utawarithisha. Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe,
hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.
WIMBO WA KATIKATI: Kum.32:3-4,7-9,12 (K)9
1. Maana nitalitangaza Jina la Bwana;
Mpeni ukuu Mungu wetu.
Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu;
Maana, njia zake zote ni haki.
(K) Sehemu ya Bwana ni watu wake
2. Kumbuka siku za kale,
Tafakari miaka ya vizazi vingi;
Mwulize baba yako, naye atakuonyesha;
Wazee wako, nao watakuambia. (K)
3. Yeye Aliye Juu alipowapa mataifa urithi wao,
Alipowabagua wanadamu,
Aliweka mipaka ya watu
Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli. (K)
4. Maana, sehemu ya Bwana ni watu wake,
Yakobo ni kura ya urithi wake.
Bwana peke yake alimwongoza,
Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye. (K)
SHANGILIO: Yn.15:15
Aleluya, aleluya!
Bwana asema
mimi nimewaita nyinyi rafiki,
kwa sababu nimewajulisha yote
ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu.
Aleluya!
INJILI: Mt.18:1-5,10,12,14
Wanafunzi walimwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita
mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto,
hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto
huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano
wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi. Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana
nawaambia ya kwamba malaika zao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.
Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda
milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Vivyo hivyo haipendezwi mbele za Baba yenu aliye mbinguni
kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu wapendwa, tunahitaji unyenyekevu kama ule wa
watoto wadogo, na msaada wa malaika wa mbinguni.
Basi, tuombe neema ya Mungu:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Malaika wako wamlinde Baba Mtakatifu wetu F.
na Maaskofu wote, ili wawafikishe waamini
wako huko mbinguni. Ee Bwana.
2. Uwajalie uhodari na moyo thabiti wote wenye
dhamana ya kupigania haki, ukweli na amani hapa
duniani. Ee Bwana.
3. Wabatizwa wote waone fahari ya kulisoma na
kulitafakari neno lako kama chakula chao cha kila
siku, wapate kukua katika imani na roho ya
umisionari. Ee Bwana.
4. Sisi sote tujaliwe kuitumia fadhila ya unyenyekevu;
tuone fahari kuwahudumia wenye shida, na hivi
kujiwekea hazina mbinguni. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wasipotee; bali wafike salama
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetupatia malaika watulinde na kutuongoza
ili tusipotee, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.