JUMANNE JUMA 15 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.2:1-15
Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi aliondoka akaoa binti mmoja wa Lawi. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa
mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. Na alipokuwa hawezi kumficha tena,
akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika
majani kando ya mto. Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. Basi binti Farao akashuka,
aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani,
akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. Akaifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia.
Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. Basi umbu lake mtoto akamwambia
binti Farao, Je! niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto
huyu? Binti Farao akamwambia, Haya! enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. Binti
Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke
akamtwaa mtoto, akamnyonvesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita
jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini. Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima,
akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa
ndugu zake. Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule,
akamficha ndani ya mchanga. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa
wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake. Mbona unampiga mwenzako? Yule akasema, Ni nani
aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule
Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! jambo lile limejulikana. Basi Farao alipopata habari, akataka
kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na
kisima.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.69:3,14,30-31,33-34 (K)32
1. Uniponye kwa kunitoa matopeni,
Wala usiniache nikazama
Na niponywe nao wanaonichukia,
Na katika vilindi vya maji.
(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe,
kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji.
2. Wakanipa uchungu kuwa chakula changu;
Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki.
Meza yao mbele yao na iwe mtego;
Naam, wakiwa salama na iwe tanzi. (K)
3. Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
Nami nitamtukuza kwa shukrani.
Nayo yatampendeza Bwana kuliko ng’ombe,
Au ndama mwenye pembe na kwato. (K)
4. Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafunga wake.
Mbingu na nchi zimsifu,
Bahari na vyote viendavyo ndani yake. (K)
SHANGILIO: Zab.119:18
Aleluya, aleluya!
Unifumbue macho yangu niyatazame,
maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya!
INJILI: Mt.11:20-24
Yesu alianza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa
sababu haikutubu. Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika
kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.
Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu
kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa
kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.
Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu
kuliko wewe.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, tumwombe Mungu anayetulinda kwa njia ya
malaika tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Malaika wako watakatifu wawalinde kwa namna ya
pekee Maaskofu na viongozi wetu wa Kanisa,
wanaofundisha imani sahihi na kuilinda. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia wazuie sera zenye ubaguzi wa
aina yoyote na kutoruhusu aina yoyote ya utumwa.
Ee Bwana.
3. Sisi sote tuwe na upendo usio na mipaka; na utujalie
moyo wa unyenyekevu na ari ya kuacha dhambi tunazotenda
mara kwa mara. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wote waliofarakana na kukosa
amani, ili watulie, wasiogope wala wasife moyo;
bali wakutegemee Wewe. Ee Bwana.
5. Uwapokee kwako mbinguni ndugu zetu wote waliofariki
dunia wakiwa na imani kwako. Ee Bwana.
Ee Mungu, malaika wanaokuja kukusifu wapeleke pia
sala zetu mbele yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.