JUMAMOSI BAADA YA KUPAA BWANA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.
Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie -
Ulio mwetu mioyoni -
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.
Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho.
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
Zab.119:81-88 XI Sala wakati wa kudhulumiwa
Niko hoi kwa kukungojea uniokoe;*
naweka tumaini langu katika neno lako.
Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi.*
Nauliza:“Utakuja lini kunifariji?”
Nimekunjamana kama kiriba katika moshi,*
hata hivyo sijasahau amri zako.
Nitasubiri mpaka lini?*
Utawaadhibu lini wenye kunidhulumu?
Wenye kiburi, wasiojali sheria yako,*
wamenichimbia mashimo kunitega.
Amri zako zote ni za kuaminika;/
watu waongo wananidhulumu,*
tafadhali unisaidie!
Karibu wangefaulu kuniangamiza,*
lakini mimi sijavunja amri zako.
Unisalimishe kadiri ya upendo wako mkuu,*
nipate kuzingatia maagizo yako.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.61 Kuomba ulinzi
Sala ya mwadilifu atamaniye mambo ya mbinguni (Mt. Hilari)
Usikie kilio changu, Ee Mungu;*
usikilize sala yangu.
Ninakulilia ugenini humu;*
nikiwa nimevunjika moyo.
Unipeleke kwenye mwamba wa usalama,/
maana wewe ndiwe kimbilio langu,*
kinga yangu imara dhidi ya adui.
Uniruhusu nikae hemani mwako milele*
nipate usalama chini ya mabawa yako.
Ee Mungu, umezipokea nadhiri zangu,*
umenijalia mema uliyowaahidia wakuchao.
Umjalie mfalme maisha marefu,*
miaka yake iwe ya vizazi vingi.
Atawale milele mbele yako, Ee Mungu;*
mapendo na uaminifu wako vimlinde.
Hapo nitakuimbia nyimbo za sifa,*
nikizitekeleza kila siku nadhiri zangu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.64 Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
Zaburi hii hasa yatualika kuyafikiria mateso ya Bwana (Mt. Augustino)
Usikie, Ee Mungu, usikilize lalamiko langu;*
unilinde maisha yangu na vitisho vya adui.
Unikinge na njama za waovu,*
na ghasia za watu wabaya.
Wananoa ndimi zao kama upanga,*
wanafyatua maneno ya ukatili kama mishale.
Toka mafichoni wanamshambulia mtu mnyofu,*
wanamshambulia ghafula bila kuogopa.
Wanashirikiana katika nia yao mbaya;/
wanapatana mahali pa kuficha mitego yao.*
Wakifikiri: “Hakuna atakayeweza kuiona!”
Hufanya njama zao na kusema:/
"Sasa tumekamilisha mpango.*
Nani atagundua hila zetu?”
Mipango ya siri imefichika moyoni mwa mtu!/
Lakini Mungu atawapiga mishale,*
na kuwajeruhi ghafula.
Atawaangamiza kwa sababu ya maneno yao;*
kila atakayewaona atatikisa kichwa.
Hapo watu wote wataogopa;/
watatangaza aliyotenda Mungu,*
na kufikiri juu ya matendo yake.
Waadilifu watafurahia aliyotenda Mungu,/
watakimbilia usalama kwake.*
Watu wote wema wataona fahari.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Rom.5:10-11
Tulipokuwa bado adui zake, Mungu alitupatanisha naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa
tumepatanishwa naye, ni dhahiri zaidi kwamba tutaokolewa kwa uzima wa Kristo. Wala si hayo
tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ametupatanisha
na Mungu.
K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: 1Kor.15:20-22
Ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka wafu, na ni uthibitisho kwamba wale waliolala
katika kifo watafufuliwa. Maana, kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo
hivyo nako kufufuka katika wafu kumesababishwa na mtu mmoja. Kama vile watu wote wanavyokufa
kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo.
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: 2Kor.5:14-15
Mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili
ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake. Alikufa kwa ajili ya watu wote,
ili wanaoishi wasiishi tena kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa
kwa ajili yao.
K. Kaa nasi, Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.
SALA:
Tuombe: Mungu na Baba, Mwanao alipopaa mbinguni, aliwaahidia mitume Roho Mtakatifu. Walipokea
neema nyingi za hekima kutoka mbinguni: tunakuomba utujalie na sisi karama za Roho wako. Tunaomba
hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.