JUMANNE JUMA 14 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.32:23-33
Yakobo aliondoka usiku ule akawatwaa wakeze wawili, na vijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja,
akavuka kivuko cha Yaboki. Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote alivyokuwa navyo. Yakobo
akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Naye alipoona ya kuwa hamshindi,
alimgusu panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye.
Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki. Akamwuliza, Jina
lako n’nani? Akasema, Yakobo. Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana
na Mungu, na watu, nawe umeshinda. Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema,
Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko. Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema,
Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi vangu imeokoka. Jua likamzukia akivuka Penueli, akachechemea
kwa sababu ya paja la mguu wake. Kwa hiyo wana wa Israeli hawali ule mshipa ulio katika uvungu wa paja
hata leo; maana alimgusa Yakobo panapo uvungu wa paja katika mshipa wa kiuno.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.17:1-3,6-8,15 (K)15
1. Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo ya hila.
(K) Nikutazame uso wako katika haki.
2. Hukumu yangu na itoke kwako,
Macho yako na yatazame mambo ya adili.
Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku,
Umenihakikisha usione neno;
Nimenuia kinywa changu kisikose. (K)
3. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie neno langu.
Dhihirisha fadhili zako za ajabu,
Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia;
Kwa mkono wako wa kuume
Uwaokoe nao wanaowaondokea. (K)
4. Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
mimi nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako. (K)
SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu waisikia sauti yangu,
nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya!
INJILI: Mt.9:32-39
Walimletea Yesu mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastaajabu,
wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wowote. Lakini Mafarisayo wakasema, Kwa nguvu za
mkuu wa pepo atoa pepo. Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika
masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.
Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio
na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache.
Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apelike watenda kazi katika mavuno yake.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, pamoja na uhodari wao, malaika wanalishika neno
la Mungu. Nasi tuombe neema yake Mungu tukisema.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Umjalie Baba Mtakatifu F. na viongozi wote wa
Kanisa lako uhodari, katika kuzikabili changamoto
zote zinazolikumba Kanisa katika ulimwengu wa
sasa. Ee Bwana.
2. Uwaonye walimwengu wanaodiriki kulikufuru jina
lako na uwaongoe, ili waanze maisha mapya
yenye imani katika nguvu yako kuu dhidi ya dhambi,
shetani na mauti. Ee Bwana.
3. Uwajalie vijana wengi kuitikia wito wako kila siku;
na wale uliokwisha wateua kuwa watangazaji wa
Injili yako, wadumu kiaminifu katika utume huo.
Ee Bwana.
4. Utujalie kuzitumia fedha na raslimali zetu kulijenga
Kanisa na kulitukuza jina lako; na siyo kusababisha
machafuko au maabudu ya sanamu. Ee Bwana.
5. Uwapokee ndugu zetu marehemu kwenye makao
yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, pamoja na malaika wako twayaleta maombi yetu kwako.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.