JUMANNE JUMA 17 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.33:7-11;34:5-9,28
Desturi ya Musa, ilikuwa kuitwaa ile hema, na kuikita nje ya marago mbali na hayo marago; akaiita,
Hema ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa Bwana, akatoka, akaenda hata hema ya
kukutania, iliyokuwa nje ya marago. Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka
wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani. Ikawa
Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye Bwana
akasema na Musa. Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka
wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake. Naye Bwana akasema na Musa uso kwa uso. kama vile mtu
asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumish wake Yoshua, mwana wa
Nuni, naye ni kijana hakutoka mle hemani. Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimam; pamoja naye
huko, akalitangaza jina la Bwana Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana Bwana, Mungu mwingi wa
huruma, mwenye fadhili si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli mwenye kuwaonea huruma watu
elfu elfu. Mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana
hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha
tatu na cha nne. Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu. Akasema, Ikiwa
sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana ni watu wenye shingo
ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako. Naye alikuwa pamoja na Bwana
siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao,
hayo maneno ya maagano. hizo amri kumi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.103:6-13 (K)8
1. Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki,
na hukumu kwa wote wanaoonewa.
Alimjulisha Musa njia yake,
wana wa Israeli matendo yake.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
2. Bwana amejaa huruma na neema,
haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Yeye hatateta sikuzote,
wala hatashika hasira yake milele. (K)
3. Hakututenda sawasawa na hatia zetu,
wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.
Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao. (K)
SHANGILIO: 2Tim.1:10
Aleluya, aleluya!
Mwokozi wetu Yesu Kristu alibatili mauti,
na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili.
Aleluya!
INJILI: Mt.13:36-43
Yesu aliwaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie
mfano wa magugu ya kondeni. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu;
lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule
mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika.
Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa
dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa
katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong’aa
kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu uliyenena kwa njia ya malaika na manabii
wako na kuwaahidia watu wako msamaha wa dhambi,
twakuomba:-
Kiitikio: Utujalie huruma yako.
1. Malaika wako wawalinde kwa namna ya pekee Baba
Mtakatatifu wetu F. na
Maaskofu wetu wote, dhidi ya maadui wafanyao maasi
kwa Kanisa lako. Ee Bwana.
2. Ubariki juhudi za viongozi wetu za kuwapa watu
maarifa, kuzuia mauaji, kupambana na njaa,
magonjwa na maafa mbalimbali; ili kuondoa
fadhaa, kudumisha amani na kulitukuza jina lako.
Ee Bwana.
3. Uwashukie na kuwaonya waovu wote wenye shingo
ngumu, wanaopingana na utawala wako hapa duniani.
Ee Bwana.
4. Uzilinde mbegu njema ulizozipanda mioyoni mwetu,
zipate kuzaa matunda ya wokovu. Ee Bwana.
5. Uwapokee marehemu wetu, ili wapate kung'aa
kama jua kwenye ufalme wako huko mbinguni. Ee
Bwana.
Tunaomba hayo yote kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.