JUMANNE JUMA 18 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Hes.12:1-13
Miriamu na Haruni walimnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa
amemwoa mwanamke Mkushi. Wakasema, Je! ni kweli Bwana amenena na Musa tu? hakunena na sisi pia?
Bwana akasikia maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote
waliokuwa juu ya uso wa nchi. Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia,
Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje. Bwana akashuka
katika nguzo ya wingu, akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka
nje wote wawili. Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana,
nitajifunua kwake katika maono, nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa;
yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; kwake nitanena mdomo kwa mdomo, maana, waziwazi wala si
kwa mafumbo; na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa kumnenea mtumishi wangu,
huyo Musa? Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu likaondoka kutoka
pale juu ya Hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia
Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma. Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu. nakusihi sana
usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi. Nakusihi, asiwe kama
mmoja aliyekufa, ambaye nyama ya mwili wake nusu imelika hapo atokapo tumbo la mama yake. Musa
akamlilia Bwana, akasema, Mpoze, Ee Mungu, nakusihi sana.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.51:1-5,10-11 (K)1
1. Ee Mungu unirehemu, sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
uyafute makosa yangu.
(K) Ee Mungu uturehemu, kwa kuwa tumefanya dhambi.
2. Unioshe kabisa na uovu wangu,
unitakase dhambi zangu.
Maana nimejua mimi makosa yangu,
na dhambi yangu i mbele yangu daima. (K)
3. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo,
Na kuwa safi utoapo hukumu.
Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu;
Mama yangu alinichukua mimba hatiani. (K)
Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)
Shangilio: Zab.19:8
Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru.
Aleluya.
INJILI: Mt.15:1-2,10-14
Ndipo Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema, Mbona wanafunzi wako
huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. Akawaita makutano akawaambia
Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani
ndicho kimtiacho mtu unajisi. Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa
Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa? Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba
yangu wa mbinguni litang'olewa. Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza
kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.
AU
INJILI: Mt.14:22-36
Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo,
wakati yeye alipokuwa akiwaaga makutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani
faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha
kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati
wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona
akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu akanena,
akawaambia, Jipeni moyo; ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe,
niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu
ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo. akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe,
akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani
haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo
wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu. Na walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya
Genesareti. Na watu wa mahali pale walipomtambua, walituma watu kwenda nchi zile zilizo kandokando,
wakamletea wote waliokuwa hawawezi; nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu; na wote
waliogusa wakaponywa kabisa.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, kwa imani na matumaini tumwombe Mungu
anayewapa watu utakatifu kama ule wa malaika.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wetu wa Kanisa wazidi kukutambulisha
Wewe kwa watu na kuwatangazia neno lako wokovu. Ee Bwana.
2. Uwajalie wote wenye madaraka roho ya kuyapambanua
mambo vizuri, wapate kuwatendea haki watu wanaowategemea. Ee Bwana.
3. Utuepushe sisi sote na ukorofi au ubishi wa bure,
na kutuamshia imani ya kweli na moyo wa toba. Ee Bwana.
4. Utujalie marafiki wa kweli, wenye kutufaa wakati
wa raha na taabu, tupate kuwa watu wako; nawe upate kuwa Mungu
wetu pekee. Ee Bwana.
5. Uwaponye wagonjwa; na marehemu wetu wajaliwe
uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, malaika wanaotuongoza kwenye utakatifu
wayapeleke maombi yetu mbele zako. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.