JUMAMOSI JUMA LA 7 PASAKA
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo Bwana ametuahidia Roho Mtakatifu: njooni, tumwabudu, aleluya.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.
Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.
Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.
Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.
Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.
Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.
Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.
2 (33)
Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.
E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!
Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.
Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.
Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.
Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.
Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.
3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;
Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;
Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.
Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal
4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.
Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.
Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.
Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434
5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.
Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.
Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930
ANT. I: Maneno niliyowaambieni ni ya uzima, aleluya.
Zab.119:145-152 XIX Kuomba usalama
Nakulilia kwa moyo wangu wote;/
unisikilize, Ee Mungu,*
nami nitazishika kanuni zako.
Nakusifu mara saba kila siku,*
nipate kuyashika mafundisho yako.
Asubuhi na mapema naamka niombe msaada;*
nitaitumainia kabisa ahadi yako.
Nakaa macho usiku kucha,*
ili niyatafakari maagizo yako.
Kwa upendo wako mkuu, Ee Mungu, unisikilize;*
uoneshe huruma yako, ukanisalimishe.
Wadhalimu wangu wakatili wanakaribia,*
watu ambao hawaishiki kamwe sheria yako.
Lakini wewe u karibu nami, Ee Mungu,*
na maagizo yako yote ni ya kuaminika.
Tangu zamani nimejifunza maagizo yako;*
wewe umeyaweka yadumu hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Maneno niliyowaambieni ni ya uzima, aleluya.
ANT. II: Bwana, umejenga hekalu lako na altare yako katika mlima
wako mtakatifu, aleluya.
WIMBO: Hek.9:1-6,9-11 Ee Bwana, unijalie hekima
Nitawapeni hekima na uwezo wa kusema hivyo kwamba maadui wenu hawataweza kustahimili
wala kupinga (Lk.21:15)
Ee Mungu wa baba zetu,/
BWANA, mwenye kuihifadhi rehema yako,*
umevifanya vitu vyote kwa neno lako;
na kwa hekima yako ukamwumba mwanadamu,*
ili avitawale viumbe vilivyoumbwa nawe,
na kumiliki ulimwengu katika utakatifu na kwa haki,*
na kutoa hukumu kwa unyofu wa moyo.
Nakusihi unipe Hekima,/
ambayo huketi karibu nawe*
katika kiti chako cha enzi,
wala usinikatae mimi*
miongoni mwa watumishi wako.
Mimi niliye mtumwa wako,*
na mwana wa mjakazi wako,
mtu dhaifu asiye na siku nyingi,*
wala sina nguvu kufahamu hukumu na sheria.
Kwa maana mtu ajapokuwa ni mkamilifu*
miongoni mwa wanadamu,
pasipo Hekima itokayo kwako*
atahesabiwa kuwa si kitu.
Na pamoja nawe hukaa Hekima,*
ijuayo matendo yako,
ikawapo hapo ulipoumba ulimwengu,/
ikayatambua yakupendezayo*
na yaliyo mema sawasawa na amri zako.
Uipeleke kutoka mbingu takatifu,*
na kutoka kwa kiti chako kitukufu,
ili ikae nami na kutenda kazi pamoja nami,*
nijifunze yale yakupendezayo.
Kwa maana huyajua mambo yote*
na kuyafahamu;
na katika kutenda kwangu/
itaniongoza kwa njia za kiasi,*
na kunilinda katika utukufu wake.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. II: Bwana, umejenga hekalu lako na altare yako katika mlima
wako mtakatifu, aleluya.
ANT. III: Mimi ndio Njia, Ukweli na Uzima, aleluya.
Zab.117 Kumsifu Mungu
Nawaambieni,.. nao watu wa mataifa mengine wamtukuze Mungu kwa sababu ya
huruma yake (Rom.15:8-9)
Enyi mataifa yote, msifuni Mungu!*
Enyi watu wote, msifuni!
Upendo wake mkuu kwetu ni thabiti;*
na uaminifu wake wadumu milele!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Mimi ndio Njia, Ukweli na Uzima, aleluya.
SOMO: Rom.14:7-9
Hakuna mtu ye yote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa
ajili yake mwenyewe; maana tukiishi, twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya
Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana. Maana Kristo alikufa, akafufuka
ili apate kuwa Bwana wa wazima na wafu.
KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Tazameni, mimi nipo nanyi siku zote, hata mwisho wa ulimwengu, aleluya.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Tazameni, mimi nipo nanyi siku zote, hata mwisho wa ulimwengu,
aleluya.
MAOMBI
Tukiwa tumeimarishwa na Roho Mtakatifu, na tuungane na wote waliobatizwa katika kumtukuza Bwana.
W. Bwana Yesu, ututakatifuze kwa Roho wako.
Ututie Roho Mtakatifu akilini na mioyoni mwetu;
- utuwezeshe kutangaza mbele ya watu wote kuwa wewe ni mfalme na Bwana. (W.)
Utujalie upendo wa kweli;
- utuwezeshe kuheshimiana na kupendana kwa dhati. (W.)
Uifanye upya mioyo ya waamini kwa neema yako itiayo uzima;
- uwawezeshe waamini hao kupokea na kuzitumia kwa furaha karama za Roho Mtakatifu. (W.)
Utujalie nguvu ya Roho Mtakatifu, ili tuweze kurekebisha maisha yetu yaliyopotoka;
- tunaomba Roho akiwezeshe kile kilichooza kuchipua na kukua. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Kwa mara nyingine tena, tumtukuze na kumwomba Baba kwa
maneno ya Kristo mwenyewe, tukisema: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Mwenyezi, utupatie neema ili tuweze kuzingatia, katika maisha na mwenendo, fumbo
tuliloadhimisha Pasaka. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi
na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.