JUMANNE JUMA 11 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: 2Kor.8:1–9
Ndugu zetu, twaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu. Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu. Hata tukamwonya Tito kuwatimilizia neema hii kwenu kama vile yeye alivyotangulia kuianzisha. Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.146:2,5–9 (K)2
1. Ee nafsi yangu umsifu Bwana Nitamsifu Bwana muda ninaoishi, Nitamwimbia Mungu wangu ningali hai.

(K) Ee nafsi yuangu, umsifu Bwana.

2. Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, Na tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake, Aliyezifanya mbingu na nchi, Bahari na vitu vyote vilivyomo. (K)

3. Huishika kweli milele, Huwafanyia hukumu walioonewa, Huwapa wenye njaa chakula, Bwana hufungua waliofungwa. (K)

Bwana huwafumbua macho waliopofuka, Bwana huwainua walioinama, Bwana huwapenda wenye haki Bwana huwahifadhi wageni, Huwategemeza yatima na mjane. (K)

SHANGILIO: Ebr.4:12
Aleluya, aleluya!
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu,
li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya!

INJILI: Mt.5:43-48
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, tukiongozwa na neno la Mungu linalotufunulia namna nyingi za kupata ukamilifu, tumwombe Mungu neema yake:-

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Kwa ajili ya viongozi wa Kanisa, ili wadumu katika kuwahubiria watu wako umuhimu wa pendo lako la kimungu, wapate kuwa watakatifu kama Wewe. Ee Bwana.

2. Serikali yetu iwajibike kwa wakati na ipasavyo, katika kuwanusuru wote wanaokumbwa na majanga mbalimbali hapa nchini. Ee Bwana.

3. Uamshe moyo wa toba kwa watenda mabaya, wapate kupokea msamaha wako na kuirudisha amani na haki duniani. Ee Bwana.

4. Utujalie kutoa michango yetu kwa ukarimu, kadiri ya hali yetu, kwa ajili ya wenzetu wenye shida. Ee Bwana.

5. Uwakaribishe katika makao yako ya milele huko mbinguni ndugu zetu wote waliofariki dunia. Ee Bwana.

Ee Mungu, uyapokee maombi yetu; hata yale yaliyo bado mioyoni mwetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.