Generic placeholder image

JUMAMOSI JUMA LA 7 PASAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bwana Mungu na wa vyote Muumba,
Ulimwengu nawe wategemezwa.
Vyote hubadilika na kuoza,
Wewe hapana, wabaki ni Mpya.

Ndiwe faraja na ya mtu kinga,
U Mwamba juu yake wa kujenga.
Ndiwe makao tulivu ya roho,
Yote hutimilika ndani yako.

Asifiwe Baba na Mwana Mungu,
Asifiwe Roho Mtakatifu;.
Na utukuzwe Utatu milele,
Nguvu yetu maisha yetu yote.

ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya

Zab.119:121-128 XVI Utii kwa sheria ya Mungu
Nimefanya mambo mema na maadilifu;*
usiniache katika makucha ya adui zangu.

Uahidi kunisaidia mimi mtumishi wako;*
usikubali wenye kiburi wanidhulumu.

Macho yangu yamechoka kungojea msaada wako,*
kungojea ukombozi ulioahidi.

Unitendee mimi mtumishi wako*
kadiri ya upendo wako mkuu, unifundishe amri zako.

Mimi ni mtumishi wako, unipe maarifa,*
nipate kujua mafundisho yako.

Ee Mungu, sasa ni wakati wa kufanya kitu,*
kwa maana watu wanavunja sheria yako.

Naam, nayapenda maagizo yako,*
kuliko hata dhahabu safi kabisa.

Kwa hiyo nafuata amri zako zote;*
kila njia potovu naichukia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.34 Sifa kwa wema wa Mungu
Mmeonja na kuona kuwa Bwana ni mwenye fadhili (1Pet.2:3)

I
Nitamtukuza Mungu nyakati zote,*
sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.

Nitamwonea Mungu fahari,*
wanaodhulumiwa wasikie na wafurahi.

Mtukuzeni Mungu pamoja nami,*
sote pamoja tulisifu jina lake.

Nilimwomba Mungu, naye akanisikiliza,*
akaniondolea hofu zangu zote.

Mgeukieni Mungu, mpate kufurahi;*
hamtapata kamwe kusikitika.

Maskini alimlilia Mungu, naye akamsikiliza,*
na kumwokoa katika shida zake zote.

Malaika wa Mungu huwalinda wote wamchao,*
na kuwaokoa katika hatari.

Jioneeni wenyewe jinsi Mungu alivyo mwema.*
Heri wanaokimbilia usalama kwake.

Mcheni Mungu, enyi watakatifu wake;*
wenye kumcha hawakosi mahitaji yao.

Hata simba huona njaa kwa kutindikiwa;*
bali wanaomtii Mungu wana kila kitu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

II
Njoni, enyi vijana, mkanisikilize,*
nami nitawafundisheni kumcha Mungu.

Je, wapenda kufurahia maisha;*
kuishi maisha marefu na ya fanaka?

Basi, acha kusema mabaya;*
achana na hila.

Jiepushe na uovu, utende mema;*
tafuta amani na kuizingatia.

Mungu huwaangalia waadilifu,*
na kusikiliza malalamiko yao;

lakini huwapinga watendao mabaya,*
awaondoa duniani, wasahauliwa kabisa.

Waadilifu wakimlilia Mungu, huwasikiliza,*
na kuwaokoa katika taabu zao zote.

Mungu yu karibu na waliovunjika moyo;*
huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.

Mateso ya mwadilifu ni mengi,*
lakini Mungu humwokoa katika yote.

Mungu humlinda mtu mwadilifu,*
hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.

Ubaya utawaangamiza watu waovu;*
wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.

Mungu atawaokoa watu wake, *
wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Rom.5:10-11
Tulipokuwa bado adui zake, Mungu alitupatanisha naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa tumepatanishwa naye, ni dhahiri zaidi kwamba tutaokolewa kwa uzima wa Kristo. Wala si hayo tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ametupatanisha na Mungu.

K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: 1Kor.15:20-22
Ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka wafu, na ni uthibitisho kwamba wale waliolala katika kifo watafufuliwa. Maana, kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo hivyo nako kufufuka katika wafu kumesababishwa na mtu mmoja. Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo.

K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 2Kor.5:14-15
Mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake. Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi tena kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao.

K. Kaa nasi, Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, utupatie neema ili tuweze kuzingatia, katika maisha na mwenendo, fumbo tuliloadhimisha Pasaka. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.