Generic placeholder image

JUMAMOSI BAADA YA KUPAA BWANA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo Bwana ametuahidia Roho Mtakatifu: njooni, tumwabudu, aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.

Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.

Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.

Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.

Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.

Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.

Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.


2 (33) Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.

E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!

Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.

Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.

Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.

Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.

Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.

3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;

Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;

Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.

Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal

4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.

Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.

Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.

Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434

5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.

Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.

Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930

Ant. I: Umenifurahisha, Ee Bwana; kwa kazi ya mikono yako nitashangilia, aleluya.

Zab.92 Wimbo wa kumsifu Mungu
Matendo ya Mwana wa pekee wa Mungu yanasifiwa (Mt. Athanasius)

Ni vema kukushukuru, Ee Mungu,*
kuimba kwa heshima yako, Ee Mungu Mkuu.

Ni vema kutangaza upendo wako mkuu asubuhi,*
na uaminifu wako kila usiku,

kwa muziki wa zeze na kinanda,*
kwa sauti tamu ya kinubi.

Ee Mungu, matendo yako makuu yanifurahisha;*
nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda.

Matendo yako, Ee Mungu, ni makuu mno!*
Mawazo yako ni mazito mno!

Mtu mpumbavu hawezi kufahamu,*
wala mjinga hajui jambo hili:

kwamba waovu waweza kusitawi kama nyasi;*
watenda maovu waweza kupata fanaka,

lakini mwisho wao wote ni kuangamia milele;*
maana wewe, Ee Mungu, ni mkuu milele.

Maana tazama, Ee Mungu,/
adui zako hakika wataangamia;*
Wote watendao maovu, watatawanyika!

Wewe umenipa nguvu kama nyati;*
umenimiminia mafuta ya furaha.

Kwa macho nimeona adui zangu wameshindwa;*
nimesikia kilio chao watendao maovu.

Waadilifu husitawi kama mtende;*
hukua kama mwerezi wa Lebanon!

Kama mti uliopandwa katika nyumba ya Mungu,*
wanasitawi katika nyua za Mungu wetu.

Ingawa wamezeeka, wataendelea kuwa na nguvu;*
wapate kuutangaza uadilifu wa Mungu,

na kwamba hamna uovu wowote,*
kwake yeye aliye ngome yangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Umenifurahisha, Ee Bwana; kwa kazi ya mikono yako nitashangilia, aleluya.

ANT. II: Mimi ndiye nitoaye mauti na uzima; ndimi pia ninayejeruhi na kuponya, aleluya.

WIMBO: Kum.32:1-12 Fadhili alizowatendea Mungu watu wake
Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya kwangu watoto wako, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake (Mt.23:37)

Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitanena;*
Na nchi isikie maneno ya kinywa changu.

Mafundisho yangu yatadondoka kama mvua,*
Maneno yangu yatatonatona kama umande;

Kama manyunyu juu ya majani mabichi;*
Kama matone ya mvua juu ya mimea.

Maana nitalitangaza Jina la BWANA;*
Mpeni ukuu Mungu wetu.

Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu;*
Maana, njia zake zote ni haki.

Mungu wa uaminifu, asiye na uovu,*
Yeye ndiye mwenye haki na adili.

Wametenda mambo ya uharibifu,/
Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao;*
Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka.

Je! mnamlipa BWANA hivi,*
Enyi watu wapumbavu na wajinga?

Je! yeye siye baba yako aliyekununua?*
Amekufanya, na kukuweka imara.

Kumbuka siku za kale,*
Tafakari miaka ya vizazi vingi;

Mwulize baba yako, naye atakuonesha;*
Wazee wako, nao watakuambia.

Yeye Aliye Juu alipowapa mataifa urithi wao,*
Alipowabagua wanadamu,

Aliweka mipaka ya watu*
Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli.

Maana, sehemu ya BWANA ni watu wake,*
Yakobo ni kura ya urithi wake.

Alimkuta katika nchi ya ukame,*
Na katika jangwa tupu litishalo;

Alimzunguka, akamtunza;*
Akamhifadhi kama mboni ya jicho;

Mfano wa tai ataharikishaye kiota chake;*
Na kupapatika juu ya makinda yake,

Alikunjua mbawa zake, akawatwaa,*
Akawachukua juu ya mbawa zake;

BWANA peke yake alimwongoza,*
Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Mimi ndiye nitoaye mauti na uzima; ndimi pia ninayejeruhi na kuponya, aleluya.

ANT. III: Bwana, umemvika taji ya utukufu na heshima Masiha wako, aleluya.

Zab.8 Utukufu wa Mungu na cheo cha binadamu
Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa Kanisa, akiwa ndio mkuu wa vitu vyote (Ef.1:22)

Ee Mwenyezi, Bwana wetu,/
jina lako latukuka kote duniani!*
Utukufu wako wafika hata mbinguni;

wasifika na vinywa vya watoto wadogo na wachanga/
Wewe uko imara mbele ya wapinzani wako;*
wawakomesha maadui na waasi.

Nikiangalia anga,/
kazi ya vidole vyako mwenyewe,*
mwezi na nyota ulivyoviumba:

mtu ni nini, Ee Mungu, hata umfikirie?*
Mwanadamu ni nini hata umjali?

Hata hivyo, ulimfanya mdogo kidogo tu,/
kuliko wewe mwenyewe,*
na umemvika taji ya utukufu na heshima.

Ulimpa mamlaka juu ya kazi zako zote;*
uliviweka viumbe vyote chini ya miguu yake:

kondoo, ng'ombe na wanyama wa porini;*
ndege, samaki na viumbe vyote vya baharini.

Ee Mwenyezi, Bwana wetu:*
Jina lako latukuka duniani kote!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Bwana, umemvika taji ya utukufu na heshima Masiha wako, aleluya.

SOMO: Rom.14:7-9
Hakuna mtu ye yote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe; maana tukiishi, twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana. Maana Kristo alikufa, akafufuka ili apate kuwa Bwana wa wazima na wafu.

KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Kweli, nawaambieni, cho chote muombacho kwa Baba kwa jina langu, atawapeni, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Kweli, nawaambieni, cho chote muombacho kwa Baba kwa jina langu, atawapeni, aleluya.

MAOMBI
Sifa na utukufu kwa Kristo! Aliwaahidi mitume kwamba nguvu ya Roho Mtakatifu ingewashukia.
W. Utuletee mwanga wa ukweli wako.

Wewe ni Neno wa ukweli, hekima na utukufu wa Baba;
- utuwezeshe kukushuhudia leo, kwa maneno na matendo yetu. (W.)

Utuwezeshe kutambua na kuyachuchumia mambo ya Roho;
- pale ilipo mioyo yetu, ndipo pia itakapokuwa hazina yetu. (W.)

Umtume Roho Mtakatifu, aje kutusaidia katika udhaifu wetu,
- na kutufundisha jinsi itupasavyo kusali. (W.)

Tunaomba tujazwe elimu na mapendo;
- utuwezeshe kushauriana, tukizingatia ukweli na mapendo. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Kwa mara nyingine tena, tumtukuze na kumwomba Baba kwa maneno ya Kristo mwenyewe, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu na Baba, Mwanao alipopaa mbinguni, aliwaahidia mitume Roho Mtakatifu. Walipokea neema nyingi za hekima kutoka mbinguni: tunakuomba utujalie na sisi karama za Roho wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.