JUMANNE JUMA 10 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 2Kor.1:18–22
Kama Mungu alivyo mwaminifu, neno letu kwenu si Ndiyo na siyo. Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu,
aliyehubiriwa katikati yenu na sisi, mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na siyo; bali katika
yeye ni Ndiyo. Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye
ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi. Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Krito, na
kututia mafuta, ni Mungu, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:129–133,135 (K)135
1. Shuhuda zako ni za ajabu,
Ndiyo maana roho yangu imezishika.
Kufafanusha maneno yako kwatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga.
(K) Umwangazie mtumishi wako uso wako.
2. Nalifunua kinywa changu nikatweta,
Maana naliyatamani maagizo yako.
Unigeukie, unirehemu mimi,
Kama iwahusuvyo walipendao jina lako. (K)
3. Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako,
Uovu usije ukanimiliki.
Umwangazie mtumishi wako uso wako,
Na kunifundisha amri zako. (K)
Shangilio: Zab.19:18
Aleluya, aleluya.
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru.
Aleluya.
INJILI: Mt.5:13-16
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa
nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya
ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini
ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na
iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, huku jeshi la malaika watakatifu likiusifu
utukufu wako, twakuomba.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa
wawe chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, ili
Wewe Mungu upate kutukuzwa kwa mfano wa maisha
yao matakatifu. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka katika jamii zetu watoe majibu
ya kweli na kwa wakati wa kufaa, ili kuboresha maisha
ya watu wako. Ee Bwana.
3. Kila mmoja wetu awajibike kutimiza wajibu wake
kiaminifu, na hivi kuwa kama chumvi na nuru ya
ulimwengu kwa matendo mema. Ee Bwana.
4. Muujiza aliotendewa mwanamke mjane wa Sarepta
utukumbushe daima kuwa kutoa ni moyo, wala siyo
utajiri; na kwamba kila mmoja atalipwa kadiri ya
matendo yake. Ee Bwana.
5. Uwageukie na uwarehemu marehemu wetu, wapate
kuiona nuru yako iangazayo milele huko mbinguni.
Ee Bwana.
Ee Mungu, malaika wako watakatifu waipeleke mbele
yako sala yetu hii. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.