JUMAMOSI KUU MKESHA WA PASAKA
MASOMO
Mbiu ndefu ya Pasaka
Sasa jeshi la Malaika wa mbinguni na wafurahi: wafurahi watumishi wa kimungu: na panda ya
wokovu ipigwe kutangaza ushindi wa Mfalme mkuu. Nayo nchi iliyoangazwa na nuru kubwa sana
ifurahi: na kwa kuwa imemulikwa na mwangaza wa Mfalme wa milele, itambue ya kuwa imeondokewa
na giza la ulimwengu.
Naye mama Kanisa aliyepambwa vizuri kwa taa nyingi zenye kuwaka, afurahi:
na sauti za watu zivume katika ukumbi huu.
(Basi ndugu zangu wapendwa sana, mnaosimana hapa, katika nuru kubwa ya mwanga huu mtakatifu,
tafadhali mwombe pamoja nami huruma ya Mungu mwenyezi.
Yeye aliyependa kuniweka miongoni mwa Walawi ingawa sistahili, aniangaze nuru ya mwanga wake
na aniwezeshe kutangaza mbiu ya sifa ya mshumaa huu).
(M/. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.)
M/. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
M/. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki tuziimbe sifa za Mungu, Baba mwenyezi asiyeonekana, na za Mwanawe pekee,
Bwana wetu Yesu Kristo, kwa mapendo yote ya moyo na akili na kwa huduma ya sauti.
Yeye alitulipia deni la Adamu kwa Baba wa milele, na kwa damu yake takatifu akafuta hati ya mashtaka
ya ile dhambi ya kale.
Hakika hii ndiyo sikukuu ya Pasaka, anapochinjwa yule Mwanakondoo halisi, ambaye kwa damu yake
milango ya waamini inawekwa wakfu.
Huu ndio usiku, ulipowatoa Misri mara ya kwanza baba zetu, wana wa Israeli, ukawavusha pakavu
katika Bahari ya Shamu. Huu basi ndio usiku, ulioondoa giza la dhambi kwa nuru ya ile nguzo ya moto.
Huu ndio usiku, ambapo leo popote duniani wenye kumwamini Kristo wanatengwa na maovu ya dunia na
giza la dhambi, wanarudishiwa naye neema na kushirikishwa utakatifu.
Huu ndio usiku, ambapo Kristo alikata minyororo ya mauti, akatoka kuzimu ameshinda. Kwa maana kuzaliwa
hakungalitufaa kitu, tusingalikombolewa.
Lo, jinsi gani huruma yako kwetu ni ya ajabu! Lo, wema usiopimika wa upendo! Ulimtoa Mwanao upate
kumkomboa mtumwa! Lo, kwa kweli ilihitajika dhambi ya Adamu, iliyofutwa kwa kifo cha Kristo! Lo,
kosa lenye heri, lililostahili kumpata Mkombozi mkuu kama huyo!
Lo, usiku uliobarikiwa kweli, peke yake umestahili kujua majira na saa ya kufufuka kwake Kristo
kutoka kuzimu!
Huu ndio usiku, ulioandikiwa: Usiku utang'aa kama mchana: na usiku waniangaza kati ya furaha
zangu.
Kwa hiyo utakatifu wa usiku huu wafukuza dhambi, wafuta makosa: huwarudishia usafi
walioanguka, na furaha wenye huzuni.
Wafukuza chuki, waleta umoja wa mioyo na kuzinyenyekesha dola.
Basi, ee Baba mwema, kwa ajili ya neema ya usiku huu, upokee sadaka hii ya jioni ya kukusifu.
Ni sadaka linayokutolea Kanisa takatifu kwa mikono ya watumishi wake katika ibada kuu ya huo
mshumaa wa nta iliyotengenezwa kwa kazi ya nyuki.
Na sasa tunafahamu sifa za nguzo hii iliyowashwa kwa heshima ya Mungu kwa moto huu uwakao.
Ingawa moto huo umegawanyika, haukupunguka kwa kuwasha mioto mingine. Kwa maana walishwa kwa
nta inayoyeyuka, iliyotengenezwa na mama nyuki, ikapata kuwa taa hii iliyo bora.
Lo, usiku uliobarikiwa kweli, yalipounganishwa ya mbingu na ya nchi, ya Mungu na ya wanadamu.
Basi, ee Bwana, tunakusihi, mshumaa huu uliobarikiwa kwa heshima ya jina lako uangamize giza
la usiku huu, na uendelee kuwaka.
Tena uupokee kama harufu nzuri, uchanganyike na nuru za mbinguni.
Nyota ya asubuhi iukute unawaka: yaani nyota ile isiyotua kamwe: ndiye Kristo Mwanao, aliyetoka
kuzimu, akawaangaza wanadamu kwa nuru yake angavu, naye anaishi na kutawala milele na milele.
W. Amina.
Mbiu fupi ya Pasaka
Sasa jeshi la Malaika wa mbinguni na wafurahi: wafurahi watumishi wa kimungu: na panda ya
wokovu ipigwe kutangaza ushindi wa Mfalme mkuu. Nayo nchi iliyoangazwa na nuru kubwa sana
ifurahi: na kwa kuwa imemulikwa na mwangaza wa Mfalme wa milele, itambue ya kuwa imeondokewa
na giza la ulimwengu.
Naye mama Kanisa aliyepambwa vizuri kwa taa nyingi zenye kuwaka, afurahi:
na sauti za watu zivume katika ukumbi huu.
(M/. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.)
M/. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
M/. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki tuziimbe sifa za Mungu, Baba mwenyezi asiyeonekana, na za Mwanawe pekee,
Bwana wetu Yesu Kristo, kwa mapendo yote ya moyo na akili na kwa huduma ya sauti.
Yeye alitulipia deni la Adamu kwa Baba wa milele, na kwa damu yake takatifu akafuta hati ya mashtaka
ya ile dhambi ya kale.
Hakika hii ndiyo sikukuu ya Pasaka, anapochinjwa yule Mwanakondoo halisi, ambaye kwa damu yake
milango ya waamini inawekwa wakfu.
Huu ndio usiku, ulipowatoa Misri mara ya kwanza baba zetu, wana wa Israeli, ukawavusha pakavu
katika Bahari ya Shamu.
Huu basi ndio usiku, ulioondoa giza la dhambi kwa nuru ya ile nguzo ya moto.
Huu ndio usiku, ambapo leo popote duniani wenye kumwamini Kristo wanatengwa na maovu ya dunia
na giza la dhambi, wanarudishiwa naye neema na kushirikishwa utakatifu.
Huu ndio usiku, ambapo Kristo alikata minyororo ya mauti, akatoka kuzimu ameshinda.
Kwa maana kuzaliwa hakungalitufaa kitu, tusingalikombolewa.
Lo, jinsi gani huruma yako kwetu ni ya ajabu! Lo, wema usiopimika wa upendo! Ulimtoa Mwanao
upate kumkomboa mtumwa!
Lo, kwa kweli ilihitajika dhambi ya Adamu, iliyofutwa kwa kifo cha Kristo! Lo, kosa lenye
heri, lililostahili kumpata Mkombozi mkuu kama huyo! Lo, usiku uliobarikiwa kweli, peke yake
umestahili kujua majira na saa ya kufufuka kwake Kristo kutoka kuzimu!
Kwa hiyo utakatifu wa usiku huu wafukuza dhambi, wafuta makosa: huwarudishia usafi walioanguka,
na furaha wenye huzuni. Wafukuza chuki, waleta umoja wa mioyo na kuzinyenyekesha dola.
Basi, ee Baba mwema, kwa ajili ya neema ya usiku huu, upokee sadaka hii ya jioni ya kukusifu.
Ni sadaka linayokutolea Kanisa takatifu kwa mikono ya watumishi wake katika ibada kuu ya huo
mshumaa wa nta iliyotengenezwa kwa kazi ya nyuki.
Lo, usiku uliobarikiwa kweli, yalipounganishwa ya mbingu na ya nchi, ya Mungu na ya wanadamu.
Basi, ee Bwana, tunakusihi, mshumaa huu uliobarikiwa kwa heshima ya jina lako uangamize giza la
usiku huu, na uendelee kuwaka.
Tena uupokee kama harufu nzuri, uchanganyike na nuru za mbinguni.
Nyota ya asubuhi iukute unawaka: yaani nyota ile isiyotua kamwe: ndiye Kristo Mwanao, aliyetoka
kuzimu, akawaangaza wanadamu kwa nuru yake angavu, naye anaishi na kutawala milele na milele.
W. Amina.
LITURUJIA YA NENO
Kabla ya kuanza masomo, kuhani anawaelezea watu kwa maneno kama haya:
Ndugu wapendwa sana, tumeingia kwa shangwe katika kesha, sasa tusikilize neno la Mungu kwa
moyo mtulivu. Tutafakari jinsi Mungu alivyoliokoa taifa lake wakati ulipowadia, na mwishowe
akamtuma kwetu Mwanawe awe Mkombozi. Tumwombe Mungu wetu aitimilize kazi hii ya Pasaka yenye
kuleta wokovu, ili tupate ukombozi kamili.
SOMO 1:
Somo refu Mwa.1:1-2:2
Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu,
na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.
Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru
na giza, Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi,
siku moja.
Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. Mungu akalifanya anga,
akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo. Mungu
akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili.
Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane;
ikawa hivyo. Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona
ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao
matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. Nchi ikatoa
majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake,
kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu.
Mungu akasema, na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo
dalili na majira na siku na miaka; tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya
nchi; ikawa hivyo. Mungu akafanya mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo
utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi
na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni
ikawa asubuhi, siku ya nne.
Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi
katika anga la mbingu. Mungu akaumba nyangumi wakubwa; na kila kiumbe chenye uhai kiendacho,
ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu
akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya
baharini, ndege na wazidi katika nchi. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano.
Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na
wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo. Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na
mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu
akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu; kwa sura yetu; wakatawale
samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa
kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanaume
na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi,
na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai
kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso
wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu;
na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho
juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona
kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.
Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake
yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya.
Somo fupi Mwa.1:1,26-31
Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu,
Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu; kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini,
na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya
nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanaume na mwanamke
aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha;
mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu
ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia,
na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila
mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye
uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu
alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita. Basi mbingu
na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote
aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya.
WIMBO WA KATIKATI: Zab33:4-7,12-13(K)5
1. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana.
(K) Nchi imejaa fadhili za Bwana.
2. Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika,
Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.
Hukusanya maji ya bahari chungu chungu,
Huviweka vilindi katika ghala. (K)
3. Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
Toka mbinguni Bwana huchungulia,
Huwatazama wanadamu wote pia. (K)
Baada ya somo refu (Kuumbwa kwa ulimwengu):
SALA
Tuombe. Ee Mungu mwenyezi wa milele, umepanga kazi zako zote kwa namna ya ajabu. Tunakuomba ili,
waliokombolewa nawe wafahamu kwamba hapo mwanzo uumbaji wa ulimwengu ulikuwa mwema, lakini bora
zaidi ni Kristo Pasaka wetu kutolewa sadaka mwisho wa nyakati. Anayeishi na kutawala milele na
milele.
W. Amina.
Au, baada ya somo fupi (Kuhusu uumbaji wa mtu):
Tuombe. Ee Mungu ulimwumba mtu kwa namna ya ajabu, ukamkomboa kwa namna ya ajabu zaidi.
Tunakuomba uimarishe akili zetu tuzidi kupinga anasa za dhambi, tupate kuzifikia furaha za
milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
SOMO 2:
Somo refu Mwa.22:1-18
Wakati ule, Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema,
Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe
sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Ibrahimu akaondoka alfajiri,
akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa
ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. Siku ya
tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali. Ibrahimu akawaambia vijana wake,
kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena.
Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi
mwake, wakaenda wote wawili pamoja. Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babaangu! Naye
akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama, moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi
mwanakondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwanakondoo kwa hiyo
sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja.
Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu. Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari
kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Ibrahimu
akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka
mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono
wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia
mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko
nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo,
akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.
Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa Bwana
itapatikana.
Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni, akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu
asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika
kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na
kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa
yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.
Somo fupi Mwa.22:1-2,9-13,15-18
Wakati ule, Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema,
Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe
sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Ibrahimu akaondoka alfajiri,
akatandika punda wake, Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu. Ibrahimu akajenga madhabahu
huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya
zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa
Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema,
Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu,
iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama,
kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa
huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.
Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni, akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu
asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika
kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na
kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako
mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.16:5,8-11(K)1
1. Bwana ndiye fungu la posho langu,
Na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
(K) Mungu, unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
2. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu,
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu (K)
3. Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume
Mna mema ya milele. (K)
SALA
Tuombe. Ee Mungu, Baba wa waamini uliye mbinguni, kwa kueneza neema ya kufanywa wana unaongeza
popote duniani idadi ya watoto wa ahadi; na kwa fumbo la Pasaka, wamfanya Ibrahimu mtumishi
wako awe baba wa mataifa yote, kama ulivyoahidi kwa kiapo. Uwajalie watu wako wapokee vema
neema ya wito wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Somo lifuatalo ni lazima lisomwe.
SOMO 3: Kut.14:15-15:1
Bwana alimwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele.
Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli
watapita kati ya bahari katika nchi kavu. Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu,
nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa
magari yake na kwa wapanda farasi wake. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana,
nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi zake. Kisha malaika wa
Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya
wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao; ikafika kati ya jeshi la Misri na jeshi
la Israeli; napo palikuwa na lile wingu na lile giza, lakini lilitoa nuru wakati wa usiku; na
hawa hawakuwakaribia hawa usiku kucha.
Musa akanyosha mkono wake juu ya bahari; Bwana akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu
utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika. Wana wa
Israeli wakaenda ndani kati ya bahari katika nchi kavu; nayo maji yalikuwa ukuta kwao mkono
wa kuume, na mkono wa kushoto. Na wale Wamisri wakawafuatia, wakaingia ndani kati ya bahari,
farasi zote za Farao, na magari yake, na wapanda farasi wake. Ikawa katika zamu ya alfajiri,
Bwana akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha
jeshi la Wamisri. Akayaondoa magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri
wakasema, Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa kuwa Bwana anawapigania, kinyume cha Wamisri.
Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri,
juu ya magari yao, na juu ya farasi zao. Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na
kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na Bwana
akawakukutia mbali hao Wamisri kati ya bahari. Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na
wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata
mtu mmoja. Lakini wana wa Israeli wakaenda katika nchi kavu katikati ya bahari; na hayo maji
yalikuwa ni makuta upande wao wa kuume, na upande wao wa kushoto. Ndivyo Bwana alivyowaokoa
Israeli siku ile mikononi mwa Wamisri; Waisraeli wakawaona Wamisri ufuoni kwa bahari, wamekufa.
Israeli akaiona ile kazi kubwa aliyoifanya Bwana juu ya Wamisri, ndipo hao watu wakamcha Bwana,
wakamwamini Bwana, na Musa mtumishi wake. Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo
huu wakanena, na kusema,
WIMBO WA KATIKATI: Kut 15:1-6,17-18(K)1
1. Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana:
Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.
Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu;
Naye amekuwa wokovu wangu.
Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu;
Ni Mungu wa Baba yangu, nami nitamtukuza.
(K) Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana.
2. Bwana ni mtu wa vita,
Bwana ndilo jina lake.
Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini.
Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu.
Vilindi vimewafunikiza,
Walizama vilindini kama jiwe. (K)
3. Bwana, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo,
Bwana, mkono wako wa kuume wawasetaseta adui.
Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha chini
wanaokuondokea. (K)
4. Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako,
Mahali pale ulipojifanyia, ee Bwana ili upakae,
Pale patakatifu ulipopaweka imara, Bwana,
kwa mikono yako.
Bwana atatawala milele na milele. (K)
SALA
Tuombe. Ee Mungu, twaiona miujiza yako ya kale iking'aa hata siku hizi zetu. Kwa maana jambo
ulilolitendea taifa moja kwa nguvu ya mkono wako wa kuume, ulipoliopoa katika dhuluma ya Farao,
ndilo unalolitenda kwa ajili ya wokovu wa mataifa yote kwa maji ya kuzaliwa upya. Uwajalie watu
wote wa dunia wahesabiwe miongoni mwa wana wa Ibrahimu na kushiriki utukufu wa taifa la Israeli.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Au:
Ee Mungu umefumbua kwa nuru ya agano jipya ile miujiza iliyotendeka zamani za kale. Hivyo,
bahari ya Shamu ndio mfano wa kisima cha Ubatizo; nao watu walioopolewa utumwani wanaashiria
fumbo la taifa la Wakristo. Uyajalie mataifa yote yapate kushiriki uteuzi wa Israeli kwa
njia ya imani, na kuzaliwa upya kwa kushirikishwa Roho wako Mtakatifu. Tunaomba hayo kwa
njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
SOMO 4: Isa.54:5-14
Kwa sababu Muumba wako ni mume wako, Bwana wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli
ndiye Mkombozi wako, yeye ataitwa Mungu wa dunia yote. Maana Bwana amekuita kama mke aliyeachwa
na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako. Kwa kitambo kidogo
nimekuacha, lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya. Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu
dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema Bwana, Mkombozi wako. Kwa maana
jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu; maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu
hayatapita juu ya dunia tena, kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea.
Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa, bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano
langu la amani halitaondolewa; asema Bwana akurehemuye. Ewe uliyeteswa, uliyerushwa na tufani,
usiyetulizwa, tazama, nitaweka mawe yako kwa rangi nzuri, nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi.
Nami nitaifanya minara yako ya akiki nyekundu, na malango yako ya almasi, na mipaka yako yote ya
mawe yapendezayo. Na watoto wako wote watafundishwa na Bwana, na amani ya watoto wako itakuwa
nyingi. Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa, na mbali na hofu,
kwa maana haitakukaribia.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.30:1.3,4.5.10-11.12(K)1
1. Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
Umeniinua nafsi yangu,
Ee Bwana, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa
Miongoni mwao washukao shimoni.
(K) Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua.
2. Mwimbieni Bwana zaburi,
Enyi watauwa wake,
Na kufanya shukrani,
Kwa kumbukumbu la utakatifu wake. (K)
3. Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
Katika radhi yake mna uhai.
Huenda kilio huja kukaa usiku,
Lakini asubuhi huwa furaha. (K)
4. Ee Bwana, usikie, unirehemu,
Bwana, uwe msaidizi wangu.
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo,
Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
Ee Bwana, Mungu wangu,
Nitakushukuru milele. (K)
SALA
Tuombe. Ee Mungu mwenyezi wa milele, uzidishe kwa heshima ya jina lako yale uliyowaahidia mababu
wa imani. Uongeze idadi ya watoto wa ahadi kwa neema ya kufanywa wana; ili, hayo ambayo watakatifu
wa kale waliamini bila kusita kwamba yatatokea, sasa Kanisa lione yametimia kwa sehemu kubwa.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
SOMO 5: ISa.S:1-11
Bwana asema hivi: Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, naye asiye na fedha, njoni, nunueni mle;
naam, njoni, nunueni divai na maziwa, bila fedha na bila thamani. Kwani kutoa fedha kwa ajili ya
kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, mle
kilicho chema, na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono. Tegeni masikio yenu, na kunijia, sikieni,
na nafsi zenu zitaishi! Nami nitafanya nanyi agano la milele, naam, rehema za Daudi zilizo imara.
Angalieni, nimemweka kuwa shahidi kwa kabila za watu, kuwa kiongozi na jemadari kwa kabila za
watu. Tazama, utaita taifa usilolijua, na taifa lisilokujua wewe litakukimbilia, kwa sababu ya
Bwana, Mungu wako, na kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli, maana amekutukuza. Mtafuteni Bwana,
maadamu anapatikana, mwiteni, maadamu yu karibu. Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki
aache mawazo yake; na amrudie Bwana, naye atamrehemu; na arejee kwa Mungu wetu, naye atamsamehe
kabisa. Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu, asema Bwana, Kwa maana
kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu,
na mawazo yangu kuliko mawazo yenu. Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni,
wala hairudi huko, bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu,
na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu:
halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale
niliyolituma.
WIMBO WAKATIKATI: Isa.12:2-6(K)3
1. Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana Mungu ni nguvu zangu na wimbo wangu,
Naye amekuwa wokovu wangu.
(K) Kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu.
2. Na katika siku hiyo mtasema,
"Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)
3. Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako." (K)
SALA
Tuombe. Ee Mungu mwenyezi wa milele, ndiwe peke yako tumaini la ulimwengu. Ulitangaza kama mbiu
ya manabii wako mafumbo ya nyakati hizi. Upokee kwa wema maombi ya watu wako na kuyatimiza; kwa
maana hakuna maendeleo ya waamini katika fadhila isipokuwa kutokana na uvuvio wako. Tunaomba
hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
SOMO 6: Bar.3:9-15,32-4:4
Sikia, ee Israeli, amri za uzima, tega sikio lako kujua hekima. Imekuwaje, ee Israeli, uko
katika nchi ya adui zako, ukizeeka katika nchi ya kigeni? Umetiwa najisi na wafu, umehesabiwa
nao washukao shimoni? Umeiacha chemchemi ya uzima! Maana kama ungaliifuata njia ya Mungu
ungalikaa kwa amani siku zote. Itafute hekima ilipo, na nguvu, na maarifa, ili ujue ulipo wingi
wa siku, na uzima, ilipo nuru ya macho na amani. Ni nani aliyeona mahali pake? Na kuingia katika
ghala zake? Lakini Yeye ajuaye yote anaijua, aliitambua kwa ufahamu wake. Yeye aliyeweka dunia
milele na kuijaza wanyama wenye miguu minne; Yeye aitumaye nuru ikaenda, akaiita ikamtii kwa
kicho. Nyota zikang'aa katika majira yake zikafurahi; alipoziita zilisema, "Tupo hapa!” na kwa
furaha zikamng'aria Muumba wao. Huyu ndiye Mungu wetu, wala hakuna afananaye naye; ameivumbua
njia yote ya hekima akampa Yakobo mtumishi wake, na Israeli mpendwa wake. Baadaye hekima
ikaonekana duniani ikakaa na watu. Hiki ni kitabu cha amri za Mungu na sheria idumuyo milele.
Wote waishikao wataona uzima, lakini waiachao watakufa. Rudi, ee Yakobo, uishike, uiendee nuru
yake katika mwangaza wake. Usimpe mwingine utukufu wako, wala mataifa ya kigeni mafaa yako. Ee
Israeli, tu heri sisi, maana mambo yampendezayo Mungu yamejulishwa kwetu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.19:7-10(K) Yn.6:69
1. Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima.
(K) Wewe unayo maneno ya uzima wa milele,
ee Bwana.
2. Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufrahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru. (K)
3. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa. (K)
4. Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
Kuliko sega la asali. (K)
SALA
Tuombe. Ee Mungu, unalikuza daima Kanisa lako kwa kuwaita mataifa. Uwajalie hao, unaowatakasa
kwa maji ya Ubatizo, watunzwe siku zote kwa ulinzi wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana
wetu.
W. Amina.
SOMO 7: Eze.36:16-28
Neno la Bwana likanijia, kusema, "Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokaa katika nchi yao
wenyewe, waliitia uchafu kwa njia yao na kwa matendo yao. Njia yao mbele zangu ilikuwa kama
uchafu wa mwanamke wakati wa kutengwa kwake. Kwa hiyo nalimwaga hasira yangu juu yao, kwa
ajili ya damu waliyoimwaga juu ya nchi, na kwa sababu wameitia uchafu kwa vinyago vyao.
Nikawatawanya katika mataifa, wakatapanyika katika nchi nyingi; kwa kadiri ya njia yao, na
kwa kadiri ya matendo yao, naliwahukumu. Nao walipoyafikilia mataifa yale waliyoyaendea,
walilitia unajisi jina langu takatifu, kwa kuwa watu waliwanena, wakisema, 'Watu hawa ni watu
wa Bwana, nao wametoka katika nchi yake.' Lakini naliwahurumia kwa ajili ya jina langu takatifu,
ambalo nyumba ya Israeli walikuwa wamelitia unajisi katika mataifa waliyoyaendea. Kwa hiyo
waambieni nyumba ya Israeli, Bwana Mungu asema hivi, Sitendi hili kwa ajili yenu, ee nyumba ya
Israeli, bali kwa ajili ya jina langu takatifu, mlilolitia katika mataifa mliyoyaendea. Nami
unajisi nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati
yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, asema Bwana Mungu, nitakapotakaswa kati yenu
mbele ya macho yao. Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi
zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi;
nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami
nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami
nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu,
nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu,
nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.42:2,4;43:3-4(K)42:1
1. Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?
(K) Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji,
vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku,
ee Mungu.
2. Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu,
Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano,
Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu,
Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu. (K)
3. Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,
Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu
Na hata maskani yako. (K)
4. Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu,
Kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu;
Nitakusifu kwa kinubi,
Ee Mungu, Mungu wangu. (K)
SALA
Tuombe. Ee Mungu, uliye nguvu isiyotetereka na mwanga wa milele, uwe radhi kuliangalia fumbo
la ajabu la Kanisa zima. Na kwa kutimiza mpango wako wa milele, utende kazi ya wokovu wa
wanadamu katika amani, ili ulimwengu wote utambue na kuona kwamba kile kilichobomolewa kimejengwa
tena, kilichochakaa kimefanywa upya, na vitu vyote vimepata tena uzima wake kwa njia ya Kristo
mwenyewe, aliye asili ya vitu vyote. Anayeishi na kutawala milele na milele.
W. Amina.
Au:
Tuombe. Ee Mungu, kwa maandiko ya Agano la Kale na Agano Jipya unatufundisha tuadhimishe fumbo
la Pasaka. Utujalie tufahamu huruma yako, ili, kwa kupokea zawadi za sasa, tuimarishwe katika
kuzitarajia zile zijazo. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
- mishumaa ya altareni inawashwa, na
- kuhani anaanza kuimba Utukufu kwa Mungu juu na wote wanaendelea kuuimba.
- Hapo kengele zinapigwa, kama ilivyo desturi ya mahali hapo.
- Baada ya wimbo, kuhani anasema kolekta kama kawaida.
KOLEKTA
Tuombe. Ee Mungu, umeuangaza usiku huu mtakatifu sana kwa utukufu wa kufufuka kwake Bwana wetu.
Uamshe katika Kanisa lako roho ya kufanywa wana, ili, tukiisha kufanywa upya mwilini na rohoni,
tukutukuze kwa utumishi safi. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi
na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
W. Amina.
Kisha msomaji anasoma somo la waraka.
SOMO LA WARAKA: Rum.6:3-11
Ndugu zangu, hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti
yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya Ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo
alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika
upya wa uzima. Kwa maana kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika
tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; tukijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale
ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena; kwa kuwa
yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi. Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo,
twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye; tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu
hafi tena, wala mauti haimtawali tena. Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja
tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa
wafu kwa dhambi, na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.
- Baada ya somo la Waraka, wote wanasimama, na kuhani anaanza kuimba
Aleluya mara tatu kwa shangwe, akiinua sauti yake kila mara kidogo zaidi, na wote wanarudia
kuimba.
- Ikiwa ni lazima, mwimba zaburi ndiye anayeanzisha kuimba Aleluya! Halafu mwimba zaburi au
mwimbaji anaimba zaburi 118, wakati watu huitikia Aleluya!
WIMBO WA KATIKATI: Zab.118:1-2,16-17,22-23
1. Aleluya!
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
(K) Aleluya, Aleluya, Aleluya!
2. Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi,
Nami nitayasimulia matendo ya Bwana. (K)
3. Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu. (K)
INJILI
MWAKA A
INJILI: Mt.28:1-10
Hata sabato ilipokwisha, ikapambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu
yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi;
kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia.
Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi
wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa
maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema.
Njoni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka
katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia.
Wakaondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi
wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia
wakamshika miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie
ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.
Mwaka B
INJILI: Mk.16:1-8
Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua
manukato wapate kwenda kumpaka. Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini,
jua lilipoanza kuchomoza. Wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe
mlangoni pa kaburi? Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa;
nalo lilikuwa kubwa mno. Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa
vazi jeupe; wakastaajabu. Naye akawaambia Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa;
amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi
wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; nuko mtamwona, kama alivyowaambia.
Wakatoka nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingiwa tetemeko
na ushangao; wala hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa.
Mwaka C
INJILI: Lk.24:1-12
Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato
waliyoweka tayari. Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi, wakaingia, wasiuone
mwili wa Bwana Yesu. Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili
walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumetameta; nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi
hata nchi, hao waliwaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu? Hayupo hapa, amefufuka.
Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya, akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kutiwa
mikononi mwa wenye dhambi, na kusulibiwa, na kufufuka siku ya tatu. Wakayakumbuka maneno yake.
Wakaondoka kaburini, wakarudi; wakawaarifu wale kumi na mmoja na wengine wote habari za mambo
hayo yote. Nao ni Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine
waliokuwa pamoja nao: hao waliwaambia mitume habari ya mambo hayo. Maneno yao yakaonekana kuwa
kama upuzi kwao, wala hawakuwasadiki. Lakini Petro aliondoka akaenda mbio hata kaburini, akainama
akachungulia ndani; akaviona vile vitambaa vya sanda tu; akaenda zake akiyastaajabia
yaliyotukia.
LITURUJIA YA UBATIZO
Litania yanaweza kuongezwa majina fulani ya Watakatifu, hasa ya Msimamizi wa kanisa au
msimamizi wa mahali pale na wa wale watakaobatizwa.
Litania
Bwana, utuhurumie. = Bwana, ut.
Kristo, utuhurumie. = Kristo, ut.
Bwana, utuhurumie. = Bwana, ut.
Maria mtakatifu, Mama wa Mungu, = utuombee.
Mtakatifu Mikaeli, = ut.
Watakatifu Malaika wa Mungu, = mt.
Mtakatifu Yohane Mbatizaji, = ut.
Mtakatifu Yosefu, = ut.
Watakatifu Petro na Paulo, = mt.
Mtakatifu Andrea, = ut.
Mtakatifu Yohane, = ut.
Mtakatifu Maria Magdalena, = ut.
Mtakatifu Stefano, = ut.
Mtakatifu Ignasi wa Antiokia, = ut.
Mtakatifu Laurenti, = ut.
Watakatifu Perpetua na Felisita, = mt.
Mtakatifu Agnesi, = ut.
Mtakatifu Gregori, = ut.
Mtakatifu Augustino, = ut.
Mtakatifu Atanasi, = ut.
Mtakatifu Basili, = ut.
Mtakatifu Martino, = ut.
Mtakatifu Benedikto, = ut.
Watakatifu Fransisko na Dominiko, = mt.
Mtakatifu Fransisko (Ksaveri), = ut.
Mtakatifu Yohane Maria (Vianei), = ut.
Mtakatifu Katarina wa Siena, = ut.
Mtakatifu Teresa wa Yesu, = ut.
Mtakatifu Yohane XXIII, = ut.
Mtakatifu Paulo VI, = ut.
Mtakatifu Yohane Paulo II, = ut.
Watakatifu wote wa Mungu, = mt.
Uturehemie, = utuokoe, Bwana.
Katika uovu wowote, = utuo.
Katika dhambi yoyote, = utuo.
Katika mauti ya milele, = utuo.
Kwa kujifanya mwanadamu, = utuo.
Kwa kufa na kufufuka kwako, = utuo.
Kwa kumpeleka Roho Mtakatifu, = utuo.
Sisi wakosefu, = twakuomba, utusikie.
Wakiwapo wa kubatizwa
Upende kuwajalia wateule hawa uzima mpya kwa
neema ya Ubatizo, = twakuomba, utusikie.
Wasipokuwapo wa kubatizwa
Upende kutakatifuza kwa neema yako kisima hiki
cha Ubatizo, ambamo kwako watazaliwa wana, = twakuomba, utusike.
Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, = twakuomba, utusike.
Kristo, utusikie. = Kristo, utusikie.
Kristo, utusikilize. = Kristo, utusikilize.
Iwapo kuna wateule wa kubatizwa, kuhani, hali amefumbua mikono, anasema
sala hii:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, uoneshe uwepo wako katika maadhimisho ya sakramenti za rehema yako
kuu. Utume roho ya kufanywa wana, ili kuwapa uhai watu wapya ambao kisima cha ubatizo kinakuzalia.
Hivyo, yale yatakayotendwa kwa njia ya huduma yetu nyenyekevu, yatimizwe kwa njia ya nguvu zako.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
BARAKA YA MAJI YA UBATIZO
Kisha kuhani anabariki maji ya Ubatizo, akisema sala ifuatayo, hali amefumbua mikono:
Ee Mungu, unatenda kwa nguvu isiyoonekana mambo ya ajabu kwa njia ya sakramenti. Umeyafanya maji
kwa namna mbalimbali yawe ishara ya neema ya Ubatizo. Ee Mungu, Roho wako alitua juu ya maji hapo
mwanzo wa dunia, ili toka hapo maji yapate nguvu ya kuwatakasa watu. Ee Mungu, uliweka ishara ya
kuzaliwa upya katika tufani kuu ili katika fumbo la gharika hiyo, iwe ndio mwisho wa maovu na
mwanzo wa fadhila. Ee Mungu, ulipowavusha pakavu wana wa Ibrahimu katika Bahari ya Shamu, ulitaka
hilo taifa, lililokombolewa katika utumwa wa Farao, liwe mfano wa taifa la wale waliobatizwa.
Ee Mungu, Mwanao aliyebatizwa na Yohane katika maji ya Yordani alipakwa Roho Mtakatifu. Naye
alipokuwa ametundikwa msalabani, alitaka maji pamoja na damu yatoke ubavuni mwake. Na baada ya
kufufuka kwake, aliwaamuru wanafunzi wake: "Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,
mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu". Ulitazame Kanisa lako, upende
kulifungulia kisima cha Ubatizo. Maji haya na yatwae neema ya Mwanao pekee kwa Roho Mtakatifu,
ili mwanadamu aliyeumbwa kwa mfano wako, atakaswe unajisi wote wa zamani kwa sakramenti ya
Ubatizo, astahili kufufuliwa katika hali ya mtoto mpya kwa maji na Roho Mtakatifu.
Kisha, kadiri inavyofaa, anautia mshumaa katika maji mara moja au
tatu, akiendelea kusema:
Ee Bwana, tunaomba nguvu ya Roho Mtakatifu ishuke ndani ya maji yote ya kisima hiki kwa njia
ya Mwanao,
na akishika mshumaa katika maji, anaendelea kusema:
kusudi wote waliozikwa katika mauti pamoja na Kristo kwa Ubatizo, wafufuke pamoja naye katika
uzima. Anayeishi na kutawala nawe, katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
W. Amina.
Kisha anautoa mshumaa katika maji, watu wakishangilia:
Chemchemi, mhimidini Bwana, msifuni na kumwadhimisha milele.
BARAKA YA MAJI
Kama hakuna yeyote wa kubatizwa, wala kisima cha Ubaizo hakikubarikiwa, kuhani anawaalika
waamini kwenye baraka ya maji, akisema:
Ndugu zangu, tumsihi Bwana Mungu wetu, apende kuyabariki maji haya, tutakayonyunyiziwa kutukumbusha Ubatizo wetu. Yeye mwenyewe apende kututengeneza upya, tupate kudumu amini kwa Roho
Mtakatifu tuliyempokea.
Na baada ya muda mfupi wa ukimya, anasema sala hii, hali amefumbua
mikono:
Ee Bwana Mungu wetu, tunaomba uwe pamoja na sisi watu wako tunaokesha usiku huu mtakatifu sana.
Upende kuyabariki maji haya kwa ajili yetu sisi tunaokumbuka kazi ya ajabu ya kuumbwa kwetu na
kazi iliyo bora zaidi ya kukombolewa kwetu. Ndiwe uliyeyaumba maji haya yapate kustawisha
mashamba yetu, kuburudisha miili yetu na kuitakasa. Isitoshe, umeyaumba maji yawe kitu cha
kutuletea huruma yako. Maana kwa maji ulilikomboa taifa lako utumwani, ukatuliza kiu yao
jangwani; kwa maji manabii waitangaza agano jipya ambalo baadaye ulilifanya na watu. Hatimaye
kwa maji yaliyowekwa wakfu na Kristo mle Yordani, ulitengeneza upya katika kisima cha Ubatizo
ubinadamu wetu ulioharibika. Basi maji haya yawe ukumbusho kwetu sisi tuliokwisha kubatizwa.
Utujalie tufurahi pamoja na ndugu zetu waliobatizwa Pasaka hii. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo
Bwana wetu.
W. Amina.
KUWEKA TENA AHADI ZA UBATIZO
- wanasimama wameshika mikononi mishumaa inayowaka na kurudia ahadi za Ubatizo wao.
- Kuhani anawaambia waamini maneno kama haya:
Ndugu zangu, katika Ubatizo sisi tumezikwa pamoja na Kristo kwa fumbo la Pasaka, tupate
kutembea pamoja naye katika uzima mpya. Kwa hiyo, baada ya mfungo wa Kwaresima, tuweke tena
ahadi zetu za Ubatizo tulizofanya zamani tulipomkataa shetani na mambo yake, tukaahidi kumtumikia
Mungu katika Kanisa takatifu Katoliki.
Basi:
Kuhani: Mwamkataa shetani?
Wote: Ninamkataa.
Kuhani: Na matendo yake yote?
Wote: Ninayakataa.
Kuhani: Na fahari zake zote?
Wote: Ninazikataa.
Au:
Kuhani: Mwaikataa dhambi, mpate kuishi katika uhuru wa wana wa Mungu?
Wote: Ninaikataa.
Kuhani: Mwavikataa vishawishi vya uovu, msipate kutawaliwa na dhambi?
Wote: Ninavikataa.
Kuhani: Mwamkataa shetani aliye asili na mkuu wa dhambi?
Wote: Ninamkataa.
-------
Kuhani: Mwasadiki kwa Mungu Baba mwenyezi, mwumba mbingu na dunia?
Wote: Ninasadiki.
Kuhani: Mwasadiki kwa Yesu Kristo, Mwanawe pekee, Bwana wetu, aliyezaliwa
na Bikira Maria, akateswa akafa na kuzikwa, akafufuka katika wafu, ameketi kuume kwa Baba?
Wote: Ninasadiki.
Kuhani: Mwasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu katoliki, ushirika
wa watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili na uzima wa milele?
Wote: Ninasadiki.
Kuhani: Naye Mungu Mwenyezi, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, alitupatia
uzima mpya kwa maji na Roho Mtakatifu, akatujalia maondoleo ya dhambi. Yeye mwenyewe atulinde kwa
neema yake katika Kristo Yesu Bwana wetu tupate uzima wa milele.
Wote: Amina.
Kuhani anawanyunyizia waamini maji ya baraka, wakati wote wakiimba:
ANTIFONA
Niliona maji yakitoka hekaluni upande wa kuume, aleluya; na wote waliofikiwa na maji hayo waliokoka,
nao watasema: Aleluya, aleluya!
MAOMBI
Ndugu, kwa furaha kubwa usiku huu tunamshangilia Bwana wetu Yesu Kristo aliyeshinda mauti na
kuturudishia uzima wa kimungu tupate kuwa nuru ya ulimwengu. Sasa hivi tumshukuru Mungu na
kumwomba neema zake. Ee Mungu Mwenyezi twakuomba:
1. Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa lako wapate mwamko
mpya wa kumhubiri Kristo Mfufuka katika ulimwengu huu wa sasa.
2. Viongozi wote wa dunia hii wawaongoze raia wao, huku wakijua kuwa wanamwakilisha Kristo Mfufuka
aliyewatokea na kuwapa kazi wafuasi wake.
3. Kwa ufufuko wa Mwanao, uwajaze waamini wote furaha ya kushiriki mateso ya Mwanao kwa matumaini
ya kupata utukufu wa ufufuo usio na mwisho.
4. Utuimarishe sisi sote katika imani ya ufufuko; na Mwanga wako wa Pasaka utusaidie kupambana na
nguvu za giza.
5. Uwajalie wote waliobatizwa Usiku huu wa leo kutembea katika Mwanga wa Pasaka hadi kwenye uzima
wa milele.
6. Kwa huruma yako, marehemu wetu wafufuke leo pamoja na Kristo na kuuona mwanga wako wa milele.
Ee Mungu, kwa ufufuko wa Mwanao umeifurahisha dunia na kututhibitishia matumaini ya ufufuko na
utukufu baada ya maisha ya hapa duniani. Kwako iwe sifa na utukufu, daima na milele. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakuomba uzipokee sala za watu wako, pamoja na dhabihu hizi; ili yale yaliyoanza kwa
mafumbo ya Pasaka, kwa utendaji wako, yawe dawa inayotufaa kwa ajili ya uzima wa milele. Kwa njia
ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
UTANGULIZI wa Pasaka: Fumbo la Pasaka
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, kukutukuza
kila wakati, ee Bwana, lakini hasa usiku huu kutangaza utukufu wako, kwa kuwa Kristo, Pasaka wetu,
ametolewa sadaka.
Yeye ndiye Mwanakondoo wa kweli aliyeondoa dhambi za ulimwengu. Yeye ndiye aliyeangamiza mauti
yetu kwa kufa kwake, na alitengeneza upya uzima kwa kufufuka kwake.
Kwa sababu hiyo, katika upeo wa furaha ya kipasaka, ulimwengu mzima unashangilia. Lakini pia
nguvu za mbinguni na majeshi ya Malaika wanaimba utenzi wa utukufu wako, wakisema bila mwisho:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu...
ANTIFONA YA KOMUNYO: 1Kor.5:7.8
Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani Kristo; basi na tuifanye karamu kwa
yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli, aleluya!
SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Bwana, umimine Roho wa upendo wako ndani yetu, ili sisi uliotushibisha kwa mafumbo ya Pasaka,
utufanye kuwa moyo mmoja kwa huruma yako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
BARAKA KUU
Mungu mwenyezi awabariki, tunapoadhimisha usiku huu sherehe ya Pasaka, na kwa rehema yake awakinge na kila shambulio la dhambi.
W. Amina.
Yeye ambaye, kwa ufufuko wa Mwanae pekee, anawafanya upya kwa ajili ya uzima wa milele, awajalie tuzo za milele.
W. Amina.
Nanyi mnaoadhimisha furaha za Pasaka, baada ya kumaliza siku za mateso ya Bwana, mjaliwe kufikishwa kwa moyo mchangamfu kwenye ile sherehe ya furaha isiyo na mwisho.
W. Amina.
Na baraka yake Mungu mwenyezi, Baba, + na Mwana, na Roho Mtakatifu iwashukie na kukaa nanyi daima.
W. Amina.
kuhani: Nendeni na amani, aleluya, aleluya!
Wote: Tumshukuru Mungu, aleluya, aleluya!