JUMAMOSI JUMA 7 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Yak.5:13-20
Mtu wa kwenu amepatika na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa Imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi akaomba kwa bidii mvua isinye; na mvua haikunya juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake. Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.141:1-3,8(K)2
1. Ee Bwana, nimekuita, unijie hima,
Uisikie sauti yangu nikuitapo.
Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba,
Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.

(K) Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba.

2. Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu,
Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.
Macho yangu yanakuelekea Wewe, Mungu Bwana,
Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu. (K)

SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya!
Neno lako ndiyo kweli, ee Bwana,
ututakase kwa ile kweli.
Aleluya!

INJILI: Mk.10:13-16
Makutano walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukuzwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, uliyemwumba mwanadamu kwa sura na mfano wako na kumpa amri juu ya vitu vyote duniani, twakuomba.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie viongozi wanaolihudumia Kanisa badala ya Mwanao, Yesu Kristo, kuonesha adhama ya kazi yake na kulihimidi jina lake takatifu. Ee Bwana.

2. Wote uliowajaza hekima na maarifa ya dunia hii wajaliwe kuvitumia vipaji hivyo kwa sifa na utukufu wako na kukijulisha kicho chako ulimwenguni. Ee Bwana.

3. Uwajalie wabatizwa wote kuiona enzi ya utukufu wako, kuisikia sauti yako yenye nguvu na kumtendea haki jirani. Ee Bwana.

4. Utuongezee moyo wa sala; na uwaimarishie wagonjwa imani katika uwezo wako wa kuponya roho na mwili kwa Sakramenti ya Mpako Mtakatifu. Ee Bwana.

5. Kwa maombezi ya Mama Bikira Maria, marehemu wetu wafikishwe mbele ya uso wako mtukufu. Ee Bwana.

Ee Baba mwema unayetaka tuukubali ufalme wako kama watoto wadogo, upokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.